Habari za Punde

*RAIS JAKAYA, ARMANDO WAZINDUA DARAJA LA UMOJA



Rais Jakaya Kikwete (kushoto) na Rais wa Msumbiji, Armando Guebuza, wakikata utepe kuzindua daraja la umoja lililopo eneo la mtambaswala, wilaya mpya ya Nanyumbu, mkoani Mtwara wakati wa hafla ya zinduzi wa daraja hilo lililozinduliwa jana. Picha na Freddy Maro



Na Mwandishi Wetu, Mawasiliano Ikulu
Kati ya vitu ambavyo vitaendelea kukumbukwa na kuimarisha ushirikiano uliojengwa kwa muda mrefu kati ya Tanzania na Msumbiji pamoja na nchi nyingine za kusini mwa bara la Afrika, ni daraja la Umoja linalokatisha kwenye Mto Ruvuma.
Daraja hilo lenye urefu wa mita 720 limejengwa kusini mwa Tanzania eneo la Mtambaswala wilaya ya Nanyumbu kuelekea upande wa Kaskazini wa Msumbiji wa jimbo la Gabo Delgado.
Rais Jakaya Kikwete anatarajia kuzindua daraja hilo tarehe 12 Mei mwaka huu katika sherehe itakayohudhuriwa na pia na Rais Armando Gwebuza wa Msumbiji.
Daraja hilo limejengwa na kampuni ya M/S China Geo Engineering Corporation, iliyopewa mkataba wa ujenzi Oktoba 16, 2005 chini ya mradi maalumu unaofahamika kama “Unity Bridge” kwa gharama ya dola za Marekani 27.5 milioni sawa na zaidi ya fedha za kitanzania shilingi bilioni 34 fedha amabzo zilitolewa kwa ushirikiano sawia kati ya serikali ya Tanzania na serikali ya Msumbiji.
Ni daraja ambalo lina nguzo 18, tisa za Tanzania na zilizobaki ni nguzo za Msumbiji kama sehemu ya mpaka, ambao kwenda mbele unaunganisha upande wa kaskazini mwa nchi hiyo jirani kuelekea Cape Town , Afrika Kusini.
Aidha ujenzi wa daraja la moja kuvuka mto Ruvuma ni matokeo ya wazo lililotolewa na Marais waasisi wa nchi mbili ambao ni Hayati Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Samora Machel wa Msumbiji mwaka 1975 ili kuunganisha nchi za Tanzania na Msumbiji kupitia mikoa ya Mtwara upande wa Tanzania na Gabo Delgado upande wa Msumbiji.
Hata hivyo kupitia mkutano kati ya uongozi wa mkoa wa Mtwara na jimbo la Gabo Delgado uliofanyika mwezi Juni 1996 ilikubaliwa kuwa daraja la Umoja lijengwe sehemu ya Negomane upande wa Msumbiji na Mtambaswala upande wa Tanzania .
Mwaka 2002 mwezi Machi serikali ya Tanzania na Msumbiji zilitia saini makubaliano kwa madhumuni ya kuweka utaratibu wa kupatikana fedha na nyenzo za ujenzi wa daraja hilo na baadaye uzinduzi wa ujenzi wa mradi huo kufanyika mwaka 2005 kwa Marais Benjamin William Mkapa wa Tanzania na Rais Armando Emilio Guebuza wa Msumbiji kuweka jiwe la msingi ikiwa ni ishara rasmi ya kuanza ujenzi huo.
Mbali na mikakati ya ujenzi wa daraja hilo kuanza chini ya Serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais Benjamini Mkapa, serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete iliendeleza juhudi hizo kuhakikisha kuwa mradi huo wa kisasa unakamilika kwa ubora na viwango kwa kuongeza fedha zaidi.
Daraja la hilo linatarajiwa kuwa kichocheo cha shughuli za kijamii na kiuchumi kati ya mikoa jirani , nchi na ukanda wote wa maendeleo wa Mtwara (Mtwara Development Corridor) zaidi ya hili ujenzi wake ulipewa kipaumbele katika mipango ya maendeleo ya SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa lengo la kurahisisha mawasiliano ya barabara miongoni mwa nchi za kusini mwa Afrika.
Kubwa ambalo linaonekana hapa ni kuzidi kuimarishwa kwa uhusiano wa kihistoria, ambao ulikuwepo baina ya nchi hizo wakati wa harakati za ukombozi.
