KUELEKEA mchezo wao wa Jumapili dhidi ya US Monastir ya Tunisia, Kocha wa Yanga, Nasreddin Nabi, ameongeza dozi kwa viungo wake kutokana na ubora walionao wapinzani wao ukiongozwa na kiungo mshambuliaji, Haykeul Chikhaoui.
Yanga watakuwa wenyeji wa mchezo huo wa tano wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC), mchezo utakaochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 1.00 usiku.
Kikosi cha US Monastir ambacho kinajumla ya wachezaji 37, kinamastaa wengi lakini yupo kiungo mshambuliaji huyo raia wa Ufaransa, Chikhaoui ambaye anafanya vizuri akizimudu pia nafasi za winga wa kulia na kushoto.
Katika kuongeza umakini katika mazoezi ya jana asubuhi, yaliyofanyika katika gym za gymkhana, Kocha Nabi alifanya mazoezi binafsi na nyota wake, Stephen Aziz Ki, ambaye anacheza nafasi moja na nyota huyo wa wapinzani wao.
Aziz Ki ambaye thamani yake ni sh. milioni 376 atakuwa na kazi kubwa ya kupambana katika eneo la katikati dhidi ya Chikhaoui ambaye thamani yake ni Sh. bilioni 2.5.
Kocha Nabi alisema ameangalia baadhi ya video ambazo nyota huyo anacheza kuhakikisha anampunguza makali wanapokuja kucheza nao katika uwanja wa nyumbani.
“Nimemuongezea Aziz ki baadhi ya vitu ambavyo naamini vitamsaidia katika mchezo huo ujao na wachezaji wengine pia lakini zaidi alikuwa ni yeye kuongeza uimara,” alisema.
Nabi alisema anafahamu mbinu za US Monastir wanavyocheza na wamelazimika kuongeza muda wa mazoezi ikiwemo kwenda gym kutafuta stamina.
“Tutakuwa na mazoezi ya aina mbili asubuhi tunafanya gym na jioni uwanjani, hii mechi ni ngumu maana tumeona jinsi tulivyocheza mechi ya kwanza mapungufu yaliyojitokeza tunafanyia kazi kuelekea mechi hiyo.
“Kuna wachezaji wanakosa muendelezo mzuri, leo wanacheza vizuri mechi inayofuata wanaonesha kiwango cha chini hicho sifurahishwi nacho, kitu ambacho nafanyia kazi,” alisema Nabi.
Katika msimamo wa kundi D ambalo Yanga imepangwa, ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi saba, ikiongozwa na US Monastir ambao wanapointi kumi wakati TP Mazembe wakiwa nafasi ya tatu kwa pointi tatu na AS Real Bamako inaburuta mkia ikiwa na pointi mbili.
No comments:
Post a Comment