Kiongozi wa kundi lijulikanalo kama ''Invisible Commandos'' Ibrahim Coulibaly, aliuawa katika shambulio la jumatano kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Ulinzi.
Vikosi vya Bw.Coulibaly vilimsaidia Bw.Outtara katika juhudi za kudhibiti sehemu za mji mkuu Abidjan wakati wa mgogoro wa hivi karibuni.
Coulibaly ameshiriki majaribio kadhaa ya kuipindua serikali katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Mwaka 2002 alikuwa chachu katika mgogoro ulioigawa nchi mapande mawili hadi vikosi vya Bw.Outtara vilipompindua aliyekuwa Rais Laurent Gbagbo majuma mawili yaliyopita.
Akiwa mwenye umri wa miaka 47 na maarufu kama ''IB'' alikua mlinzi mkuu wa Bw.Outtara lakini hakutaka kusalimisha silaha zake akitaka kama wadadisi wengi walivyodhani akisubiri mchango wake katika vita vya kumuondoa Gbagbo ukubalike.
Mwandishi wa BBC mjini Abidjan, John James anasema kuwa kifo cha Bw.Coulibaly kitaondoa uwezekano wa kutokea kwa ghasia na kuikosesha utulivu serikali mpya.
Hata hivyo mwandishi wetu anasema kuwa mvutano wa ndani miongoni mwa washirika kutoka makundi ya wababe wa vita uliomuweka Rais Outtara madarakani bado unaleta wasiwasi.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi Capt Leon Alla Kouakou alielezea shirika la habari AFP kuwa aliiteka familia moja kufuatia hatua ya vikosi vya Bw.Outtara kumtaka asalimishe silaha zake.
Vikosi vya Ouattara vilipofyatua risasi za kumuonya alijibu kwa kutumia silaha nzito na walipojibizana kwa moto ndipo akauawa pamoja na wapambe wake.
Serikali ilipoteza askari wawili na Bw.Coulibaly kuuawa na wapiganaji wake sita katika mapigano yaliyofanyika katika kitongoji cha mji mkuu Abidjan kijulikanacho kama PK18 katika wilaya ya Abobo.
No comments:
Post a Comment