Hussein
Makame-NEC
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Athumani
Kihamia amesema Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Buyungu ataendelea kutekeleza
majukumu yake kwa kuwa malalamiko yaliyotolewa na Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) ya kumkataa msimamizi huyo hayakufuata taratibu za kisheria.
Akitoa ufafanuzi huo jijini Dar es Salaam leo, Dkt. Kihamia alisema kuwa
kwa mujibu wa Kifungu cha 7 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343,
malalamiko hayo hayana msingi wa kisheria kwa sababu hayakuja kama rufaa ila
yametolewa kama malalamiko.
“Kwa maana hiyo napenda kuwajulisha umma kwamba malalamiko haya
hayamuondolei sifa Msimamizi wa Uchaguzi kwa kumuondoa kusimamia shughuli za
Uchaguzi katika Jimbo la Buyungu” alisema Dkt. Kihamia na kuongeza:
“Kwa kuwa Chadema
kimelalamika kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na malalamiko hayo wameyaleta kama
barua, kwa kuwa kuna Kamati ya Maadili ngazi ya Taifa, malalamiko hayo
yalipaswa yaletwe ndani ya muda unaokubalika ambayo ni saa 48 tangu kupokea
hizo taarifa’.
Alisema majibu haya yametokana kwa jinsi Tume ilivyochunguza upande
unaolalamikiwa na kujiridhisha ingawa, alisema Tume itaendelea kufuatilia kwa
karibu kuona kila kitu kinakwenda vizuri na kwamba hakuna jambo linaloweza
kuharibu Uchaguzi.
Dkt. Kihamia alikihasa Chadema kuwa kama kuna kasoro zingine zozote
ndogo ndogo ambazo zinaweza kutatulika kwa njia ya kawaida Tume itatekeleza
majukumu yake katika kasoro hizo.
Akitaja malalamiko ya Chadema, Dkt. Kihamia alisema Chadema kupitia Katibu
Mkuu wake, kiliandika barua Tume kikimlalamikia Msimamizi wa Uchaguzi kwamba ratiba
ya mtiririko wa Uchaguzi haikutolewa.
“Baada ya kupokea malalamiko hayo tulijiridhisha na kugundua kuwa
Msimamizi wa Uchaguzi katika Jimbo hilo alikutana na vyama tarehe 7 Julai, 2018
na vyama vilipokea ratibu ya shughuli za uchaguzi wa jimbo hilo siku hiyo na
vingine vilipokea tarehe 10 Julai, 2018”, alisema Dkt. Kihamia.
Alitaja madai mingine kwamba orodha ya wasimamizi wa vituo vya kupigia kura
haikutolewa, na kueleza kuwa ushahidi ilionao Tume unaonesha kuwa orodha hiyo
ilitolewa tarehe 5 na 6 Julai, 2018 na siku ya mwisho ya kutoa ilikuwa tarehe
31 Julai, 2018.
“Hoja ya tatu ni kwamba viapo vya mawakala havikutolewa kwa
wakati.Taarifa rasmi inaonesha viapo vilitolewa siku saba kabla ya siku ya
Uchaguzi na vimezingatia matakwa ya Sheria kwa kuwa vilitolewa tarehe 5 Agosti
na Uchaguzi ni tarehe 12 Agosti mwaka huu”, alibainisha Dkt. Kihamia.
Kuhusu hoja ya nne iliyotolewa na Chadema kwamba Msimamizi wa Uchaguzi
hakuonesha sehemu ambapo kura zanatakiwa kujumlishwa, Dkt. Kihamia alisema
uchaguzi ni Agosti 12, 2018 taarifa hiyo inakiwa kutolewa isizidi siku ya
tarehe 11 Agosti, 2018 ambapo tarehe hiyo bado haijafika.
Alisema kuwa Tume inaamini kuwa muda wowote taarifa hizo zitatolewa na
pia kwa kuwa haijasikia malalamiko kutoka vyama vingine tisa vinavyoshiriki uchaguzi
katika jimbio la Buyungu, inawezekana Chadema mawasiliano hayakuwa mazuri ndani
ya chama hicho.
Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Buyungu na kata 77 unatarajiwa
kufanyika Agosti 12 mwaka huu huku Uchaguzi katika baadhi ya kata wagombea wake
wakitangazwa kupata bila kupingwa.
No comments:
Post a Comment