Habari za Punde

*MATATANI KWA KUKUTWA NA BOMU LA KULIPULIA VIFARU NA MIAMBA


Na Christopher Gamaina, Tarime

WATU wawili wanashikiliwa na Polisi katika mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya kwa tuhuma za kukutwa na bomu la kivita la kulipulia vifaru na miamba lililotengenezwa mwaka 1913.Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi Constantine Massawe, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Selemani Idd Mwita (35) mkazi wa kijiji cha Itiryo na Ramadhani James Lameck (28) mkazi wa kijiji cha Sirari, wilayani Tarime.Kwa mujibu wa Kamanda Massawe, watuhumiwa hao walikamatwa Mei 10, mwaka huu, saa nane mchana, katika mji mdogo wa Sirari wakiwa na bomu hilo lenye muundo wa kiazi kitamu.Alisema kwamba baada ya kuwatia mbaroni watuhumiwa hao aliwaita askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao walilichunguza na kulitambua bomu hilo kuwa ni aina ya Anti-take lililotengezwa mwaka 1913 mahususi kwa ajili ya kulipulia vifaru na miamba.Kamanda Massawe aliongeza kuwa watuhumiwa hao wanadaiwa kutapeli wananchi watano kwamba bomu hilo ni madini aina ya rupia na kujipatia kiasi cha Sh milioni nne kwa makubaliano ya kuwauzia.“Kuna watu watano wamejitokeza na kudai kuwa watuhumiwa hao wamewatapeli shilingi milioni nne baada ya kuwadanganya kwamba bomu hilo ni madini aina ya rupia,” alisema.Alisema polisi wanaendelea kuwahoji watuhumiwa hao na kwamba watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili mara baada ya upelelezi wa awali kukamilika.Kufuatia tukio hilo , Kamanda huyo wa Jeshi la Polisi alitoa wito kwa wananchi kutokuwa wepesi wa kurubuniwa na kutaka kujipatia fedha kwa njia ya mkato, badala yake wajenge tabia ya kutafuta kipato kwa njia na shughuli halali.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.