Habari za Punde

SERIKALI YAHIMIZA MATUMIZI YA MATOKEO YA SENSA 2022 KWA MAENDELEO


Na. Peter Haule, WFM, Dodoma.

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi Jenifa Omolo, amewaasa Watakwimu nchini kuchambua, kutafsiri na kutumia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 katika kupanga, kufuatilia na kutathmini utekekelezaji mipango na programu mbalimbali za maendeleo ili kufikia uchumi wa viwanda.

 

Alisema hayo kwa niaba ya Waziri wa Fedha wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Watakwimu wa Tanzania Bara na Zanzibar yaliyoandaliwa na Chama Cha Watakwimu Tanzania (TASTA), yanayofanyika jijini Dodoma.

 

Alisema kuwa ni muhimu kwa Watakwimu kutumia fursa ya mafunzo hayo ili kuhakikisha kuwa wanatumia matokeo ya Sensa kama katika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa programu za maendeleo za kikanda na Kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.

 

"Serikali inasisitiza matumizi ya matokeo ya Sensa kwa kutambua kuwa nchi yetu inaweza kupata thamani ya uwekezaji mkubwa katika utekelezaji wa Sensa ikiwa tu matokeo ya Sensa yatatumika kwa lengo lililokusudiwa katika kupanga, kutekeleza na kutathmini sera, mipango na programu zetu za maendeleo ambazo zitazingatia hali halisi ya idadi ya watu wetu, "alisema Bi. Omolo.

 

Aidha, alitoa wito kwa wadau wote wakiwemo wananchi kuwa sehemu ya mchakato wa matumizi ya matokeo hayo katika kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo kwakuwa wakifanya hivyo wataweza kupata thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali katika kufanikisha zoezi hilo.

 

Bi. Omolo alisisitiza mafunzo hayo yatafanyika vyema kama yalivyopangwa kwa kutimiza malengo yake ya kuwapa uelewa na hatimaye kusambaza matokeo hayo kwa wadau mbalimbali.

 

Kwa Upande wake Mtakwimu Mkuu wa SerikaliDk. Albina Chuwa, alisema kuwa Watakwimu wanatakiwa kwenda katika mlengo mmoja ili kuhakikisha takwimu zinaleta maendeleo kwa jamii.

 

"Takwimu hizi zinatakiwa kuleta maendeleo katika jamii, ni muhimu sasa kwa Watakwimu wote kuhakikisha takwimu hizi zinakuwa chachu na zinaleta maendeleo kwa nchi yetu na jamii nzima,"alisema Dk.  Chuwa.

 

Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Salum Kassim Ali, alisema Watakwimu ndio wanaopanga mipango ya maendeleo ya nchi hivyo ni wajibu wao kila mmoja kuhakikisha matokeo ya Sensa yanatumika ipasavyo.

 

Alisema kuwa anaamini watakwimu hao watakuwa mfano mzuri katika kuwafundisha wengine umuhimu wa matumizi ya matokeo ya takwimu zilizopo.

Mwisho.

 

CAPTIONS

1.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Jenifa Omolo, akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Watakwimu wa Tanzania Bara na Zanzibar yaliyoandaliwa na Chama Cha Watakwimu Tanzania (TASTA), yanayofanyika jijini Dodoma.

 

2.

 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Jenifa Omolo (katikati), Mtakwimu Mkuu wa SerikaliDk. Albina Chuwa (wa pili kulia) na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Salum Kassim Ali (wa pili kushoto), wakiwa katika picha ya Pamoja na watakwimu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, baada ya kufunguliwa kwa mafunzo ya siku mbili kwa Watakwimu hao yaliyoandaliwa na Chama Cha Watakwimu Tanzania (TASTA), yanayofanyika jijini Dodoma.

 

3.

 

Watakwimu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, wakifuatilia mafunzo yaliyolenga kuwawezesha kutafsiri matokeo ya Sensa kwa maendeleo ya wananchi, mafunzo hayo yanayofanyika jijini Dodoma, yameandaliwa na Chama Cha Watakwimu Tanzania (TASTA).

 

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dodoma)

 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.