Mwenyekiti wa kikundi cha Pwani Generation Qeens Bety Msimbe kulia akimkabidhi msaada wa vifaa mbali mbali mmoja wa wakinamama Zulfa Athumani katika halfa fupi kwa niaba ya wengine baada ya kujifungua katika kituo cha afya chalinze kilichopo Wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Baadhi ya viongozi na wanachama wa kikundi cha Pwani Generation Qeens wakiwa ndani ya kituo cha afya chalinze ambapo walifanya ziara ya kuwatembelea wagonjwa na kutoa msaada wa vifaa mbali mbali kwa ajili ya kuwasaidia wakinamama wajawazito pamoja na watoto.
Kikundi cha Pwani Generation Qeens kikiwa katika picha ya pamoja nje ya wodi ya wazazi katika kituo cha afya chalinze mara baada ya kumaliza kutoa msaada wa vifaa mbali mbali kwa wanawake wajawazito na watoto.
********************************
VICTOR MASANGU, CHALINZE
KATIKA kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kupunguza vifo vya wakinamama wajawazito pamoja na watoto wachanga kikundi cha Pwani Generation Qeens kimetoa msaada wa vifaa mbali tiba mbali katika kituo cha afya Chalinze kilichopo Wilayani Bagamoyo mkoani Pwani kwa lengo la kusaidia kutatua changamoto ambayo ilikuwa inawakabili wanawake wakati wa kujifungua.
Akikabidhi msaada wa vifaa tiba mbali mbali katika kituo hicho cha afya Mwenyekiti wa kikundi cha Pwani Generation Qeens Bety Msimbe alisema kwamba wameamua kutoa msaada katika wodi ya wazazi kutokana na kubaini kuwepo kwa uhaba wa vifaa tiba hasa kwa wanawake wajawazito ambao wanakwenda kupatiwa matibabu.
Aidha Msimbe alisema kwamba kumekuwepo na baadhi ya wanawake ambao wamekuwa wakipata shida sana pindi wanapokwenda katika zahanati, vituo vya afya pamoja na hospitali kwa ajili ya kujifungua hivyo wakaona kuna umuhimu wa kutoa msaada huo ambao utawasaidia wakinamma wajawazito, waliojifungua pamoja na watoto wachanga.
Nao baadhi ya wanawake ambao wamenufaika na msaada huo akiwemo Demertia Milichadesi pamoja na Mariam Muhoja walisema kwamba ni kweli wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa kwa ajili ya kujifungulia na wakati mwingine inawalazimu kwenda dukani kununua ukizingatia baadhi yao uwezo wao wa kifedha ni mdogo hivyo wanashindwa kumudu gharama za matibabu.
“Kwa kweli kwa upande wetu kama wanawake tumefarijika sana na msaada huu kutoka katika kikundi cha Pwani Generation Qeens maana changamoto yetu ilikuwa ni vifaa tiba pamoja na mahitaji mbali mbali hasa wakati wa kujifungua maana wakati mwingine tunajikuta tunakosa vifaa muhimu na wakati mwingine tunanunua,”walisema.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa kituo cha afya chalinze Salama Masukuzi
amebainisha kwamba changamoto zinazowakabili kwa sasa ni kuwepo kwa mlundikano mkubwa wa wagonjwa kutokana na kuwepo kwa upungufu wa majengo ya wodi za wazazi pamoja na vitanda na kupelekea wakati mwingine wagonjwa kuwalaza wawili katika kitanda kimoja.
Aidha alisema kwamba pamoja na kukabiliwa na changamoto hizo pia kuna upungufu wa madaktari pamoja na wauguzi hivyo kupelekea kufanya kazi katika mazingira magumu kutokana na kupokea idadi kubwa ya wagonjwa hivyo ameiomba serikali kuwaboreshea zaidi huduma ya afya kwa ajili ya kuweza kutoa huduma nzuri kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment