Na Zainab Nyamka, Dar
MKUU wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa klabu ya Yanga Jerry Muro ametangaza kurejea rasmi katika majukumu yake ya kikazi huku akiweka wazi mapungufu yaliyosababisha kufanya hivyo kwani hadi kufikia Julai 31 hakuwa amepatiwa nakala ya hukumu yake pamoja na kuainishiwa makosa yaliyosababisha kufungiwa kwake mwaka mmoja kutokujihusisha na kandanda.
Shirikisho la Soka Nchini (TFF) lilitoa hukumu hiyo baada ya kumkuta na hatia chini ya kamati ya nidhamu na maadili ila toka kutolewa kwa hukumu hiyo Muro hajawahi kupoikea taarifa au nakala yoyote yenye kuainisha makosa yake mpaka kufikia kufungiwa.
TFF ilimshtaki Muro na kumuita katika kikao cha kamati ya nidhamu na maadili huku hukumu yake ikionekana kusuasua kutolewa kwa takribani mwezi mzima na Mwenyekiti wa Yanga Yusuph Manji kumtaka kurejea kazini kwani hawajapata taarifa zake za kufungiwa mpaka sasa. Akizungumzia kuhusu jambo hilo, Muro amesema kuwa mbali na barua hata mwajiri wake hajapata nakala yoyote ya hukumu na kikubwa ni kwa shirikisho hilo kumtumia nakala ya hukumu yake ili kujia amefungiwa kwa kupitia kifungu kipi.
Amesema, nakala hiyo itamsaidia kujua kipi afanye au kifungu kipi kitamuwezesha kukata rufaa ya hukumu hiyo ya kufungiwa mwaka mzima. "Sijapinga hukumu ya TFF bali nilichokipata mimi ni barua ambayo haijaweka wazi nimehukumiwa kwa kupitia kifungu kipi na kanuni ipi itaniwezesha kukata rufaa", amesema Muro.
Muro amesema kuwa taarifa zinazosambazwa zikimuhusisha kuwa na ugomvi na baadhi ya watendaji wa Shirikisho hil hazina ukweli wowote ."Sina ugomvi wala mgogoro na mtu yeyote ndani ya shirikisho hilo na wote nimekuwa nikifanya nao kazi, taarifa hizo zinafaa kupuuzwa kwani zinalenga uchochezi”.

No comments:
Post a Comment