Habari za Punde

*WANANCHI WA MBEZI MTONI WAANDAMANA KUMTAKA MWENYEKITI WA SERIKALI YA MTAA WAO AJIUZULU



Na Sufianimafoto Reporter, jijini Dar es Salaam

WANANCHI wa Mbezi Mtoni Kata ya Kawe leo wameandamana kupinga uongozi wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, ambaye ameingia madarakani hivi karibuni kwa kuchaguliwa na wananchi katika uchaguzi uliopita kutokana na Mwenyekiti huyo kudaiwa kuuza maeneo ya wananchi yaliyotengwa kwa ajili ya maendeleo bila kuwashirikisha.
Wakazi hao wa Mbezi mtoni walionekana na bango lililokuwa likisomeka ‘Sasa umeingia Tarime Full Machafuko’, huku wakiwa na mapanga wakilinda maeneo ambayo bado hayajauzwa baada ya kuona watu wasiojulikana wakilandalanda katika maeneo hayo na mwenyekiti huyo tokea jana.
Vijana wa maeneo hayo waliamua kujikatia maeneo yaliyokuwa yamebakia na kuweka alama za kumiliki maeneo hayo baada ya kuona mwenyekiti huyo amezidi kujichukulia maamuzi na bila kutoa taarifa kwa wananchi kuhusiana na ujenzi aliokwisha uanza anaodai ni Hospitali ya yenye thamani ya shiilingi milioni 20.
Sufianimafoto ilifanikiwa kufika eneo la tukio na kuwakuta wananchi hao wakiwa wamekusanyika katika msingi ulioanza kujengwa ambao umeelezwa kuwa ndiyo hasa hospitali ambayo wananchi wanaipinga kutokana na gharama zilizotajwa na hali halisi inayoonekana.
Aidha gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta Mwenyekiti huyo na kufanikiwa kumkuta katika ofisi ya serikali ya Mtaa, ambayo tayari nayo ilikuwa imezingirwa na wananchi wenye hasira huku wakiimba kumshinikiza kujiuzulu madaraka kutokana na uongozi wa ubabaishaji.
Baada ya mwenyekiti huyo aliyejitambulisha kwa jina la Joseph Benjamin, kuulizwa kuhusiana na ujenzi wa hospitali hiyo unabaraka zozote za wananchi ama Kamati ya Maendeleo ya mtaa huo, alijibu kuwa alishafanya vikao vingi kuhusiana na ujenzi huo na kuhusiana na kuwaongoza wananchi hao kibabe alidai kuwa, anaamini hao waliofikisha malalamiko hayo ni wale tu ambao amekuwa akikataa kuwanunulia bia pindi wanapokutana katika Baa.
Alipotakiwa kuonyesha karatasi za kumbukumbu za vikao vilivyopita vinavyohusu ujenzi wa hospitali hiyo, aliwataka waandishi wa habari kumpa muda na kuahidi warudi siku ya pili yake ili kuandaa na baada ya kubanwa na kupewa muda wa saa moja alisimama na kuelekea nyumbani kwake iliyo umbali wa mita 15 hivi kutoka ofisi hiyo, huku akizomewa na wananchi na baada ya dakika 38 alirejea akiwa na karatasi hizo.
Baada ya kufika alipoanza kuonyesha kwa waandishi wa habari zilionekana ni za vikao vilivyopita vya maendeleo ambavyo havikuwahi kufikia muafaka wala makubaliano kama ilivyoelezwa na wananchi hao.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Mtaa huo aliyejitambulisha kwa jina la Fredick Ngonyani, alipoulizwa kuhusiana na ujenzi huo alidai kuwa hauna baraka zozote za Kamati hiyo wala wananchi badala ya kuona tu mafundi wakianza kujenga.
“Hatujui pesa zinazotumika katika ujenzi huo zimetoka wapi wala wakandarasi wa ujenzi huo hatuwatambui, wala mwekahazina ila tunaona tu ujenzi ukiendelea, na tunapohoji kuhusiana na ujenzi huo tunajibiwa hatuna madaraka ya kuhoji kwani yeye ndiyo Mwenyekiti aliyechaguliwa na watu wengi” alisema Ngonyani.

Mwenyekiti huyo, Joseph Benjamin akiwa na waandishi wa habari katika ofisi yake akihojiwa kuhusiana na tuhuma hizo zinazomkabili dhidi ya wananchi wake.

Hawa ni baadhi tu ya wananchi wa maeneo hayo waliokuwa wameizingira ofisi ya Serikali ya Mtaa huo wakiimba na kupiga makerere kumtaka mwenyekiti huyo ajiuzulu madaraka japo ana miezi michache tu tangu achaguliwe na wananchi katika uchaguzi wa Serikali za mtaa uliopita hivi karibuni.



No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.