Habari za Punde

SERIKALI YAPANIA KUIMARISHA VITUO VYA VIJANA

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bw. Sethi Kamuhanda akipata maelezo kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Kituo cha Maendeleo ya Vijana Ilonga, Bw. Ombeni Andrew kuhusu Kompyuta zinazotumika kufundishia mafunzo ya TEKNOHAMA kituoni hapo. Bw. Kamuhanda alitembelea Kituo hicho mwanzoni mwa wiki hii kwa ajili ya kukagua maendeleo ya kituo hicho.

Na Concilia Niyibitanga-Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo

Serikali imedhamiria kuviimarisha na kuvijengea uwezo vituo vya vijana ili viweze kutoa mafunzo kwa vijana wengi zaidi hali ambayo itasaidia vijana kujiajili na kujipatia kipato pamoja na kuliendeleza Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bw. Sethi Kamuhanda alipotembelea Kituo cha Maendeleo ya Vijana Ilonga kilichopo wilayani Kilosa Mkoani Morogoro.

“Lengo kubwa la Serikali kuanzisha vituo vya vijana ni kutaka vitoe mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana ili wawe na uwezo wa kujiajiri na kujitegemea.” Amesema Bw. Kamuhanda.

Aidha, Bw. Kamuhanda amesema kuwa Serikali imedhamiria kuimarisha Mfuko wa Vijana ili vikundi vingi zaidi vya vijana viweze kukopeshwa kwa ajili ya kufanikisha shughuli za kiuchumi na kutokomeza umaskini.

Amesema kuwa kwa sasa Mfuko huo unatoa mikopo kwa vikundi vya vijana kupitia saccos zilizoainishwa na halmashauri ambazo vikundi hivyo vinatokea lakini bado hautoshelezi mahitaji kwani fedha inayotengwa kwenye mfuko huo ni ndogo ukilinganisha na mahitaji yaliyopo.

Naye Kaimu Mkuu wa Kituo cha Maendeleo ya Vijana Ilonga, Bw. Ombeni Andrew amesema kuwa Kituo hicho kinatoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana, utunzaji wa mazingira, masuala yanayohusu VVU/UKIMWI na mafunzo ya Teknolojia ya habari na mawasiliano.

“Lengo hasa la kuanzisha somo la Teknolojia ya habari na mawasiliano (TEKNOHAMA) chuoni hapo ni kutaka vijna kupata habari mbalimbali zinazohusu vijana hususan zile zinazohusu masuala ya UKIMWI kupitia mtandao wa intaneti ili wawe na uwezo wa kujikinga na ugonjwa huo”. Amesema Bw. Andrew.

Ameeleza kuwa vikundi mbalimbali vya vijana vimekuwa vikifika kituoni hapo kwa nyakati tofauti kulingana na mahitaji ya wakati huo na wamekuwa wakiwapatia mafunzo ya ujasiriamali na wakati mwingine uzarishaji mali kama vile kutengeneza mkaa wa nyasi ambao husaidia kutunza mazingira.

Akielezea namna wanavyowahudumia vijana wanaofika chuoni hapo kwa ajili ya kujifunza, Bw. Andrew amesema kuwa Kituo kina mabweni yenye uwezo wa kulaza vijana 48 na chakula kinapikwa hapo kituoni kwa ajili ya wanafunzi.


Kaimu Mkuu huyo wa kituo ametoa wito kwa Serikali kuanzisha programu za mafunzo nyingi zaidi na kutafuta watumishi sahihi na wa kutosha kwa ajili ya kuendesha mafunzo hayo.

Kituo cha Maendeleo ya Vijana Ilonga ni moja kati ya vituo vitatu vya maendeleo ya vijana ambavyo viko chini ya usimamizi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Vituo vingine ni Sasanda kilichopo wilayani Mbozi Mkoani Kilimanjaro na Kituo cha Vijana Marangu cha Mkoani Kilimanjaro.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.