Habari za Punde

*MAKAMU WA RAIS MHE. SAMIA AHITIMISHA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA KIZIMKAZI ZANZIBAR

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Ndugu Idrisa Kitwana wakati wa kilele cha sherehe za siku ya Kimkazi (Kizimkaziday) kwenye kijiji cha Kizimkazi Mkunguni. 
Mashindano ya kuvuta kamba
Vijana wa Kiume wakishindana kukuna nazi ikiwa sehemu ya mashindano ya Siku ya Kizimkazi (Kizimkazi Day).
Wakina Mama wakishindana kufunga kamba kwenye kilele cha sherehe za Kizimkazi.
**************************************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewahimiza wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mapambano dhidi ya rushwa,ufisadi kama hatua ya kukomesha tabia hiyo ambayo inarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo 13-Aug-16 wakati anahitimisha kilele cha sikukuuu ya Kizimkazi katika kijiji cha Kizimkazi Mkunguni wilayani ya Kusini Unguja – Zanzibar ambaye yeye ni mwasisi wa sikukuu hiyo ambayo inatumiwa na wakazi wa maeneo hayo kufanya michezo mbalimbali ya jadi pamoja na kujadili na kuweka mipango na mikakati ya kujiletea maendeleo kwa ushirikiano na viongozi wao.

Makamu wa Rais amewahakikishia kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa watendaji wanaorudisha nyuma maendeleo ya wananchi ikiwemo ubadhirifu wa fedha za umma ili kukomesha tabia hiyo. 

Amesema kuwa ili wananchi waweze kupata maendeleo ya haraka ni muhimu wananchi wakaimarisha ushirikiano miongoni mwao katika kubaini changamoto zinazowakabili na kushirikiane na viongozi wao katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo. 
Makamu wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan amesema yeye kama kiongozi wa kwanza kupata wadhifa huo kutoka kwenye kijiji cha Kizimkazi - Zanzibar ataendelea kushirikiana wananchi hao kutatua matatizo yanayowakabili wananchi hao ikiwemo tatizo la upatikanaji wa maji. 
Makamu wa Rais pia amehimiza wananchi wa Kizimkazi kutafuta eneo haraka kwa ajili ya ujenzi wa shule ya awali ambayo bado ni tatizo kubwa katika eneo hilo ili aweza kuwasaidia katika ujenzi wake kama hatua ya kuondoa kero ya watoto kushindwa kupata elimu ya awali. 
Katika Risala maalum ya wananchi wa kijiji cha Kizimkazi na Katibu wa Sherehe hizo Said Ramadhani Mgeni kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wamewapongeza viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada wanazofanya za ukusanyaji wa mapato ya serikali na wamesema wanaimani kubwa kuwa fedha zinazopatikana zitatumika katika kuinua uchumi na kujenga ustawi wa Jamii bora wananchi. 
Wananchi hao wameahidi kuwa watadumisha na kuimarisha ushirikiano kati yao na serikali hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. 
Baadhi ya Viongozi wa wilaya na Mkoa wa Kusini Unguja waliopata nafasi ya kuzungumza katika hafla hiyo ya hutimisha sikukuu ya wakizimkazi wamewaomba wananchi kudumisha amani na utulivu katika maeneo yao. Katika kilele cha sherehe hizo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alikabidhi zawadi mbalimbali kwa washindi ambao walishiriki kwenye mashindano ya siku ya Kizimkazi zikiwemo fedha taslimu.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.