SAKATA la diwani wa chama cha mapinduzi (CCM) kata ya Mgama wilaya ya Iringa vijijiini Denis Lupala (pichani)ambaye alimvaa Naibu katibu mkuu wa CCM bara Kepten John Chiligati na kumwita fisadi huku akimtaka kuvua gamba ndani ya CCM limezidi kuiweka pabaya CCM baada ya uongozi wa CCM kumsimamisha uanachama wake ndani ya Chama hicho.
Hatua ya CCM kumwandikia barua ya kumsimamisha uanachama imekuja zikiwa ni siku chache toka diwani huyo kumvaa Chiligati wakati wa ziara yake katika kata ya Mgama na kumhoji sababu ya CCM kujigamba kujivua gamba wakati kati ya watu waliokuwemo katika orodha ya kuvuliwa magamba wakiendelea kupewa uongozi ndani ya chama hicho akiwemo Chiligati mwenyewe.
Habari za uhakika kutoka ndani ya CCM zinathibitisha kusimamishwa kwa diwani huyo ambapo kikao cha sekretarieti /usalama na maadili ya CCM wilaya ya Iringa vijijini kilichoketi April 26 mwaka huu kilimwandikia barua hiyo ya kumkabidhi katibu wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Iringa vijijini ili kwenda kumkabidhi rasmi diwani huyo.
Chanzo hicho cha habari kilidokeza kuwa kusimamishwa uanachama kwa diwani huyo kumetokana na CCM wilaya ya Iringa kuagizwa na uongozi wa juu wa chama hicho kuhakikisha diwani huyo anashughulikiwa ama kufukuzwa kabisa ndani ya CCM kwa kuhofia kuumbuliwa mambo yao.
Kuwa CCM imekuwa ikihofia tabia ya diwani huyo ya kutowaogopa viongozi wa kitaifa na kuwa kabla ya kumvaa naibu katibu mkuu huyo inadaiwa kuwa diwani huyo tayari alikuwa amewachomea viongozi wa wilaya hiyo kwa mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Jakaya Kikwete akilalamikia kuchakachuliwa kwa vocha za ruzuku na utendaji mbovu wa viongozi wa CCM wilaya hiyo.
Hata hivyo inadaiwa wajumbe wa kikao hicho cha kamati ya maadili kilimwangiza katibu wa CCM wilaya ya Iringa vijijini Mohamed Dhikri kuandika haraka barua kwa diwani huyo ili kumsimamisha rasmi uanachama wake.
Kwa madai ya kuchoshwa na uchokonozi wake ambao amekuwa akiufanya kwa kutowaogopa viongozi wa chama na kutozingatia mipaka ya nafasi yake kama diwani na mwanachama wa CCM.
Pia wajumbe hao walidai kuwa katika kikao hicho ambacho walitaka jambo hilo kuwa siri na lisitolewe kwa vyombo vya habari kwa sasa kama njia ya kuepuka makombora zaidi kutoka kwa diwani huyo ,bado walidai kuwa wanafanya utaratibu wa kumwandaa mwanachama mwingine wa kugombea udiwani kata hiyo ambayo kimsingi baada ya CCM kumsimamisha diwani huyo itakuwa haina uwakilishi .
Mtandao huu ulipomtafuta katibu wa CCM wilaya ya Iringa vijijini Mohamed Dhikri ili kuthibitisha habari hiyo ya kusimamishwa kwa diwani huyo hakuweza kupokea simu yake zaidi ya kuishia kuita .
Diwani huyo alipotafutwa na mtandao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com kwa njia ya simu alithibitisha kukabidhiwa barua ya kusimamishwa kwake na kuwa kwa sasa yeye ataendelea kuwa diwani na hajutii kusimamishwa kwake na CCM.
Lupala ambaye pia alipata kumvaa mbunge wa jimbo hilo Dr .Wiliam Mgimwa kwa madai ni tatizo katika jimbo hilo la kalenga kutokana na kuendelea kuendeleza makundi ya kura za maoni bado alisema kuwa mwenye jukumu la kumvua udiwani ni wapiga kura wa kata hiyo ya Mgama na sio chama na kuwa anachotambua yeye kwa sasa si mwana CCM ila ni diwani wa kata hiyo ya Mgama. Imeripotiwa na Francis Godwin, Iringa
No comments:
Post a Comment