Habari za Punde

*VIJANA WA CHADEMA WAMGEUKIA NAPE

Wagombea wa nafasi mbali mbali ndani ya baraza la vijana wa chama cha Chadema (BAVICHA) Taifa, Aidan Pugili (30) (kulia) anayegombea nafasi ya uenyekiti Taifa na Dennis Tesha, anayegombea ujumbe wa Baraza kuu Vijana Taifa wakizungumza leo na kupinga tambo za katibu wa itikadi na uenyezi wa CCM, Nape Nnauye dhidi ya kuwabana mafisadi ndani ya CCM.

********************************************************


Na Francis Godwin, Iringa


VIJANA wa chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) mkoani Iringa wameibuka na kumvaa katibu wa itikadi ya uenezi wa chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Nape Nnauye kuwa hana uwezo wa kuzima moto wa viongozi wakuu wa Chadema dhidi ya ufisadi na kuwa CCM imemtumia Nnauye kucheza ngoma ya Chadema bila kujijua.


Wamesema kuwa wanamtaka Nnauye, kuanza kumwandikia barua ya kujivua gamba naibu katibu mkuu wa CCM bara kepteni (mstaafu ) John Chiligati mtoto mmoja wa Kigogo nchini ambaye amekuwa ni mmoja kati ya mamilionea wakubwa nchini.


“Ujue sehemu kubwa ya wanaovuliwa magamba ndani ya CCM ni wale ambao viongozi wa juu wa Chadema akiwemo Dr.Slaa na Mbowe wamekuwa wakiwataja mara kwa mara kuwa ni mafisadi na wale ambao kila mtanzania anawajua hivyo hata Nnauye na CCM yake watakapowaandikia barua hakuna mtanzania wa kushangaa juu ya uamuzi huo kwani hawa ndio waliogeuzwa kondoo wa kafara ndani ya CCM ila wapo wenyewe ambao hawaguswi kabisa”


Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi leo wakati wakitangaza azma yao ya kuwania nafasi ya uongozi ndani ya baraza kuu la vijana wa Chadema (BAVICHA) Taifa vijana hao Aidan Pugili ambaye anagombea nafasi ya uenyekiti Taifa na ujumbe wa baraza kuu Taifa na Dennis Tesha (19) ambaye anagombea ujumbe wa baraza kuu la vijana Taifa ,walimtaka Nnauye kuacha kuwafanya watanzania kana kwamba hawajui lolote dhidi ya ufisadi wa CCM katika Taifa hili.


Walisema kuwa watanzania wa sasa si wale wa miaka ya 1990 na 1980 wakati wa chama kimoja na kuwa iwapo CCM itaendelea kumtumia Nnauye kama sehemu yake ya kutaka kujijenga itakuwa inajimaliza yenyewe na kuwa yawezekano kabla ya uchaguzi mkuu mwaka 2015 CCM isifike baada ya kuwa imepasuka mapande mapande.


Pugili alisema kuwa pamoja na ziara za viongozi wapya wa CCM ambao wamekuwa wakizunguka mikoani na kufika ndani ya mkoa wa Iringa kwa lengo la kujiosha bado imani ya watanzania dhidi ya CCM imekwisha na hivyo ziara hizo ni sawa na kuendelea kujichafua na kutoa umaarufu kwa Chadema ambao ndio waanzilishi wa vita dhidi ya upinzani.


Hata hivyo alisema kuwa lengo la kuwania nafasi hiyo ni kutaka kuwaunganisha zaidi vijana ndani ya Chadema na wale waliopo CCM ili kujiunga na Chadema kwa lengo la kuongeza nguvu zaidi ya katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 ili kuona Chadema kinakuwa chama tawala na CCM inaingia katika orodha ya vyama vya upinzani nchini.


No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.