Habari za Punde

*MASHINDANO YA KILI TAIFA CUP 2010, YAZINDULIWA RASMI DAR
















Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania, Frederick Mwakalebela (wapili kulia) Mkurugenzi Masoko wa Kampuni ya TBL, David Minja (wapili) kushoto, wakizindua rasmi mashindano ya Kilimanjaro Taifa Cup, yanayotarajia kuanza Mei 8 mwaka huu, wakati wa mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo. Kushoto ni Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe na (kulia) ni Ofisa Habari wa TFF, Frolian Kaijage.



Mkurugenzi wa masoko wa Kampuni ya Bia TBL, David Minja, akizungumza na waandishi wa habari leo wakati akitangaza uzinduzi rasmi wa mashindano ya Kili Taifa Cup, yanayotarajia kuanza Mei 8, mwaka hu. Kushoto ni Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania, Frederick Mwakalebela.




Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Frederick Mwakalebela, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, wakati wa mkutano wa kutangaza uzinduzi wa mashindano ya 'Kili Taifa Cup', yanayotarajia kuanza Mei 8 mwaka huu na kushirikisha jumla ya vituo sita. Katikati ni Mkurugenzi wa Masoko wa TBL, David Minja na Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe.
Na Sufianimafoto Reporter, jijini Dar es Salaam.

Mashindano ya Kombe la Taifa (Kili Taifa Cup 2010) yamezinduliwa rasmi leo katika ofisi za Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), huku maofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wafanyakazi wa TBL na waandishi wa habari wakishuhudia.

Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Kilimanjaro Premium Lager, moja ya aina za bia za TBL kudhamini mashindano hayo yanayosaidia kung’amua na kukuza vipaji mbalimbali kuanzia ngazi za chini hadi timu ya taifa na kwenye klabu kubwa za mpira wa miguu ndani na nje ya nchi. Hata hivyo ni mara ya nne kwa kampuni ya TBL kudhamini mashindano haya.

"Tunajivunia kufadhili mashindano makubwa kama haya ambayo si tu yataleta shamrashamra miongoni mwa washabiki wa soka kote nchini, lakini pia yatasaidia kung’amua vipaji vipya na labda kuwaingiza baadhi ya wachezaji hao kwenye timu za taifa au kwenye klabu zinazoongoza," anasema David Minja, Mkurugenzi wa Masoko wa TBL.

Alisema kwamba mashindano ya mwaka huu yanafanyika chini ya dhima: ‘Kufikisha Soka ya Tanzania kwenye kilele cha mafanikio,’ yatajumuisha timu 24 zitakazocheza katika vituo sita, ambapo inatarajiwa kwamba mashindano hayo yataanza Mei 8, 2010 hadi Mei 15, 2010 katika vituo vyote hivyo, ambapo kila timu itacheza na mwenzake kwenye ngazi za mzunguko kisha zitakazopata pointi nyingi zaidi zitaingia kwenye hatua ya robo fainali.

Kwa mujibu wa Minja, robo fainali hizo zitachezwa Mei 22, 2010 na fainali zitakuwa Mei 30, 2010, na kwamba vituo hivyo sita ni pamoja na Mtwara, Arusha, Dodoma, Tanga, Iringa na Shinyanga.

"Ufadhili kwa mashindano yote ni Tsh milioni 850 na kila timu itapokea fedha za maandalizi, usafiri na malazi pamoja na seti za sare za michezo kwa ajili ya mashindano hayo," alisema Mkurugenzi huyo wa TBL.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa TFF, Frederick Mwakalebela alisema; "Tuna furaha kwa kuwa mashindano ya mwaka huu pia yatahusisha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 lakini watakaocheza ni wale waliozidi miaka 18. Timu zote zimejiandaa kwa ajili ya mashindano haya, hivyo tunawaomba Watanzania wote wajitokeze kwa wingi kuunga mkono timu zao."

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.