Menu

Tuesday, June 1, 2010

*MTOTO WA MIAKA 5 AZUA KIZAAZAA HEDARU, KITUO CHA POLISI CHACHOMWA MOTO




Na Sufianimafoto Reporter, jijini

JESHI la Polisi nchini limetoa onyo kali kwa wananchi wote wanaojichukulia maamuzi na sheria mkononi na kuahidi kuanza kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakao bainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Kauli hiyo ya Jeshi la Polisi nchini imetolewa na Mkuu wa Jeshi hilo, Said Mwema, wakati wa mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo mchana, alipokuwa akitoa taarifa ya kuchomwa moto kwa Kituo kidogo cha Polisi cha Hedaru wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro, kilichochomwa na wananchi wenye hasira kali.
Wananchi hao wenye hasira, waliamua kujichukulia hatua hiyo, baada ya kukamatwa kwa wakazi wanane wa mjio huo kwa mahojiano zaidi kutokana na tukio la kupotea kwa mtoto mdogo wa kike (5) Grace Kelvin, wakati akitoka shule, aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha.
Jenerali Mwema aliwaambia waandishi wa habari kuwa Mei 28 mwaka huu katika Kituo hicho cha Polisi kulilipotiwa taarifa za kupotea kwa mtoto Grace Kelvin mwenye miaka mitano ambapo askali walianza upelelezi mara moja,
Aliendelea kusema kuwa katika upelelezi huo, askali walipokea taarifa kuwa mtoto huyo alipelekwa katika kijiji cha Chome Mlimani karibu na msitu wa Shengena ambako kuna machimbo ya madini aina ya dhahabu kwa ikiaminia kuwa huenda alipelekwa kutolewa kafara kwa imani za kishirikina.
“Mei 31 mwaka huu askali kwa kushirikian na Mkuu wa kituo hicho waliingia katika msituni huo kwa lengo la kumtafuta mtoto huyo, lakini hawakufanikiwa, hatimaye waliwakamata watu nane akiwemo mwanamke mmoja waliokuwa na vifaa vya uchimbaji madini ya dhahabu kwenye mgodi usio rasmi” alisema.
IGP Mwema alisema kuwa wakati watuhumiwa hao nane wakiwa rumande katika Kituo hicho cha polisi kwa mahojiano zaidi baada ya kukutwa wakiwa na vifaa vya uchimbaji madini ya dhahabu katika mgodi usio rasmi, ghafra ulizagaa uvumi kwa wananchi kuwa watu hao ndio wanaohusika na upotevu wa mtoto huyo (grace).
“Baada ya uvumi huo, wananchi wapatao 300 walivamia kituo hicho na kukichoma moto kwa nia ya kutaka kuwaua watuhumiwa hao, lakini hata hivyo polisi walifanikiwa kuwatorosha watuhumi wao na hakuna yeyote aliyepoteza maisha katika tukio hilo” alisema.
”Licha ya wananchi hao kujichukulia hatua mkononi na kuamua kukichoma kituo hicho, leo asubuhi tumepata taarifa kuwa mtoto huyo amepatikana na amekwenda kuungana na familia yake, lakini hadi sasa tumefanikiwa kuwakamata watu watano waliohusika na uchomaji wa kituo hicho”.
“Nawaonya wananchi wote wenye tabia kama hizi waache mara moja kwani nchi haiwezi kuendeshwa kwa fujo na vitendo kama hivi kwasababu vinarudisha nyuma maendeleo ya nchi” alisema..
Kutokana na tukio hilo, Mkuu huyo wa jeshi la polisi hakusita kutoa wito kwa viongozi wa serikali, viongozi wa dini ikiwa ni pamojana viongozi wa vyama vya siasa kuchukua nafasi zao za uongozi kutoa elimu kuhusu kuheshimu utawala wa sheria na kuwezesha ustawi wa amani na usalama.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema, akizungumza wakati
wa mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana alipikuwa
akitoa taarifa za kituo kidogo cha Polisi cha Hedaru wilayani
Same kilichochomwa moto na wananchi wenye hasira Mei 28 mwaka
huu, kwa kile walichodai kuwateketeza waharifu waliomtoa kafala
mtoto mdogo aliyekuwa akitoka shuleni, aliyejulikana kwa jina la
Grace Kelivin (5) aliyetopotea katika mazingira ya
kutatanisha, ambaye baadaye aliweza kupatikana katika Soko la
Pasua.
Mwema akiendelea na mkutano huo.



No comments:

Post a Comment