Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, akizungumza na waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, wakati akitangaza kuanza kutumia Helkopta kuimarisha Ulinzi kwa wageni wa Mkutano wa Viongozi Wakuu wa SADC.
*Vyombo vya moto 126 vyakamatwa kwa kukiuka sheria elekezi zipo pikipiki, bajaji na magari yenye ving'ora na taa sumbufu
*******************************
Na Ripota wa Mafoto Blog, Dar
KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa, amesema kuwa jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha wageni wote wanaoingia nchini wanakuwa salama katika kipindi chote kuanzia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, Hoteli watakazofikia na wawapo katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mambosasa amesema kuwa ili kuongeza ulinzi na usalama wa raia na wageni wa Mkutano wa SADC Jeshi la Polisi limejipanga kuanza kutumia Helkopta kuanzia kesho ili kuimarisha ulinzi kila kona ya Jiji la Dar es Salaam.
"Msako na doria wa askari watumiao magari, pikipiki, mbwa, farasi, na watembeao kwa miguu unaendelea katika kila kona za jiji la Dar es Salaam na kuanzia kesho helkopta zitatumika katika kuimarisha ulinzi na usalama ndani ya jiji la Dar es Salaam" amesema Mambosasa.
Aidha Mambosasa amesema kuwa baada ya kuzuia pikipiki, magari yenye ving'ora na gari zenye rangi za taa sumbufu na bajaji kutoingia katikati ya jiji bado kuna watu wameendelea kukiuka agizo hilo ambapo hadi sasa jumla ya vyombo vya moto 126 vimekamatwa na vinashikiliwa na jeshi la polisi huku wamiliki wake waskishikiliwa kwa ajili ya sheria zinazofuata.
"Tuliweka zuio la baadhi ya vyombo vya moto kutoingia katikati ya jiji, lakini kuna baadhi wamekiuka hasa pikipiki (bodaboda) ambazo zimekuwa hazifuati sheria, wanabeba mishikikaki na hawavai kofia ngumu na kupitia msako uliofanywa na jeshi la polisi jumla ya vyombo vya moto 126 vimekamatwa vikihusisha pikipiki 87, bajaji 13 na magari yenye ving'ora na taa sumbufu barabani 26 na baadhi ya wahusika wanashikiliwa na watapelekwa mahakamani" amesma Mambosasa.
Mambosasa amewahakikishia wananchi na wageni usalama wa hali ya juu na bado wanaendelea na kazi ya kuhakikisha jiji hilo linaendelea kubaki salama salimini hata baada ya mkutano huo kumalizika
"Jiji lipo shwari kabisa tuna akiba ya askari zaidi ya 300 msako utaendelea na watakaojaribu kukaidi kile kinachoelekezwa na serikali pamoja na vyombo vya ulinzi watakutana na vyombo vya dola na ninazidi kuwahimiza wananchi kuzidi kuunga mkono jeshi la polisi hasa kwa kutoa taarifa za uharifu na waharifu kwa kuwa mafanikio yatakayotokana na mkutano huo ni yetu sote" amesema
Mwisho ameishukuru kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Paul Makonda, wakuu wa Wilaya, madiwani, wenyeviti wa mitaa, ulinzi shirikishi na wananchi kwa ujumla kwa ushirikiano wanaoonesha hasa katika kipindi hicho ambacho taifa linategemea kuupokea ugeni mzito kutoka mataifa 15.
No comments:
Post a Comment