Habari za Punde

*MKUTANO WA MAREKEBISHO YA KATIBA YANGA, MADEGA ATOLEWA UKUMBINI CHINI YA ULINZI MKALI



Na Sufianimafoto Reporter, jijiji Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Iman Madega leo ametangaza rasmi kutotetea nafasi yake hiyo katika uchaguzi ujao wa viongozi.
Madega ametoa kauli hiyo leo mchana wakati wa Mkutano wa kupitisha marekebisho ya katiba ya Klabu hiyo, baada ya kurekebisha baadhi ya vifungu na kupanga kuchaguana Juni 27 mwaka huu.
Katika mkutano huo wa katiba uliofanyika chini ya ulinzi mkali kwenye ukumbi wa Maofisa wa Polisi Osterbay, wanachama walionekana kuwa na jazba na kufikia uamuzi wa kutulia na kuridhia, baada ya maelezo ya kuridhisha yaliyotolewa na Makamu wa kwanza wa Rais wa Shirikisho la Soka (TFF), Athuman Nyamlani, pamoja na mwanasheria wao, Alex Mgongolwa na kupigiliwa msumali wa mwisho na Jaji mstaafu, John Mkwawa na kutangaza tarehe hiyo baada ya Mwenyekiti Iman Madega kuususa mkutano huo na kutaka kufuunga bila maridhiano na wanachama.
Akizungumza na wanachama lukuki wa klabu hiyo wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 4, 000, Nyamlani aliwaasa kuwa makini juu ya maamuzi yoyote na kuwataka wasifanye lolote kutokana na shinikizo la mtu au watu fulani.
“Yanga Oyee, Yanga Oyee, Mie Yanga mwenzenu Jamani, nafikiri mnafahamu hilo, lakini leo nipo kama mwakilishi wa TFF ambaye ninahitaji kuona marekebisho mnayofanya ni maagizo kweli tuliyowapa.
“Na si vinginevyo hivyo tumieni fursa hii adimu kuhakikisha mnatimiza haki yenu ya msingi na kufikia uamuzi utakaowaletea maendeleo” alisema Nyamlani.
Wanachama hao waliamua kupinga mapendekezo karibu yote yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wao Madega na kwa mantiki hiyo, Madega ni kama amepigwa ‘bao la kisigo’ na mdhamini wao Yusuf Manji baada ya mapendekezo aliyowasilisha siku moja tu kabla ya mkutano wa marekebisho hayo kupitishwa.
Jana, Manji aliwasilisha mapendekezo yake na kuwataka wanachama kuwa makini baada ya kudai katiba hiyo ilichezewa na wajanja wachache kwa manufaa yao.
Moja ya mapendekezo hayo ni kuhusiana na Ibara ya 62 (h) inayosema baraza la wadhamini litawajibika kwa Mkutano Mkuu lakini katika mapendekezo mapya ilitaka baraza hilo liwajibike kwa kamati ya utendaji na si kwingineko.
Mapendekezo mengine ni Ibara ya 22 (2) inayotaka kufanyike mabadiliko na kuongeza idadi ya wanachama wa kuitisha mkutano wa dharura kutoka nusu hadi theluthi mbili ya wanachama.
Pamoja na Ibara ya 29 (4) iliyopendekeza uongozi uliomaliza muda wake uendelee kuwa madarakani kwa mwaka mmoja zaidi hadi mwaka 2011 huku akipendekeza Uchaguzi Mkuu ufanyike Juni 27 mapendekezo ambayo yote yameridhiwa na wanachama.
Awali akitoa ufafanuzi kuhusiana na marekebisho hayo, Mwanasheria wa TFF, Alex Mgongolwa aliwaaambia wanachama kuwa ndio wenye dhamana ya yote watakayofikia katika mkutano huo lakini kuna baadhi yake hawawezi kuyakwepa kutokana na kufungwa na sheria.
