Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba (katikati) akiongea na waandishi wa habari juu ya Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na Ukame. Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa hazina Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Faustin Kamuzora na Bw. Timothy Mande Afisa Misitu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Katibu Mkuu Ofisi ya
Makamu wa Rais Prof. Faustin Kamuzora (kushoto) akifafanua jambo mbele ya
waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa utoaji wa tamko la kuadhimisha
siku ya kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame, mkutano huo umefanyika
leo katika ukumbi wa hazina Dodoma.
*******************************************
TAMKO LA MHESHIMIWA
JANUARY Y. MAKAMBA (MB), WAZIRI WA NCHI - OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA
MAZINGIRA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA KUPAMBANA
NA KUENEA KWA HALI YA JANGWA NA UKAME DUNIANI, TAREHE 17 JUNI, 2017
Ndugu Wananchi,
Mwaka 1994 Baraza la
Umoja wa Mataifa liliazimia na kuitangaza tarehe 17 mwezi Juni ya kila mwaka
kuwa ya maadhimisho ya siku ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame.
Kwa kutambua umuhimu wa kuadhimisha siku hii, tarehe 17 mwezi Juni kila mwaka,
duniani kote huadhimishwa Siku ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na
Ukame. Madhumuni ya kuadhimisha siku hii ni kukuza uelewa miongoni mwa jamii
juu ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na
Ukame na umuhimu wa utekelezaji wake duniani, hususan katika nchi
zilizoathirika zaidi na tatizo hili la kuenea kwa hali ya jangwa na ukame hasa katika
bara la Afrika. KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA
Ndugu Wananchi,
Tangu mwaka 1994
nchi zilizoridhia Mkataba wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame, Mashirika
ya Umoja wa Mataifa, Mashirika ya Kimataifa yasiyokuwa ya kiserikali pamoja na
wadau wengine, huadhimisha siku hii kwa kufanya shughuli kadhaa zinazohusu
kupambana na tatizo hili. Mkataba huu ndiyo mkataba pekee wa Umoja wa Mataifa unaolenga
kupambana na tatizo la uharibifu wa ardhi katika maeneo kame, na kufanya juhudi
za kuhifadhi na kuleta matumizi endelevu ya ardhi. Kwa kutambua umuhimu wa
Mkataba huu, Nchi zipatazo 193 ulimwenguni zimeridhia utekelezaji wake hadi
sasa. Ni wazi kuwa mkataba huu una umuhimu wa pekee kwa nchi kama Tanzania
ambayo uchumi wake unategemea ardhi kwa ajili ya kilimo ambacho kinatoa ajira
kwa wananchi wengi.
Ndugu Wananchi,
Kauli
mbiu ya mwaka huu katika kuadhimisha siku ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya
Jangwa na Ukame inasema “Ardhi ni Makazi yetu Tuitunze kwa Manufaa ya
baadaye” (‘Our Land, Our Home, Our Future’).
Kauli mbiu hii inayoadhimishwa mwaka huu ina malengo ya kuhamasisha jamii
kuitunza Ardhi kwa kuwa ndiyo makazi yetu hii ikiwa ni pamoja na kuongeza
juhudi zaidi kwa ajili ya manufaa ya baadaye kwetu sisi na vizazi vijavyo.
Malengo haya yanadhihirisha umuhimu wa utunzaji wa ardhi na udongo kwa ajili ya
matumizi endelevu hasa kuifanya iwe na uwezo wa kuzalisha mazao ya kilimo na mifugo
na kutoa huduma zingine muhimu kama vile utalii wa wanyamapori, uwindaji, miti,
vyanzo vya maji na uwekezaji wa viwanda ili kuleta ustawi wa jamii kwa vizazi vya
sasa na vijavyo. Hali ya uharibifu wa mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji
inaongezeka kwa kasi na hivyo kuongezeka kwa tatizo la ukame, upungufu wa mazao
ya kilimo na kupungua kwa chakula mara kwa mara na kuongezeka kwa umasikini
miongoni mwa jamii. Ukataji wa miti kiholela na uharibifu wa misitu
unaosababishwa na utegemezi mkubwa wa binadamu wa kupata mahitaji kutokana na
mazao ya misitu pamoja na huduma zingine muhimu, kunazidisha ukubwa wa tatizo
hili. Makazi, Mikakati na program zote muhimu za maendeleo ya nchi hufanyika kwa
kutumia ardhi.
Ndugu Wananchi,
Nchi yetu inakabiliwa kwa kiasi
kikubwa na hali ya kuenea kwa jangwa na ukame. Takwimu zinaonyesha kuwa takriban
asilimia sitini na moja (61) ya eneo la nchi liko katika hatari ya kugeuka
jangwa. Miongoni mwa mikoa ambayo imeathirika zaidi ni pamoja na Singida,
Dodoma, Shinyanga, Manyara, Simiyu, Geita
na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Arusha. Tayari madhara mbalimbali ya
kuenea kwa hali ya jangwa na ukame yameanza kuonekana ikiwa ni pamoja na
kukauka kwa vyanzo vya maji katika maeneo mbalimbali, vifo vya mifugo na
wanyama pori, upungufu wa mvua kutokana na ukataji wa miti kiholela, migogoro
baina ya wafugaji na wakulima kutokana na kupungua kwa maeneo ya kilimo na
malisho ya mifugo.
