Habari za Punde

*AIRTEL YADHAMINI BONANZA LA WAANDISHI SASA KUFANYIKA JUMAMOSI

Meneja Uhusiano wa kampuni ya simu za mkononi, Airtel Tanzania, Muganyizi Mutta (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO.

Na Sufianimafoto, Reporter jijini

KAMPUNI ya Airtel Tanzania imetangaza zawadi za washindi wa michezo tofauti zitakazotolewa katika tamasha la wanahabari litakalofanyika Jumamosi wiki hii katika viwanja vya TTCL Kijitonyama, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Meneja Uhusiano wa Airtel Muganyizi Mutta, alisema wameandaa zawadi za kuvutia katika kuongeza hamsa ya ushindani miongoni mwa vyombo vya habari vitakavyoshiriki michezo husika.

Pamoja na vikombe kwa washindi wa mpira wa miguu, pete, kuvuta kamba,kucheza dansi na kuimba lakini pia kutakuwa na zawadi za papo kwa papo kwa michezo mbalimbali ya kubahatisha itakayochezeshwa na kampuni hiyo ambapo pia kutakuwa na zawadi ya kombe kwa ajili ya mshindi wa jumla.

“Tumeandaa zawadi mbalimbali za kuvutia katika kuongeza hamasa na ushindani kwa washiriki lakini pamoja na hilo kutakuwa na zawadi za promosheni kwa michezo tofauti ya kubahatisha itakayochezeshwa na Airtel, yote hayo ni katika kuhakikisha kuwa watakaoshiriki wanaburudika kwa kiwango chake,” alisema Mutta.

Hii ni mara ya pili kwa kampuni ya Airtel iliyobadilishwa jina kutoka Zain kufanya tamasha kwa wanahabari ambapo tamasha la kwanza kama hili kwa wanahabari lilifanyika mwaka 2009.

Kwa upande wa burudani alisema bendi ya Msondo Ngoma “Baba ya Muziki” italipamba tamasha hilo na tayari bendi hiyo ipo kamili kuporomosha burudani katika siku hiyo ya aina yake kwa wanahabari nchini.

Kwa upande wake Mratibu wa tamasha hilo Mawazo Waziri wa kampuni ya Capital Plus International alisema maandalizi yamekamilika na kila kitu kipo katika mstari kusubiri siku ya tamasha ambapo alitoa rai kwa washiriki kuwahi ili ratiba ya michezo iweze kwenda kama ilivyopangwa.

“Wanahabari wamekuwa na mchango mkubwa katika shughuli mbalimbali za
kiuchumi na kijamii na hivyo Airtel imeona ni kitendo cha uungwana kuandaaa tukio hili maalum kwa wanahabari ambalo litawakutanisha na kuwaburudisha kupitia michezo”. alisema.

Kiongozi wa bendi hiyo Kibiriti aliwaahidi wanahabari burudani ya kipekee siku hiyo na kwamba wamedhamiria kudhihirisha kuwa wao ni ‘baba ya muziki’ wa kweli katika ulimwengu wa muziki wa dansi nchini.

“Tumefurahi kupata mwaliko wa kuwaburudisha wanahabari siku hiyo na sisi hatutafanya makosa tutatoa burudani ya kipekee na kudhihirisha kuwa hakuna mwingine kama msondo katika muziki wa dansi nchini,” alisema Kibiriti.
Mwimbaji na Rapa wa bendi ya Msondo, Roman Mng’ande, akiimba wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo, kuhusu bonanza la waandishi wa habari linalotarajiwa kufanyika jumamosi ya Februari 12 kwenye Uwanja wa Chuo cha Posta, Kijitonyama, chini ya Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel. Kulia ni Kiongozi wa bendi hiyo, Said Mabela.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.