Habari za Punde

*UONGOZI MPYA SIMBA WAKABIDHIWA OFISI RASMI, LAKINI KUNAWALAKINI





Na Sufianimafoto Reporter, jijini

UONGOZI mpya wa Mabingwa wa soka Tanzania Bara, timu ya Simba ya jijini Dar es Salaam leo umekabidhiwa rasmi nyaraka za ofisi pamoja na mali za klabu kutoka kwa uongozi uliopita.

Makabidhiano hayo yaliyofanyika kwenye Makao Makuu ya klabu hiyo yaliyopo mtaa wa Msimbazi Kariakoo, ilionekana kuwapo kwa dosari kwa uongozi wa klabu hiyo chini ya Mwenyekiti Hassan Dalali kushindwa kukabidhi hati ya majengo mawili ya klabu hiyo.

Katibu Mkuu wa klabu hiyo Mwina Kaduguda, alisema kuwa hati hizo wameshindwa kukabidhi kwa uongozi mpya kwa kuwa hati ya jengo jipya ipo mikononi mwa mpangaji Haji Salim Hemed, ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2014, wakati ile ya jengo la zamani anayo Mjumbe wa Baraza la Wazee wa klabu hiyo Hamisi Kilomoni.

Makabidhiano mengine yaliyofanyika ni pamoja na mkataba wa timu hiyo na Kampuni ya Bia Tanzania [TBL], mkataba wa Push Mobile, Katiba ya Klabu hiyo, Akaunti tatu za Benki, mabasi mawili yaliyotolewa na TBL, Coaster yenye namba za usajili T 677 AZR, T 688 AZU na lile ambalo lilikuwa kwa ajili ya kocha, T 229 AUF lililopo yadi na ule mkataba wa kampuni ya Kimarekani ya Snejjer Sports and Casual Wear amabo utaiwezesha timu hiyo kupatiwa vifaa vya michezo kwa mwaka mzima na Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu.

Katika hatua nyingine, Katibu huyo, Kaduguda aliwataka viongozi wa klabu hiyo chini ya Mwenyekiti wake Ismail Aden Rage, Makamu wake Gofrey Nyange ambao wameingia madarakani baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Mei 9 mwaka huu kujali maslahi ya timu na kuendeleza umoja na mshikamano ili amani itawale ndani ya klabu na kuifanya iwe na mafanikio zaidi.

Naye Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Dalali alitumia fursa hiyo kuwapongeza wachezaji kwa ushindi wa mabao 2-1 jana dhidi ya Atraco katika Mashindano ya Kombe la Kagame yanayoendea nchini Rwanda.

“Nashukuru na kuwapongeza sana vijana na wahakikishe kuwa Kombe hilo linakuja nyumabani, lakini leo tunaweka msingi wa kihistoria wa kukabidhiana ofisi na mali za klabu kwa amani na kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Klabu hii, naamini tukiendeleza umoja huu Simba itakuwa ya kisasa zaidi”, alisema.

Naye Rage alimpongeza Dalali kwa kuonyesha kitendo cha uungwana kwa kukabidhi ofisi na kusema kuwa hiyo ni dalili ya uadilifu.

“Kanuni ya 29 ya FIFA (Shirikisho la Soka Duniani) inazungumzia uadilifu na hata wenzetu wa nyumbani (Shirikisho la Soka Tanzania TFF) wanasisitiza juu ya hilo, hii ndiyo Fair Play inayotakiwa”, alisema Rage.


Dalali na Msemaji wa zamani wa Klabu hiyo, Cliford Ndimbo, wakiwa ndani ya Ofisi hiyo wakati wakisubiri wafanyakazi kumalizia usafi ili kuanza makabidhiano.

Viongozi hao wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari, wakati wa makabidhiano ya mali na Ofisi ya Klabu hiyo.

"Wacha nisepe na kilicho changu mapema"
Msemaji wa zamani wa Klabu hiyo Ndimbo akisepa na begi lake kutoka ndani ya Klabu hiyo, baada ya makabidhiano ya ofisi.

Viongozi hao wakifurahia jambo baada ya makabidhiano hayo, wote meno thelarhinanje yote mbili kwa furaha.
Mafundi wakimalizia kufunga taa ndani ya ofisi hizo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.