Mdau wa Sufianimafoto je, uliwahi kusikia maajabu ya Kaburi hili la mtu maarufu katika fani ya waganga wa jadi Almaarufu Kiyeyeu? Eti Kakobe naye alitaka kujifananisha na mtu huyu kipindi Shirika la Umeme Tanesco likiwa katika harakati za kupitisha nguzo kubwa za umeme mbele ya Kanisa lake, ambapo aliibuka na kusema kuwa hata nguzo hizo zikipita mbele ya Kanisa hilo basi umeme hautawaka kamwe kwa miujiza na nguvu zake, kumbe haya yanawenyewe hebu pata kisa cha Kaburi hili japo kwa ufupi.....Kaburi la Kiyeyeu, lipo Njiapanda ya Mlolo pembezoni kabisa mwa barabara iendayo Mkoani Mbeya ukitokea Iringa lipo upande wako wa kulia, katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Hili ni kaburi alilozikwa mtu mmoja aliyekuwa Mganga maarufu wa jadi katika ukanda mzima wa maeneo ya mkoa huo, ambaye alifariki dunia miaka ya nyuma kidogo lakini hadi leo hii kaburi hilo ukiliona ni kama limejengwa jana.
Baada ya kufariki dunia mganga huyu, alizikwa kwa kufuata taratibu na mira za Machifu ambapo alizikwa kwa kusindikizwa na mtu aliye hai, aliyejitolea kwa ajili ya kuzikwa naye akiwa hai ili kumsindikiza, ambapo inadaiwa mtu huyo aliketi na kumpakata mganga huyo aliyezikwa huku akiwa amekaa.
Kaburi hilo limekuwa liwashangaza watu waliowengi na hata ndugu wa marehemu huyo kutokana na kuwa na maajabu na miujiza isiyoisha kana kwamba mtu huyo amezikwa mahala hapo jana.
Moja kati ya maajabu makubwa yaliyowahi kutokea mahala lilipo kaburi hilo ni wakati Shirika la umeme lilipokuwa katika zoezi la kuweka Nguzo za umeme pembezoni mwa barabara hiyo na kutokana na kaburi hilo kuwa karibu kabisa na barabara kubwa, Imedaiwa kuwa Tanesco walifanya mazungumzo na ndugu wa marehemu huyo ili wakubali kusogeza ama kuhamisha kaburi hilo ili kupisha zoezi la kuweka nguzo za umeme ili kupitisha umeme mahala hapo.
Imeelezwa baadhi ya ndugu hao walikubali baada ya mazungumzo hayo na kuwaruhusu Tanesco kuhamisha kaburi hilo, lakini zoezi la kuhamisha lilishindikana na walipojaribu kulibomoa hata nyundo haikuweza kufua dafu kubomoa hata sehemu ya tofali lililojenga kaburi hilo.
Ndipo ilipoamuliwa kuweka nguzo hizo na kupitisha nyaya za umeme kiubishi.
Lakini baada ya kumaliza zoezi hilo walishangazwa kwa kuona kuwa eneo la juu ya kaburi hilo hapakuwa ukipita umeme hali ya kuwa ulipoanzia hadi kabla na baada ya kaburi hilo umeme umejaa tele, ila eneo la juu ya kaburi hilo tu hakuna umeme.
Jambo hilo liliwafanya Tanesco kukubali matokeo na kuamua kuchukua uamuzi wa busara kwa kuhamishia baadhi ya nguzo hizo upande wa pili wa barabara ili kukwepa eneo hilo, hivyo nyaya hizo zikavuka barabara kabla ya kufikia kaburi hilo na baada ya kulivuka kaburi hili, na baada ya kufanya hivyo ummeme huo uliwaka na hadi hii leo unaendelea kuwaka, hivyo Serikali japo haiamini uchawi lakini hapa iliamini uchawi upo. Angalia picha hiyo katika alama nyekundu ndizo nyaya zilizovushwa kutoka upande wa pili kukwepa kaburi hilo.
No comments:
Post a Comment