Habari za Punde

*MUATHIRIKA WA UKIMWI AFIA GESTI DAR

Katambulisho cha marehemu kilichokutwa ndani ya mkoba wake.
Na Sufianimafoto Reporter, jijini
KATIKA hali ya kutatanisha, msichana mmoja aliyetambulika kwa jina la Amina Ramadhan, amekutwa amekufa katika chumba cha nyumba ya kulala wageni ijulikanayo kwa jina la Mkomboni Bar & Guest House, iliyopo Mtaa wa Mkunguni Kata ya Hananasifu jijini Dar es Salaam juzi usiku.

Msichana huyo aliyekutwa na Kitambulisho cha Ubungo High School, kinachomuonyesha kuwa amemaliza elimu ya Sekondari katika shule hiyo mwaka 1997, pia amekutwa na Cheti kinachomuonyesha kuwa ni muathirika wa Ugonjwa wa Ukimwi aliyekuwa akitumia dawa za kurefusha maisha.

Akizungumza na Gazeti hili mhudumu wa Gesti hiyo, Lydia Paul, alisema kuwa alimpokea msichana huyo juzi majira ya saa kumi jioni akiwa ameongozana na mwanaume na kufika eneo la baa na kuagiza soda.

“Baada ya muda msichana yule msichana aliingia ndani na kutoa noti ya Sh. 10,000, ili apatiwe chumba, na baada ya kumaliza taratibu za kulipia na kuandika jina lake pekee alirudi nje na kumchukua mwanaume huyo na wakaingia chumba hicho namba sita pamoja,

Kwa kipindi hicho chote hatukuweza kusikia kelele hadi jioni walipotoka na kuingia bafuni kwa ajili ya kuoga na kurejea tena ndani, hadi ilipofika mida ya saa moja jioni, yule jamaa alitoka na kutuaga kuwa anakwenda kumnunulia chakula mwenzake,

Alipoondoka nilikuwa nikitoka nje na ndipo nikaona mlango huo ukiwa wazi nikajaribu kumuita yule binti ili aurudishie mlango, lakini akawa kimya na nilipojaribu kugonga bado akawa kimya ndipo nikaingia ili kumuamsha nikijua amepitiwa na usingizi, lakini baada ya kuingia nikamkuta akiwa amejifunika gubi gubi na kanga huku mikono yake ikiwa nje,

Kila nilipojaribu kumuamsha hakuweza kuitika, nikawaita wenzangu tukaanza kumpepea baada ya kumfunua na kumuona kuwa hatingishiki tukijua amezimia, na ndipo tukaamua kwenda kutoa taarifa katika kituo kidogo cha Mkunguni hadi saa nne usiku askari walifika na kumpekuwa na kuchukuwa mwili huo” alisimulia Lydia.

Nao baadhi ya mashuhuda ambao hawakupenda kutaja majina yao, walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa kwa siku tatu zilizopita katika gesti hiyo hiyo, walimuona mdada mmoja akitoka mbio ndani huku akipiga makelele.

“ Siku kama tatu zilizopita tulimuona mwanadada akitoka mbio humo ndani huku akipiga kelele na akiwa na nguo zake mkononi, na majuzi pia tulipata stori kuwa jamaa huyo huyo aliyeingia na marehemu, aliingia na mdada mwingine lakini walipoondoka katika chumba chao zilikutwa damu zilizokuwa zimetapakaa” alisimuliwa mmoja wa mashuhuda.

Akizungumza na gazeti hili Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kufika eneo la tukio juzi usiku na kumkuta marehemu.

Aidha alisema kuwa baada ya kumpekuwa marehemu huyo walimkuta na kitambulisho cha Ubungo High School kinachoonyesha kuwa alianza kidato cha kwanza katika shule hiyo, 1996 na kumaliza 99, pamoja na cheti cha kuchukulia dawa za kurefusha maisha katika kituo cha Hospitali ya Sinza.

“Katika cheti hicho kilichokuwa na namba 002061, kilionyesha tarehe ya mwisho kuchukua dawa katika kituo hicho ilikuwa ni Januari 26 mwaka huu na alitakiwa kurudi kuchukuwa tena dawa hizo Februari 24 mwaka huu,

Na pia alikutwa pembeni yake kukiwa na mipira miwili ya kimue na mmoja ukiwa umetumika” alisema Kenyela
Gari la Polisi lililobeba mwili wa marehemu likiwa nje ya Gesti hiyo jana usiku, lilipofika kuchukua mwili wa marehemu.
Askari wakisaidia na raia wa mtaa wa Mkunguni, kumbeba marehemu Amina Ramadhan, aliyekutwa amekufa katika chumba namba 6 cha nyumba ya kulala wageni inayojulikana kama Mkomboni Bar & Guest House jana usiku baada ya kuingia katika nyumba hiyo akiwa ameongozana na mwanaume ambaye hakuweza kufahamika jina lake, ambaye pia alitoweka huku akiwaaga wahudumu kuwa anakwenda kumnunulia chakula mwenzi wake huyo (marehemu) na kutokomea kusikojulikana.
Mhudumu wa Gesti hiyo, Lydia, akitandika kitanda kilichotumiwa na marehemu, baada ya kuondolewa.




No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.