NAIBU Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi
na Mawasiliano Mhandisi Atashanta Nditiye amesema Serikali ina mkakati wa
kupeleka Bungeni muswada wa ya kulinda taarifa binafsi za mtu lengo likiwa ni
kulinda mawasiliano binafsi na udukuzi.
Mhandisi Nditiye ameyasema hayo
leo Agosti 14 , 2019 wakati anazungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa
Mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam alipokuwa
akielezea mikakati ya wizara hiyo kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini
mwa Afrika(SADC).
Hivyo pamoja na kutoa maelezo ya
mikakati hiyo ya Wizara, Mhandisi Nditiye aliulizwa iwapo Wizara imeweka
mkakati wowote kudhibiti udukuzi wa kuingilia taarifa za mtu binafsi na namna ilivyojipanga
kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni.
“Matumizi sahihi ya mawasiliano
nchini bado yana changamoto na pamoja na juhudi zilizoweka kupambana na wote
wanaochafua wenzao kupitia mawasiliano.Tutapeleka muswada wa sheria bungeni
mwaka huu.
“Tunapambana na wote wanaochafua
wenzao kwa mawasiliano ya simu, Mamlaka yetu ya Mawasiliano (TCRA) kwa
kushirikiana na kitengo cha uhalifu wa mtandaoni (Cyber Crime) katika Wizara ya
Mambo ya Ndani, tunashirikiana katika hili,” amesisitiza Mhandisi Ndetiye.
Hata hivyo kwa mujibu wa Mhandisi
Ndetiye, amesema asilimia 98 ya mawasiliano ya ujanja ujanja wa kuunganisha
simu za kimataifa zimedhibitiwa nchini.
Ameongeza sekta ya mawasiliano ni mtambuka na imeendelea
kuchangia mapato ya Serikali kutoka asilimia 13.1 mwaka 2017 hadi asilimia 14.7
mwaka 2018 huku akieleza kipaumbele ni kuona inachangia zaidi.
Wakati huo huo Mhandisi Nditiye
amesema kwa sasa nchini Tanzania watumiaji wa simu wamefikia milioni 43.6 na wa
mtandao wa intaneti wamefikia watumiaji milioni 23.140.Hivyo sekta ya
mawasiliano ikitumika vizuri ni muhimili mkubwa wa maendeleo ya uchumi nchini.
Kwa upande wa malengo ya kikanda,
amesema nchi ya Tanzania inamkakati wa kuziunganisha nchi zote za jumuiya hiyo
kwenye Mkongo wa Taifa kwa lengo la kuhakikisha nchi hizo zinakuwa na uhakika
wa mawasiliano kwa ajili ya kuleta maendeleo.
Amefafanua tayari serikali ya
Tanzania imeziunganisha nchi mbili za Zambia na Msumbiji na nne za Jumuiya ya
Afrika Mashariki ambazo ni Uganda , Kenya, Burundi na Rwanda. “Mkakati uliopo
kupitia Mkongo wa Taifa tunampango wa kuzifikia nchi zote za SADC”.
No comments:
Post a Comment