Moja ya mambo hayo ni kuhusiana na ukomo wa uongozi ambao alisema hata kama watakubaliana miaka mitatu au minne lakini viongozi waliopo ni lazima wang’atuke na watakaochaguliwa ndio watawatumikia kwa muda wakataoafikiana.
Mbali na hoja hiyo, pia aliwaeleza kamwe bodi yao ya udhamini haiwezi kuwajibika kwa Kamati ya Utendaji kama walivyoleta mapendekezo badala yake ni Mkutano kama huo ndio wenye dhamana na bodi hiyo.
Kuhusiana na kupanga uchaguzi, hilo liko mikononi mwao lakini baada kwanza kuafikiana baadhi ya vifungu vya marekebisho ya katiba jambo lililowakutanisha hapo.
Naam, hapo ndipo sinema ilipoanzia baada ya Mwenyekiti Madega kuinuka na kuwauliza wanachama kama wameafiki mapendekezo ya TFF mara tatu kisha akasema lililowaleta limekwisha kwani huo ulikuwa mkutano wa marekebisho na kuwaambia mkutano umefungwa.
“Natamka mkutano umefungwa kwani hili ndilo lililotuleta” kisha akainuka kutoka meza kuu na kuanza kuondoka kabla ya kuwatangazia wanachama tarehe ya uchaguzi na hapo ndipo walipoanza kupiga kelele na kumzomea.
“Mwizi, mwizi huyoooo, huyooo” na kuonekana wenye hasira ambao wangeweza hata kumzuru kwa kitendo hicho ndipo Polisi waliokuwapo kwa ajili ya usalama wakaamua kumzuia kwa muda na kutoa fursa kwa Jaji Mkwawa kuongea.
Jaji Mkwawa alisimama kutoka meza kuu na kuanza kuzungumza na wanachama kwa salamu za Yanga oyee, tusikilizane, jamani sikilizeni ili kurudisha hali ya utulivu katika ukumbi huo baada ya baadhi ya wanachama kukerwa hivyo amani kuanza kupotea.
Baada ya dakika kama mbili hivi, hatimaye wanachama walitulia na kumsikiliza Jaji Mkwawa ambaye aliwaaambia “ kisheria uongozi umemaliza muda wake tangu Mei 29.
“Na kama bado wapo madarakani ukomo wao ni ndani ya siku 40 ambazo zinakoma Juni 27, hivyo upo uwezekano wa uchaguzi kufanyika tarehe hiyo au siku nyingine je mko tayari kwa tarehe hiyo au la” aliwauliza na ukumbi wote ulilipuka kwa kelele na vifijo wakionekana kuiafiki tarehe hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kuondoka ukumbini hapo chini ya ulinzi mkali, Madega alisema yote hayo yamefanyika kutokana na shinikizo la mtu ambaye hakutaka kumtaja jina ila akiwaonya Yanga iko siku wataujutia uamuzi waliochukua.
“Nyie waandishi ndio wanafiki wakubwa, mnaniuliza niseme nini kuhusu mkutano na mlikuwapo kilichotokea si mmekiona lakini niwaonye wanachama wasije kuujutia uamuzi walioufanya leo siku za usoni” alisema huku akionekana kuwa mwenye kutaka kulia.
Wakizungumzia mwenendo mzima wa mkutano huo, baadhi ya wanachama waliozungumza na Mtanzania walisema kwa kiasi kikubwa umekwenda vizuri huku wengi wakionekana kufurahia kupangwa kwa tarehe ya uchaguzi.
“Mkutano ulikuwa mzuri, jambo ambalo sijaelewa vizuri ni kuhusu tarehe ya uchaguzi kwani awali Madega alitaka Julai 4, lakini kabla ya kumaliza vizuri alishikwa na hasira na kukatiza mkutano.
“Kabla ya Jaji Mkwawa kuamua kutangaza tarehe 27 Juni kwa uelewa wangu najua Mwenyekiti ndio mtu wa mwisho, lakini furaha yangu ni kufanyike uchaguzi” alisema Evance Matee ambaye anatarajia kuwania ujumbe katika klabu hiyo.

