Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Laurance Mafuru (katikati) akipiga kengere kuashiria kufunga rasmi Hatifungani JASIRI ya Benki ya NMB, wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika Ofisi za Soko la Hisa la Dar es Salaam, leo. Wa pili (kushoto) ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, (kulia) ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Nicodemus Mkama (kushoto) ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko Hisa la Dar es Salaam (DSE) Moremi Marwa. .Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Laurance Mafuru, akisoma hotuba yake wakati wa hafla ya ufungaji rasmi wa Hatifungani JASIRI ya Benki ya NMB, iliyofanyika katika Ofisi za Soko la Hisa la Dar es Salaam.
********************************
BENKI ya NMB imefunga mauzo ya Hati Fungani ya Jasiri (NMB Jasiri Bond) kwa mafanikio makubwa yaliyoweka rekodi ya makusanyo Afrika Mashariki na Kati ya Sh. Bil. 74.27 na kuvuka lengo la Sh. Bil. 25, ufungaji ulioenda sambamba na kuiorodhesha rasmi hati hiyo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Hafla ya ufungaji huo iliyohudhuriwa na Wakurugenzi, Maafisa Watendaji Wakuu wa Taasisi Binafsi na Mashirika ya Umma, imefanyika jijini Dar es Salaam leo (Alhamisi Aprili 28), Mgeni Rasmi akiwa ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrance Mafuru, aliyemwakilisha Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Waziri huyo, Mafuru aliipongeza NMB kwa ubunifu chanya wa Jasiri Bond, hati fungani iliyolenga kukusanya fedha za kutanua wigo wa utoaji wa huduma za fedha kwa kampuni zinazoendeshwa na wanawake, sambamba na nyinginezo zinazotoa huduma zinazowagusa wanawake Tanzania.
“Hii sio mara ya kwanza kwa NMB kuja na Hati Fungani na kuvuka lengo la makusanyo, hii ni mara ya nne na kwa hati hii ambayo ni ya kipekee, kama jina lake lilivyo, kumekuwa na ujasiri mkubwa sana, kwani jina Jasiri linaashiria mambo mengi sana.
“Kwanza, ujasiri wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), ya kuiruhusu Hati Fungani hii kuingia sokoni kabla hata ya sheria zake hazijawa tayari, jambo linalothibitisha imani ya mamlaka hii kwa NMB ilivyokuwa kubwa.
“Pili, ni ujasiri wa NMB kubuni huduma inayowalenga wanawake, huu ni ujasiri wa kipekee kwa benki hii, kwani kundi hili la wanawake linaonekana ni dhaifu, ambalo halina nguvu za kiuchumi.
“Lakini NMB ikalenga kupata Sh. Bil. 25 na hatimaye inafunga mauzo ikiwa imepata zaidi ya mara tatu ya lengo, hii ni kuthibitisha kwamba kuna nguvu kubwa ya kiuchumi miongoni mwa wanawake, tunachotakiwa ni kuweka mazingira wezeshi ya kuwaamini kama wenzetu NMB walivyofanya,” alisisitiza Mafuru.
Aliwapongeza NMB kwa kubuni huduma zinazolenga kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha huduma za fedha zinawafikia wanawake na naamini kufungwa kwa mauzo haya, kunaashiria kuwa NMB iko tayari kutanua wigo wa utoaji wa huduma ya fedha kwa wanawake na kampuni zinazofanya biashara zinazowagusa wanawake.
Aliitaka NMB, benki nyingine na taasisi za fedha kwa ujumla, ziendelee kubuni mikakati mbalimbali ya kuhakisha wanawake wanafikiwa na huduma mbalimbali za kukidhi mahitaji yao, huku akisema Serikali kupitia Wizara ya Fedha, inaahidi ushirikiano kwa wadau mfano wa benki katika kufanikisha malengo tarajiwa.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema NMB ilipokea maombi 1,630 yaliyowwezesha kukusanya Sh. Bil. 74.27 badala ya Bil. 25 na kuwa mwitikio mkubwa uliooneshwa na wawekezaji tangu kufunguliwa kwa mauzo ya Jasiri Bond, unathibitisha kuaminika kwa benki yake miongoni mwa Watanzania.
“Kuaminika kwa NMB katika hili kunathibitishwa na ukweli kwamba asilimia 96 ya waliotuma maombi ya kununua Hati Fungani, yamepitia katika matawi yetu, huku asilimia 4 tu yakifanyika kupitia Madalali wa Soko la Hisa waliosajiliwa.
“Muitikio huu ni ishara kwamba lengo letu la kusaidia wanawake na kuboresha uchumi wao, limeungwa mkono na Watanzania na wawekezaji wengine katika kufanikisha utoaji wa mikopo inayolenga kuboresha biashara na huduma zinazomilikiwa na wanawake pamoja zile ambazo mnyoro wake unawagusa wanawake.
Zaipuna aliwashukuru wadau wote walioiunga mkono NMB katika kufanikisha mauzo hayo yaliyoweka rekodi na kusaidia kuingia sokoni kwa hati fungani hiyo, likiwemo Shirika la Financial Sector Deepening Afrika (FSD Africa), UN Woman, UNCDF, FSDT, IFC, CMSA, DSE na wengineo wengi.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama, aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Uongozi wa NMB, kwa kufanikisha uuzwaji wa Jasiri Bond kwa Umma wa Watanzania na hatimaye kufikia hatua ya kuiorodhesha DSE, tayari kwa mauzo ya walionunua na manunuzi ya waliokosa katika mchakato uliofungwa.
“Makusanyo haya (Sh. Bil. 74.27 badala ya Sh. Bil. 25) yaliyotokana na mauzo yaliyoanza Februari 7, ni sawa na mafanikio ya asilimia 297 na huu ni uthibitisho kwamba wawekezaji wana imani kubwa na NMB na CMSA na kuwa kuna ukwasi wa kutosha na wawekezaji wako tayari kuwekeza kwenye hati fungani zinazokidhi matakwa yao.
“Kati ya wawekezaji 1,630, wawekezaji 1353 wanatoka nje ya Dar es Salaam ambao ni sawa na asilimia 83, na kati ya hao, 1,607 ni wawekezaji wadogo wadogo ambao ni sawa na asilimia 99, wakati wawekezaji 23 tu ndio taasisi. Hatua hii ni muhimu, kwani imewapa fursa wawekezaji wadogo wengi,” alibainisha Mkama.Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, akizungumza wakati wa hafla ya ufungaji rasmi wa Hatifungani JASIRI ya Benki ya NMB, iliyofanyika katika Ofisi za Soko la Hisa la Dar es Salaam leo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko Hisa la Dar es Salaam (DSE) Moremi Marwa, akizungumza wakati wa hafla ya ufungaji rasmi wa Hatifungani JASIRI ya Benki ya NMB, iliyofanyika katika Ofisi za Soko la Hisa la Dar es Salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Nicodemus Mkama,
No comments:
Post a Comment