NA MWANDISHI WETU
KATIKA kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha Sekta ya Elimu mchini, Benki ya NMB imekabidhi msaada wa madawati 100, viti na meza 100 vyenye thamani ya Sh. Mil. 20 kwa Shule ya Msingi Mbutu na Sekondari ya Minazini, zilizoko wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Msaada huo umekabidhiwa jana Jumatatu Februari 27 na Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Halima Bulembo, ambaye naye alikabidhi kwa Walimu Wakuu wa shule hizo katika hafla iliyofanyika Shule ya Msingi Mbutu.
Akizungumza kabla ya kukabidhi msaada huo, Donatus alisema madawati 100 yenye thamani ya Sh. Milioni 10 yametolewa kwa Shule ya Msingi Mbutu, huku viti 100 na meza 100 vyote vikiwa na thamani ya Sh. Milioni 10 vikienda kwa Shuyle ya Sekondari Minazini, katika Kata ya Somangila wilayani humo.
“Msaada huu ni sehemu ya Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ambako NMB imekuwa na utamaduni endelevu wa kutoa asilimia moja ya faida yake kwa mwaka, kurejesha kwa jamii kupitia sekta za elimu, afya, majanga na mwaka huu tumeongeza mazingira.
“Katika mwaka uliopita, faida yetu ilikuwa Sh. Bilioni 429, ambazo kwa utaratibu wa awali ilikuwa tutoe asilimia moja ambayo ni Bilioni 4.2 katika elimu, afya na majanga.
“Lakini kutokana na janga la mabadiliko ya tabianchi, ambako Serikali imewekeza nguvu kubwa kusaidia utatuzi utokanao na athari zake, nasi tukaongeza fungu letu kwa mwaka huu na tutatoa misaada ya Bilioni 6.2 katika elimu, afya, majanga na mazingira,” alisema Donatus.
Kwa upande wake, DC Bulembo aliishukuru NMB kwa namna inavyojitoa kusaidia sekta za elimu na afya na kwamba msaada huo unathibitisha namna benki hiyo inavyoijali jamii na kutaka wadau zaidi kuiga mfano wa NMB katika kurejesha sewhemu ya faida yao kwa jamii.
“NMB mnastahili pongezi kwa jinsi mnavyosapoti harakati chanya za serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu na afya. Misaada hii inatrhibitisha hilo na niseme kwamba mmesaidia pakubwa sana na msituchoke katika hilo, kwani changamoto ni nyingi,” alisema Bulembo.
Aliwataka wanafunzi hao kutumia misaada hiyo kama chachu ya kujisomea na kukuza kiwango cha ufaulu, huku akiwasisitiza umuhimu wa kuyatunza madawati, viti na meza hizo, ili zitumike kwa muda mrefu katika shule hizo, ili kuwatia moyo wadau wa elimu kama NMB katika kusaidia shule nchini.
Awali, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mbutu, Shaha Mzanda, aliipongeza NMB katika kusaidia utatuzi wa changamnoto ya madawati shuleni hapo, ambapo awali shule hiyo yenye wanafunzi 1018, ilikua ikikabiliwa na uhaba wa madawati 189 na kwamba sasa uhaba utakuwa madawati 89.
Kwa niaba ya wanafunzi wa shule hiyo, Rosemary James alibainisha kwamba madawati hayo yanaenda kuwaondolea changamoto ya kukaa chini inayowakabili wanafunzi wa shule hiyo iliyoanziashwa mwaka 1989, huku akiwataka wadau zaidi kujitokeza ili kuwajengea uzio kuzunguka Shule hiyo.
No comments:
Post a Comment