Wanachama wa Yanga, wakishangilia kwa staili ya pekeem ukumbini baada ya kutangazwa tarehe ya uchaguzi wa Klabu hiyo, ambao umepangwa kufanyika juni 27 mwka huu.

Kwakweli ilikuwa ni bonge la furaha ukumbini hapo kwa Wanacha wa Yanga, baada ya kutangaziwa tarehe rasmi ya kufanya uchaguzi, hapa wakishangilia kwa nfuvu zote.

Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega, akizungumza wakati wa mkutanoa huo ambapo kila alilokuwa akiongea ukumbini hapo alipingwa na wanachama kwa kupigiwa makelele, "Hatukutakiiii tokaaaaa"

Wanachama wakipiga kauli ya Madega ukumbini hapo....

Makamu wa kwanza wa Rais wa Shirikisho la Soka nchini, TFF, Athuman Nyamlani, akizungumza kwa niaba ya TFF, ukumbini hapo.

Wanachama wakishangilia na kufurahia baada ya kusikia kauli na maneno mazuri ya kuridhisha yaliyotolewa na Makamu huyo.

Wengine walikuwa wamejichokea tu jamani hata hawakutaka kushiriki katika makelele, bali walikuwa wkisubiri kitakachoamliwa ndicho wakifuate, kama huyu jamaa, anatamani mkutano uishe tu ili akajipatie tiketi yake asepe home....
Na sasa ilikuwa ni furaha tupu huku wengine wakimzomea Mwenyekiti huyo kwa kumwimbia, "Mwizi, Mwizi huyoooo, Mwizi Mwizi Huyoooo.......

Askari nao hawakuwa nyuma katika kufanya kile kilichowaleta ukumbini hapo, kwani baada ya kuona hali imezidi kuwa tete, walijipanga na kumuweka kati ili kumuhakikishia usalama wake wakati akitoka nje ya ukumbi huo....haka akiwa chini ya ulinzi mkali...

Wanachama bwana eti wameshasahau yaliyokuwa yakiwapigisha makelele ukumbini. Hapa ni Baadhi ya Wanachama wa Yanga, wakiruka ukuta kutoka ndani ya Ukumbi wa Maofisa wa Polisi Oysterbay baada ya kumalizika mkutano wa marekebisho ya Katiba ili kuwahi kupanga foleni ya kugaiwa tiketi za kuingia uwanja wa Taifa kushuhudia mchezo wa kirafiki baina ya Taifa Stars na Brazil.

Kila mmoja akijaribu kuwahi kuruka ukuta huo ili kuwahi tiketi hizo....

Hebu cheki hapa wengine wakiruka na wengine wakitimua mabio kuwahi foleni hiyo....

Hawa ni wale wenzangu na mie, kupanda kwao ilikuwa kaaaazi kweli kweli.........
Hili moja kati ya mabox, yaliyokuwa na tiketi hizo likiwa chini ua ulinzi wa askari....kabla ya kuanza kwa zoezi la ugawaji wa tiketi hizo..

Wanachama wa Yanga, wakiwa katika foleni ya kugaiwa tiketi zilizotolewa ofa na Mfadhili wa Yanga, Yusuph Manji, kwa ajili ya kushuhudia mchezo wa kirafiki baina ya Taifa Stars naBrazil unaochezwa leo kwenye uwanja wa Taifa jijini, baada ya kumalizika kwa mkutano wa marekebisho ya Katiba kwenye Ukumbi wa Maofisa wa Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam leo mchana.
"MAHOJIANO NA EVANCE MATEE ANAYEJIANDAA KUWANIA UJUMBE"
Waandishi wa habari, Rachel Mwiligwa (kulia) na Zaituni Kibwan, wakifanya mahijiano na mmoja kati wale waliojinadi kutaka kuwania nafasi za uongozi za uongozo katika Klabu ya Yanga, Evance Matee (katikati).









No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.