Mkuu wa wilaya ya Masasi Saidi Alli Amanzi ambaye awali mradi huo ulikuwa chini ya wilaya yake kabla ya kuhamishiwa wilaya mpya ya Nanyumbu zinafanyika anasema kukamilika kwa daraja la Umoja kunalifanya eneo hilo la kusini mwa Tanzania kuwa mlango wa kuziunganisha nchi za kusini na kaskazini mwa bara la Afika.
“Sasa wilaya mpya ya Nanyumbu itakuwa njia kuu kwa upande wa kusini mwa Tanzania ikiunganisha mataifa mengine kutokana na kuwa kituo kikuu na kitovu cha biashara cha nchi kusini mwa Bara la Afrika na Kaskazini mwa Bara la Afrika,” anabainisha Bw. Amanzi.
Anafafanua kuwa, wilaya ya Masasi itapata mabadiliko makubwa kutokana na kuanza kutumika kwa daraja hilo kutokana na kuwa katikati kwa kuwa kuiunganisha cha miji mingine ya Tanzania inayotabiriwa kuendelea kukua kwa kasi kutokana na mabadiliko ya kuwepo kwa daraja hilo.
Bw.Amanzi anaendelea kufafanua kuwa pamoja na mabadiliko hayo yote mchango wa daraja hilo utaendelea kuwa mkubwa hasa kwa ukanda wa Mtwara (Mtwara Corridor) kupitisha bidhaa mbalimbali ambazo zitapitia katika bandari ya Mtwara kuelekea nchi za Kusini zisizokuwa na bandari.
Aidha baadhi ya wafanyabiashara kutoka Tanzania wataendelea kunufaika kutokana na fursa za biashara zilizopo katika nchi ya Msumbiji hasa madini na biashara ya mbao.
Kiafya anasema wananchi wa Msumbiji walio mpakani watanufaika zaidi hasa kupitia hospitali ya Ndanda.
Anasema changamoto iliyopo ni kuelimnisha jamii kuhusu ugonjwa wa Ukimwi kutokana na urahisi wa mwingilino wa wananchi kutoka nchi moja kwenda nyingine hali inayoweza kuwa kichocheo cha ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI.
Hivi sasa wananchi wa pande hizo mbili wanatumia baiskeli kuvuka mpaka wakati huu ambapo magari hayajaruhusiwa rasmi kupita katika daraja hilo .
Hata hivyo anaafanua kuwa fungamano la kiutamaduni baina ya wakazi wa maeneo ya kusini hasa makabila ya Wamakonde, Wayao na Wamakua limeongezeka kutokana na jamii hizi kuelewana lugha na wakati mwingine kuoa au kuolewa upande mwingine ingawa lugha ya Kireno inabaki kuwa tazizo kubwa kueleweka miongoni mwa watu wengi kutoka Tanzania .
Kielimu vijana wengi kutoka Tanzania watanufaika zaidi kutokana na urahisi wa kuigia nchini Msumbiji kwani kabla ya kukamilika kwa daraja walikua wanakwenda nchini Msumbiji kujifunza aidha kupitia taasisi mbalimbali za utafiti kwa kutumia majahazi ambayo usalama wake ulikuwa mdogo hasa wakati wa masika ambapo mto Ruvuma unakuwa umejaa maji na wakati mwingine hatari ya kuliwa na mamba.
Naye Katibu Tawala wa wilaya ya Masasi, Bw. Bakari Abdallah Shamkupa anasema tayari serikali kupitia kuweka mazingira mazuri ku kupitia wizara mbalimbali inajipanga kuhakikisha kuwa miundombinu ya ukanda wa kusini inaimarika.
Katibu Tawala huyo anasema kukamilika kwa daraja hilo kutakuwa ni ufunguo kwani kutarahisisha mwingiliano wa shughuli za kiuchumi kati ya Tanzania na jirani kutoka Msumbiji na maeneo mengine na tayari serikali iko mbioni kuhakikisha kuwa sanjari na kuanza kutumika kwa daraja hilo ujenzi wa miundimbinu, Ujenzi wa maeneo ya Wageni, Vituo vya Polisi , vituo vya kisasa vya uhamiaji na mipango miji kwa ajili ya makazi ya watu unaanza mara moja ili kulifanya eneo hilo kuwa la kisasa na salama.
