Habari za Punde

*AURORA SECURITY YAPIGA TAFU UZINDUZI WA MASHINDANO YA 'DAR SECONDARY SCHOOL CUP'

*NI YA VIJANA CHINI YA UMRI WA MIAKA 16

*YASHIRIKISHA SHULE 6 ZA KINONDONI


*WAZAZI WAHIMIZWA KUJITOKEZA KWA WINGI


Na.Mwandishi wetu


KAMPUNI ya ulinzi ya Aurora Premium Outlet Security (T) Ltd, Security ya jijini Dar es Salaam, imedhamini ufunguzi rasmi wa mashindano ya mchezo wa soka ya 'DAR SECONDARY SCHOOL CUP'.


Mashindano hayo yanayoshirikisha timu za vijana wa shule za sekondari wenye umri chini ya miaka 16 yamezinduliwa rasmi leo katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.


Mashindano hayo yameandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Upendo Youth Development Organization – UYODEO lenye makao yake makuu huko Kilwa – Masoko.


Akizungumza na MO BLOG Mjumbe wa Heshima wa UYODEO na Mratibu wa mashindano hayo Annick Verstraelen amesema lengo kuu la mashindano hayo ni kuwakutanisha pamoja wanafunzi kutoka shule mbali mbali chini ya kauli mbiu ya ‘TUCHEZE PAMOJA’ ili waweze kufahamiana, kushiriki michezo pamoja na kujenga uhusiano.


Amefafanua kuwa mashindano hayo pia yanalenga kutafuta, kukuza na kuvitumia vipaji miongoni mwa wanafunzi ili waweze kujitambua wakiwa bado katika umri wa kukua.


Mashindano hayo mwaka huu yamehusisha timu za shule sita (6) kutoka wilaya ya Kinondoni, lakini ni matarajio ya UYODEO kupanua wigo ya mashindano hayo na kufanyika pia katika wilaya za Ilala na Temeke.


Akizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo katika kuandaa na kufanikisha mashindano hayo, Annick amesema uhaba wa fedha umekuwa ni kikwazo kikubwa kutokana na gharama za maandalizi kuwa kubwa ikilinganishwa na uwezo wa shirika hilo, hivyo ametoa wito kwa wadhamini kujitokeza ili kuwezesha mashindano hayo kufanikiwa kwa kiwango kilichokusudiwa.


Aidha Annick ametoa wito kwa wazazi kujitokeza kwa wingi kuja kushuhudia mashindano hayo, ili waweze kujionea nini watoto wao wanafanya uwanjani na kuweza kuwapa moyo na kuwaunga mkono ili waweze kutimiza malengo yao katika michezo, kwani michezo ni afya.


Shule za Sekondari za wilaya ya Kinondoni zinazoshiriki mashindano hayo ni Kinondoni Muslims, Salma Kikwete, Makongo Sekondari, ESACS, Mtakuja Beach na DIS.


Shule hizo zimepangwa katika makundi mawili yenye timu tatu kila moja, ambapo kila shule itapaswa kucheza mechi mbili katika mfumo wa ligi.


Kundi la kwanza lina timu za shule za Mtakuja Beach, DIS na Kinondoni Muslim wakati kundi la pili lina timu za Salma Kikwete, Makongo na ESACS.


Mechi za ligi ya mashindano ya DAR SECONDARY SCHOOL CUP zitafanyika tarehe 30 April na tarehe Mosi Mei 2011.


Kwa upande wa udhamini makampuni yaliyojitokeza kudhamini kwa namna moja ama nyingine kuwezesha ufunguzi wa mashindano hayo ni pamoja na Aurora Premium Outlet Security (T) Ltd, Image Masters, Continental, MO BLOG –More Benefits, PPF na Azam Football Club.


Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Esacs wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza mchezo wao wa kwanza leo.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mtakuja wakiwa katika picha ya pamoja viwanjani hapo leo.






No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.