Habari za Punde

*VIKAO VYA KAMATI ZA BUNGE KUANZA AGOSTI 22 MJINI DODOMA

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUANZA KWA VIKAO VYA  KAMATI ZA BUNGE TAREHE 22 AGOSTI, 2016 MJINI DODOMA                                                                    _________  
Kamati za Kudumu za Bunge zitaanza kukutana tarehe 22 Agosti hadi tarehe 3 Septemba, 2016 Mjini Dodoma kutekeleza majukumu yake kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Nne wa Bunge uliopangwa kuanza tarehe 6 Septemba 2016.  Kufuatia ratiba hiyo ya shughuli za Kamati, Waheshiwa Wabunge wote wanapaswa kuwa wamewasili Mjini Dodoma ifikapo Jumapili tarehe 21 Agosti, 2016 tayari kwa kuanza vikao vya Kamati.  Katika kipindi hiki Kamati za Kudumu za Bunge zitakapokuwa zinakutana Mjini Dodoma, shughuli zitakazo tekelezwa na Kamati hizo ni pamoja na:- 
a) Uchambuzi wa Miswada ya Sheria Jumla ya miswada sita (6) ya Sheria ambayo imekwisha somwa kwa mara ya kwanza Bungeni itachambuliwa na Kamati  kama inavyojionesha kwenye kila Muswada kama ifuatavyo:   
i. Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari Na. 4 wa mwaka 2016, (Kamati ya Katiba na Sheria)  
ii. Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali  Na. 8 wa mwaka 2016 (Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii)  
iii. Muswada wa Sheria ya Wanataaluma ya Kemia Na. 1 wa mwaka 2016 (Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii)  
iv. Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini Na.5 wa mwaka 2016, (Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii)  
v. Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Na.2 wa mwaka 2016 (Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji)  
vi. Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Na 3 wa mwaka 2016. (Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji)  

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA BUNGE LA TANZANIA   
Simu: +255 022 2112065-7 Fax No. +255 022 2112538 E-mail:  info@bunge.go.tz     
                     Ofisi ya Bunge,                  S.L.P. 9133,   DAR ES SALAAM   
Uchambuzi huo wa miswada utaenda sambamba na mikutano ya kusikiliza maoni ya wadau katika baadhi ya Miswada.  
b) Uchambuzi wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali Aidha, Kamati mbili zinazoshughulikia masuala ya fedha za Umma ambazo ni Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zitafanya uchambuzi wa Taarifa ya Mdhibiti na Makaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyowasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge ambapo Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) itapokea na kujadili Taarifa ya Hesabu za Serikali Kuu na  Mashirika ya Umma zilizokaguliwa na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) itapokea na kujadili Taarifa ya Hesabu zilizokaguliwa za Serikali za Mitaa na Halmashauri.  
c) Uchambuzi wa Taarifa ya Msajili wa Hazina Vilevile, Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) itapokea na kujadili Taarifa ya Msajili wa Hazina kuhusu hali ya uwekezaji wa Mitaji ya Umma nchini.  
d) Kupokea na kujadili Taarifa za kawaida za Wizara na Taasisi za Serikali. Kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Wizara na Taasisi za Serikali Kamati nyingine za Kisekta zitapokea na kujadili taarifa za kawaida za Wizara na Taasisi za Serikali.  Kamati hizo ni pamoja na Kamati yaViwanda, Biashara na Mazingira, Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, Kamati ya Nishati na Madini, Kamati ya Masuala ya UKIMWI na Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.  
e) Uchambuzi wa Sheria Ndogo Pamoja na shughuli hizo, Kamati ya Sheria Ndogo pia inatarajia kufanya uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa wakati wa Mkutano wa Tatu wa Bunge na kupokea Taarifa ya utekelezaji wa maoni kuhusu Sheria Ndogo zilizochambuliwa Mwezi Machi, 2016.  
Aidha ratiba zote za Shughuli za Kamati za Bunge zinapatikana katika Tovuti ya Bunge ambayo ni www.parliament.go.tz  
Imetolewa na:  
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Ofisi ya Bunge DAR ES SALAAM  
18 Agosti, 2016. 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.