Kwa upande wake Afisa Uhamiaji wa Wilaya ya Masasi ambaye kituo chake bado kinahusika na usimamizi wa shughuli za uhamiaji katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji Bw. Hamidu Mkambala anasema kabla ya kujengwa kwa daraja hilo njia za uchochoro zilikua chache kutokana na hatari ya mto Ruvuma kuwa na mamba wengi hivyo idadi ya wananchi waliokua wanvuka kuelekea Msumbiji haikua kubwa sana.
Hata hivyo anabainisha kuwa kukamilika kwa daraja ni changamoto kwa Idara yake ambayo inakabiriwa na upungufu wa watumishi kuongeza idadi ya watumishi katika eneo hilo wakati ambapo serikali inanjipanga kuimarisha miundombinu katika eneo hilo .
Mfanyabiashara Bakari Ismabarad ambaye anafanya shughuli zake Wilayani Masasi na wakati mwingine kupeleka bidhaa nchini Msumbiji anasema kabla ya kukamilika kwa daraja walikua wakisafirisha bidhaa mbalimbali kupitia majahazi ambayo usalama wake ulikua mdogo na wakati mwingine kuzama ndani ya maji na kusababisha hasara na upotevu wa mali na wakati mwingine kusababisha vifo.
Bw. Hajji Swad mfanyabiashra maarufu katika eneo la Mangaka wilayani Nanyumbu anasema baada ya daraja la umoja kukamilika anaziona fursa tele za kibiashara kutokana na urahisi wa kuvuka na kuingia upande wa pili.
“Kwa upande wangu najiandaa kupokea vitu vingi sana kutoka msumbiji vikiwemo sukari,sabuni na bidhaa mbalimbali katika biashara yangu” anafurahia.
Bw. Zuberi Ndago dereva wa pikipiki kwa jina maarufu la Bodaboda katika eneo la Mangaka ambapo ni makao makuu ya shughuli za serikali wilayani Nanyumbu anasema kukamilika kwa daraja la umoja ni fursa nzuri hata kwenye biashara yao kwani wamekuwa wakipata abiria wengi ambao huwakodi kuelekea Mtambaswala eneo kuliona daraja kwa gharama ya kuanzia 15,000/= hadi 25,000/=.
Kwa upande wake mzee Gabriel Baina mkazi wa kijiji cha Lukula eneo la Mtambaswala niliyekutana naye katikati ya daraja la Umoja akiwa na baiskeli yake akitokea upande wa pili wa Msumbiji analielezea daraja la Umoja nguzo muhimu katika kuimarisha mahusiano kati ya na jirani zao wa Msumbiji.
Anasema kwa sasa kuna njia ya uhakika kuelekea Msumbiji tofauti na ilivyokuwa mwanzo na sasa wafanyabiashara kutoka Msumbiji wanaleta karanga, mahindi na mazao mengine wakati wao wanapeleka ufuta, mpunga na Choroko.
Kwa sasa kuwa, kwa sasa kuna njia ya uhakika kuelekea Msumbiji tofauti na ilivyokuwa mwanzo na sasa wafanya biashara kutoka Msumbiji wanaleta karanga, mahindi na mazao mengine wakati wao wanapeleka ufuta, mpunga na chooroko.
Kwa sasa wana Msumbiji wengi wanakuja kwetu Tanzania kwa sababu ni karibu na mahitaji yao wanayapata huku kwetu Mtambaswala.” Anaeleza Mzee Baina.
Wanawake nao hawakubaki nyuma katika kufurahia kukamilika kwa daraja la Umoja akiwemo Bi.Saphina Raymond mkazi wa kijiji cha Lukula ambaye nilikutana naye akiwa na wanawake wenzake wakiwa na watoto wachanga wakikatisha daraja kuelekea upande wa Msumbiji eneo la Ngomano kupata matibabu.
“Daraja linaturahisishia mambo mengi sana kwani kabla ya ujenzi wa ilitulazimu kutoa nauli ya shilingi 1000 kuelekea upande wa pili kupata matibabu kutokana na ukaribu na kijiji chetu na gharama nafuu kwani ukiwa na shilingi 1000 unatibiwa vizuri” anaeleza huku akiendelea na safari yake kuelekea Msumbiji.
Katika eneo la mto huo na daraja watoto wadogo nao wamekuwa wakifurahia eneo hilo la mpaka ikiwa ni pamoja na kucheza na wenzao wa Tanzania .
Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu Bi. Fatma Salum Ally anayo mengi ya kusimulia kwa kulifananisha daraja hilo na ukombozi wa wilaya ya Nanyumbu kutokana na fursa tele zilizopo.
Anasema kukamilika kwa daraja hilo ni fursa nzuri katika maendeleo ya wakazi wa wilaya ya Nanyumbu ambao wengi ni wakulima hasa kuongeza idadi ya wateja wa mazao wanayolima ya Muhogo, Choroko, kunde na karanga na wataanza kuona umuhimu wa kauli mbiu ya “KILIMO KWANZA ”
Anaendelea kufafanua kuwa hivi sasa zao la Choroko limekuwa likiwapatia pesa nzuri kwani huuza shilingi 1500 kwa kilogramu moja.
“Hali hii inatoa hamasa kubwa kwa wakulima kuendelea kulima zaidi ingawa hatutaweza kuzalisha kila kitu wenzetu wana sukari, maziwa na bidhaa nyingine nzuri tutanufaika wote kwa pamoja kupitia daraja hili,” Anasema Bi Fatma.
Anaeleza kuwa kuwa eneo la Mtambaswala ambalo kwa sasa ni kitongoji litapata watu wengi kutokana na watu wengi kuvutiwa kuja kuishi na hilo litachangia kuwepo kwa mji mkubwa wenye miundombinu ya kisasa na uwekezaji wa nyumba za kulala wageni, vituo vya afya, vituo vya kuuzia mafuta na vingine vingi.
Kwa upande wa utalii Bi. Fatma anasema sasa shughuli za uwekezaji zitaongezeka sanjari na ongezeko la watalii wa ndani kutokana na daraja lenyewe kuwa kivutio cha utalii wa ndani na nje ya nchi na chanzo cha kuitangaza vizuri wilaya mpya ya Nanyumbu.
“Wageni wengi watamiminika wilayani Nanyumbu kuja kuona hifadhi nzuri ya Lukwika Lumesule na kushiriki katika shughuli za utalii na uwindaji jambo ambalo linatupatia 20% mapato yanayokusanywa ambayo hurudishwa kwenye Halmashauri yetu kuimarisha shughuli za maendeleo,”
Mkuu huyo wa wilaya anatoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kuwekeza katika wilaya ya Nanyumbu wajitokeze kujenga nyumba za kisasa kwa ajili ya makazi, vituo vya biashara, maduka makubwa, shughuli za usafirishaji, kuwekeza katika huduma za afya na Elimu.
Anawahakikishia wananchi kuwa serikali kwa sasa inaendelea kuimarisha huduma mbalimbali za kijamii ili kukabiliana na mabadiliko ya kimaendeleo yanakayokuja.
Kati ya maeneo ambayo serikali inaendelea kuyaboresha pamoja na kituo cha Afya Mangaka ambayo ndiyo makao makuu ya wilaya ya Nanyumbu kwa kukifanya kuwa hospitali ya wilaya ambapo anasema tayari jengo la wagonjwa nje tayari limeshakamilika na hatua mbalimbali zinaendelea kufanywa na serikali kukamilisha ujenzi wa jingo la wodi ya wazazi pamoja na kuongeza watumishi na wataalam wa afya na uoreshaji wa miundombinu ya usafiri yakiwemo magari ya kubebea wagonjwa (Ambulance).
Aidha uimarishaji wa miundombinu ya barabara unaendelea kwa kiwango ha lami hasa barabara ya Masasi – Mangaka (km 55) ambayo ni sehemu kuu ya ukanda wa maendeleo wa Mtwara(Mtwara Development Corridor) kwa maana ya Mtwara – Masasi- Tunduru-Songea – Mbambabay kilometa 860 hadi Lilongwe nchini Malawi umbali wa km 1263.
Aidha barabara hii inatarajiwa kurahisisha shughuli za usafirishaji kuendeleza eneo la kusini lenye utajili wa mazao ya kilimo, madini na utalii na kuhudumia sehemu kubwa ya maeneo ya uzalishaji wa zao la Korosho mkoani Mtwara.
Tanzania na Msumbiji pamoja na nchi nyingine za SADC, zimekuwa na uhusiano mzuri tangu harakati za kupigania uhuru miaka ya 1970.
Sehemu ya Daraja hilo linavyoonekana, baada ya uzinduzi.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.