Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ajira
kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Robert
Masingiri akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu
Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini inayoratibiwa na Ofisi hiyo. Kushoto ni Afisa
Habari wa Ofisi hiyo Bw. Ridhiwani Wema.
Afisa Habari Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Ridhiwani Wema akiongea na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ajira kutoka Ofisi hiyo Bw. Robert Masingiri Picha na Fatma Salum-MAELEZO
**********************************************************
Na Fatma Salum – MAELEZO
Serikali imetoa wito kwa vijana kote
nchini kuchangamkia fursa ya kupata ujuzi wa fani mbalimbali kupitia Programu
ya Kukuza Ujuzi Nchini inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana,
Ajira na Wenye Ulemavu.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi
Msaidizi Huduma za Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu Bw. Robert Masingiri wakati akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam kuhusu programu hiyo.
Masingiri alibainisha kuwa programu
hiyo ni muhimu kwa vijana kwani itawawezesha kupata ujuzi na stadi stahiki ili
kumudu ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
“Utekelezaji wa programu hii ni hatua
za makusudi za Serikali za kukabiliana na kiwango kidogo cha ujuzi miongoni mwa
nguvu kazi ya Taifa.” Alisema Masingiri.
Aliongeza kuwa kiwango cha ujuzi
hakijafikia hatua nzuri ya kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati hivyo
Serikali imetenga shilingi bilioni 15 kwa ajili ya programu hiyo na utekelezaji
wake umeanza mwaka wa fedha 2015/2016 hadi 2020/2021
“Programu hii inalenga kuziba pengo
kubwa lililopo la ukosefu wa ujuzi katika sekta za utalii, ujenzi, viwanda,
nishati na madini ambapo utawawezesha vijana wengi kuajirika na kujiajiri.”
Alisema Masingiri.
Akifafanua kuhusu mfumo wa utekelezaji
wa programu hiyo, Afisa Habari kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Ridhiwani Wema
alisema kuwa programu hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali kwa
njia ya uanagenzi (apprenticeship) ambapo lengo ni kuwafunza vijana 3000 katika
viwanda vya nguo na vijana 1000 katika sekta ya ngozi.
Wema aliongeza kuwa program hiyo pia
inatekelezwa kupitia urasimishaji wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi
(Recognition of Prior Learning) na vijana 3900 watarasimishwa kupitia sekta ya
ujenzi, utalii na ukarimu.
Aidha kupitia program hiyo wahitimu
4000 watapata mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi na wafanyakazi 13400
watapatiwa mafunzo ya kuongeza ujuzi.
“Ofisi ya Waziri Mkuu imesaini
mikataba na VETA na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) ili watoe
ujuzi kwa vijana kote nchini na kupitia programu hiyo mafunzo hayo
yanagharamiwa na Serikali , hakuna malipo.” Alieleza Wema.
Serikali imejipanga kuendelea
kukamilisha miongozo ya ukuzaji ujuzi kwa njia mbalimbali itakayowezesha wadau
kushiriki katika utekelezaji wa Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini ili kufikia
sera ya kukuza viwanda na kujenga uchumi wa kati.
No comments:
Post a Comment