Raia mmoja wa Afrika Kusini ameamka na kujikuta kwenye chumba cha kuhifadhia maiti mwishoni mwa wiki iliyopita na kuanza kupiga kelele za kuomba msaada akitaka atolewe, jambo lililowaogopesha wahudumu wakidhani ni mzimu.
Familia ya jamaa huyo ilidhani amekufa baada ya kushindwa kumwamsha wakati amelala Jumamosi usiku na kuwasiliana na ofisi moja yenye vyumba vya kuhifadhia maiti ya mtu binafsi katika kijiji kimoja mjini Eastern Cape.
Msemaji wa idara ya afya mjini humo aliliambia shirika la habari la Sapa kuwa jamaa huyo alihifadhiwa ndani ya chumba hicho kwa muda wa saa 24 kabla ya kuzinduka na kuanza kupiga kelele.
Wahudumu hao baadae walirejea na kupiga simu kuita gari la wagonjwa, mtu huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, alitibiwa hospitalini kwa kukosa maji mwilini.
Msemaji wa idara ya afya ya Eastern Cape, Sizwe Kupelo, alisema, "Daktari walimfanyia uchunguzi na kuona kuwa anaendelea vizuri." alisema msemaji huyo na kuongeza kuwa hakuhitaji matibabu ya ziada.
Aidha Kupelo alisema kuwa mtu huyo aliamka saa tisa za Afrika Mashariki siku ya Jumapili, akitaka kutolewa kwenye chumba hicho chenye baridi kali kwenye kijiji cha Libode, na kuwatisha wahudumu waliokuwa zamu.
Bw Kupelo alisema, "Mwanzo watu hao walikimbia kwa kasi." wakiondoka eneo hilo la chumba cha kuhifadhia maiti.
Maofisa wameusihi umma kuwasiliana na madaktari au wanaotoa huduma za dharura ili waweze kumtangaza mtu kufariki dunia kabla ya kuwaita wahudumu wa vyumba vya kuhifadhi maiti.
Bw Kupelo alihoji kuwa "Unaanza kujiuliza ni watu wengine wangapi waliokufa kwa namna hiyo katika chumba cha kuhifadhia maiti."

No comments:
Post a Comment