Ndugu Wananchi,
Kuenea kwa hali ya jangwa na ukame
kuna madhara makubwa sana katika uchumi wa taifa letu. Kama inavyoeleweka asilimia
themanini (80) ya Watanzania inategemea kilimo ambacho kwa kiwango kikubwa kinategemea mvua. Kutokana na kuenea kwa hali
ya jangwa na ukame ni dhahiri kuwa uzalishaji wa mazao unapungua kwa kiasi
kikubwa. Hali hii inachangia kuathiri kushuka kwa uchumi hasa unaotegemea uuzaji wa mazao ya chakula
na biashara. Hali hii itapunguza pia upatikanaji wa kipato katika ngazi ya kaya
na ngazi ya taifa kiujumla. Kuenea kwa hali ya jangwa na ukame pia kunasababisha
upotevu wa rasilimali zingine kama misitu, vifo vya wanyama pori ambao ni
chanzo kikubwa cha fedha za kigeni kupitia utalii. Aidha, kuenea kwa hali ya
jangwa na ukame kunasababisha tabaka la juu la ardhi kuwa wazi na hivyo kutoa
nafasi kwa mmomonyoko wa udongo kwa njia ya maji na upepo. Hali hii inasababisha
kupungua kwa rutuba katika udongo na hivyo kupunguza uzalishaji wa mazao kwa
kiasi kikubwa.
Ndugu Wananchi
Ili kupambana na hali ya kuenea kwa
jangwa na ukame serikali imechukua hatua mbalimbali. Hatua hizo ni pamoja
kuandaa taarifa ya hali ya kuenea kwa jangwa na ukame (Status of Land
Degradation) ya mwaka 2014; Mpango kazi wa Kitaifa wa Kupambana na kuenea kwa
hali ya jangwa na ukame (National Action Program to Combat Desertification) ya
mwaka 2014-2018. Taarifa na Mpango kazi huu vimetoa maelekezo mbalimbali kwa
mamlaka husika, maelekezo ambayo utekelezaji wake ni wa muda mfupi, muda wa
kati na muda mrefu. Maelekezo haya ni pamoja na programu za upandaji miti,
kuandaa mpango wa matumizi bora wa ardhi, kulima kilimo kinachofuata njia za
kisasa, ufugaji bora na wa kisasa, kuanzisha maeneo ya hifadhi na kuyalinda
yale yaliyopo, kusisitiza matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza utegemezi
wa kuni na mkaa, kuendeleza njia bora kuhifadhi maji na uvunaji wa maji hasa
kipindi cha mvua na kuelekeza wananchi kuwa na shughuli zingine za uzalishaji
mali (Other income generating activities) ili kupunguza utegemezi katika
maliasili. Kwa mfano, programu ya
kitaifa ya upandaji miti ya mwaka 2016 hadi 2021 inalenga kupanda miti zaidi ya
milioni 280 kila mwaka na inalenga hasa
maeneo yaliyo katika hatari za kukabiliwa na hali ya jangwa na ukame.
Ndugu Wananchi,
Ili kukabiliana na tatizo
hili na kwa ajili ya kutunza na kuhifadhi maliasili, Serikali imeandaa Mkakati wa
Taifa wa Kupanda na Kutunza miti wa mwaka 2016 – 2021. Mkakati huu unalenga
kupunguza kasi ya uharibifu wa ardhi kwa njia ya kupanda na kutunza miti na
kuhakikisha kwamba kila mwananchi anahusika katika utaratibu huu. Aidha, pamoja
na mambo mengine, Mkakati wa kupambana na ukame na Jangwa na mikakati mingine
ya Mazingira inaendelea kutekelezwa. Pia serikali inaandaa mkakati wa kupunguza
matumizi ya nishati ya Mkaa itokanayo na miti ya misitu ya asili. Kuongeza
juhudi za matumizi ya Usimamizi Endelevu wa Ardhi. Kufanya Tathmini za Athari
kwa Mazingira na Tathmini za Mazingira Kimkakati. Malengo yote haya ni kutaka
kufikiwa wadau wote na endapo wadau wote katika sekta ya mbalimbali watahusika
katika utunzaji wa mazingira na matumizi endelevu ya Ardhi malengo ya baadaye
yatafikiwa.
Ndugu Wananchi;
Matumizi
endelevu ya Ardhi, Kupanda na kutunza Miti ni mojawapo ya mikakati inayoweka ulinganifu
katika shughuli za kilimo, ufugaji, misitu, uhifadhi wa vyanzo vya maji na
kuhakikisha kuwa mifumo ya ikolojia inayotegemeana haiingiliwi. Juhudi hizi
zitasaidia katika utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na
Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame (UNCCD) kwa kuhakikisha kwamba Mpango wa
Taifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame (NAP) 2014 unakuwa
nyenzo muhimu ya kuongeza uzalishaji katika kilimo; kuondokana na tatizo la uharibifu
wa ardhi; kuongoa maeneo yaliyoharibika na kurejesha misitu katika maeneo ya
nyanda kame; na hivyo kupunguza umasikini.
Ndugu Wananchi,
Ninaomba
kutoa rai kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kutekeleza kauli mbiu
ya mwaka huu 2017 ya siku ya kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame ili
kuhakikisha ardhi yetu inatunzwa, ardhi iliyoharibika imeongolewa, kwa ajili ya
kizazi cha sasa na vizazi vijavyo. Hii inawezekana `ikiwa kila mmoja wetu atashiriki
kikamilifu katika eneo Lake.
Asanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment