MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa tahadhari ya kuwepo kwa mvua kubwa na mawimbi makubwa katika baadhi ya maeneo ya Kaskazini kwenye mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Kaskazini mwa Morogoro, Visiwa vya Unguja na Pemba.
Tahadhari hiyo imetolewa leo na TMA, ikionesha uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa mvua kubwa sambamba na mawimbi makubwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia leo Oktoba 9 hadi Oktoba 12, 2019.
Angalizo hilo la mawimbi Mmakubwa limetolewa pia kwa baadhi ya maeneo Pwani ya Bahari ya Hindi na kusini mwa mikoa ya Mtwara na Lindi.
Mamlaka hiyo imewataka watumiaji wa bahari na maeneo yaliyotajwa kuchukua tahadhari.
“Tahadhari ya upepo mkali na mawimbi makubwa imetolewa kwa maeneo ya ukanda wa pwani yote, katika mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Mtwara, Lindi, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo fupi.
Katika taarifa hiyo ya kifurushi cha siku nne cha tahadhari za hali ya hewa, TMA imeeleza athari kuwa kiwango kikubwa cha athari kinaweza kujitokeza.
TMA pia imeeleza athari zinazoweza kutokea ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, kutawanyishwa na ucheleweshwaji wa usafiri baharini na nchi kavu na kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii.
No comments:
Post a Comment