Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Salma Ali Hassan akisoma tamko la Tume wakati wa mkutano na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es Salaam, leo maalum kwa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Juni 16, 2016. Kulia ni Kamishna wa Tume, Mhe. Dkt. Kelvin Mandopi na Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa Tume, Francis Nzuki.
************************************************
Tamko la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Wakati
wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16, 2016
Tunapoadhimisha
kumbukumbu ya siku ya mtoto wa Afrika hii leo Juni 16, 2016 ikiwa ni mara ya 26
tangu uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) uizindue siku hiyo mwaka
1991, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), inatoa wito kwa umma, Serikali
na wadau mbalimbali wa haki za watoto kuunganisha nguvu kupinga vitendo vyote
vya ukatili wanavyofanyiwa watoto mahali popote Tanzania.
Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora inasikitishwa na kukerwa na matukio ya ukatili wa aina
mbalimbali wanayofanyiwa watoto ambayo yamekuwa yakiripotiwa na vyombo vya
habari. Matukio hayo yanajumuisha: kutupwa kwa watoto wachanga, ubakaji, ulawiti,
ukeketaji, mauaji, na watoto wa kike kuozwa katika umri mdogo, hivyo kuwanyima
haki zao, hususan haki ya kupata elimu. Matendo haya yenye kuvunja haki za
watoto yanafanywa na watu wazima wenye akili timamu.
Tume inalaani kwa
nguvu zake zote ukatili wa aina yoyote wanaofanyiwa watoto. Hivyo inawataka wananchi
kuhakikisha kuwa watoto wote nchini wanapewa malezi na makuzi stahiki katika
familia na jamii. Pia wanalindwa dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na wanapata
fursa katika maendeleo ya ustawi wao.
Hatua hii ni
muhimu kwani maendeleo ya Taifa lolote duniani yanawategemea watoto. Sensa ya
Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 imeonyesha kuwa idadi ya watoto nchini Tanzania ni zaidi ya
asilimia 50 ya watu wote. Kwa hiyo, jukumu la kuwalinda watoto dhidi ya vitendo
vya kikatili na kuwapa fursa ya maendeleo ya ustawi wao halina mjadala. Jukumu
hili ni la kila mmoja wetu ikiwemo familia, jamii na Serikali.
Tume inasisitiza kwamba binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa na
kwamba kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake. Haki
hii ya usawa inatambuliwa katika ibara ya 12 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ya mwaka 1977 na mikataba ya haki za binadamu ya Umoja wa Afrika (AU)
na kimataifa.
Nchi yetu imesaini na kuridhia mikataba hii ya kimataifa na kikanda na
kutunga sheria mbalimbali za kuharamisha makosa ya ukatili dhidi ya binadamu.
Miongoni mwa sheria hizi ni Sheria ya Mtoto, Sheria ya Kanuni za Adhabu,
Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na
Sheria ya Makosa ya Kujamiiana.
Hivyo, vitendo vya ukatili vikiwemo vitendo vya ubakaji, ulawiti, na ndoa
za utotoni, haviwezi kuendelea kutendeka huku Serikali, wananchi na wadau wa
haki za binadamu wakitazama bila kuchukua hatua.
Ni wajibu wetu sote, kuchukua hatua stahiki kuwalinda watoto; na Serikali
kupitia vyombo vyake iendelee kushughulikia kesi za watoto kwa haraka zaidi.
Katika kuyapa
kipaumbele masuala ya watoto mwaka 2007 Tume ilianzisha dawati maalum kwa ajili
ya kushughulikia masuala ya watoto nchini, yakiwemo malalamiko mbalimbali ya
uvunjwaji wa haki za watoto.
Katika kufuatilia
malalamiko ya watoto hasa yanayohusu ulawiti na ubakaji, Tume imebaini changamoto mbalimbali, zikiwemo: upelelezi wa
kesi hizi kuchukuwa muda mrefu, jamii kutokuwa na hamasa ya kupinga vitendo vya
ubakaji na ulawiti, na kutowapeleka watoto hospitali mara inapogundulika
wametendewa unyama huo, jambo ambalo hupoteza ushahidi.
Aidha, wahusika huwatishia
maisha watoa taarifa, na wakati mwingine kwa kuwa matukio mengi yanawahusisha
wanafamilia au watu wa karibu, hivyo ndugu hao hukaa na kusuluhishana nje ya
mahakama.
Changamoto
nyingine ni baadhi ya madaktari kutotoa ushirikiano wa kutosha katika mashauri
haya, na ucheleweshwaji katika kusikiliza kesi hizi.
Hivyo basi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inatoa mapendekezo
yafuatayo:
1.
Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto kuyapa kipaumbele
mashauri yanayohusu ubakaji na ulawiti wa Watoto, kufanya upelelezi thabiti na kuwakamata
wahusika, na kuwafikisha mahakamani kujibu mashtaka.
2.
Madaktari katika hospitali mbalimbali kuyapa kipaumbele matukio ya ulawiti
na ubakaji na kuwasaidia wahanga wa vitendo hivyo, hasa katika kutoa ushahidi
mahakamani.
3.
Mahakama ziharakishe usikilizaji wa kesi za ubakaji na ulawiti na kutoa
hukumu kwa wakati.
4.
Wananchi, jamii, kamati za ulinzi na usalama kwa ujumla watoe ushirikiano kwenye
vyombo vya sheria kwa kutoa taarifa za matukio ya ukatili wa watoto kama vile
ndoa za utotoni, ubakaji na ulawiti wa watoto.
5.
Wazazi na walezi waache kuharibu mwenendo wa mashauri ya ubakaji na ulawiti
kwa kukubaliana na wabakaji nje ya vyombo vya sheria hivyo kupoteza ushahidi.
6.
Wazazi watakaobainika kulinda uhalifu kwa kutotoa taarifa wachukuliwe hatua
za kisheria.
7.
Wazazi na walezi wawe makini na mienendo ya watoto ili kubaini mabadiliko
ya kitabia.
8.
Wazazi/walezi wawe karibu na watoto na kujenga urafiki nao ili kuwafanya
waweze kutoa taarifa zozote zisizo za kawaida kwa urahisi.
9.
Wazazi/walezi wachunguze mahusiano ya mtoto na jamii ya nyumbani na nje ili
kubaini viashiria vya udhalilishaji wa watoto au vitendo vya ukatili na
kuvizuia kabla havijatokea.
UBAKAJI NA ULAWITI KWA WATOTO VINAEPUKIKA:
Chukua
hatua kumlinda mtoto!
Imetolewa na:
(SIGNED)
Salma Ali Hassan (Kamishna)
Kny. Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Juni 16, 2016
No comments:
Post a Comment