Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Amos Makala, akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Kinyenze, Kijiji cha Kipera, Tarafa ya Mlali, Wilaya ya Mvomero, Morogoro mwishoni mwa wiki katika harakati za kutatua mgogoro wa ardhi uliopo kijijini hapo, kufuatia mwekezaji Raia wa kigeni kuuziwa eneo kubwa la ardhi na kumega sehemu ya mashamba yao na kufunga barabara, shule na kubomoa baadhi ya vyoo vya wakazi wa kijiji hicho. Picha na Mroki Mroki
Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Mkoani Morogoro, Amos Makala (kushoto) akikagua uzio uliowekwa na Kampuni ya Tanbreed Poultry Limited inayomilikiwa na Mzungu aliyenunua shamba Kitogoji cha Kinyenze, Kijiji cha Kipera, Tarafa ya Mlali, Wilaya ya Mvomero na kuzua mgogoro mkubwa wa mipaka baina yake na wananchi wa eneo hilo. Anayemuongoza ni Said Ahmad mkazi wa Kinyenze.
Wananchi wa Kitongoji cha Kinyenze, Kijiji cha Kipera, Tarafa ya Mlali, Wilayani Mvomero, wakiwa katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Amos Makala aliyefika kijijini hapo mwishoni mwa wiki kufuatilia mgogoro wa ardhi ulipo kati ya wananchi hao na mwekezaji raia wa kigeni aliyenunua shamba kijijini hapo na kuweka uzio na kufunga njia na mashamba yao.
***********************************************************
*Atoa wiki moja maofisa ardhi kumaliza tatizo au kutinga Mahakamani
Na Mroki Mroki, Mvomero
MBUNGE wa jimbo la Mvomero, mkoani Morogoro, Amos Makala, ameingilia kati mgogoro wa ardhi uliopo baina ya Mwekezaji na Wananchi wa Kitongoji cha Kinyenze , Kijiji cha Kipera, Tarafa ya Mlali , Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.
Akizungumza mwishoni mwa wiki Kijijini hapo, Makala aliyeambatana na Ofisa Ardhi wa Wilaya hiyo, Majaliwa Jaffari ameiagiza idara ya ardhi kuchukua hatua za haraka na dharula kutatua mgogoro huo kabla ya kuibuka kwa machafuko ya uvunjifu wa amani.
“Nimejionea mwenyewe baada ya kusikia kilio chenu juu ya mwekezaji huyu, watu wa ardhi tafadhalini sana lishughulikieni suala hili haraka sana na mkae pamoja mgogoro huu umalizike upesi iwezekanavyo, ndani ya wiki moja tatizo hili liwe limemalizika”, alisema Makala.
Aidha Makala amesema tatizo hilo likiendelea ataungana na wananchi wake kufungua kesi Mahakamani ili kumpinga mwelezaji huyo na amemwomba Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero kutumia mamlaka waliyonayo kufika kijijini hapo na kufungue uzio huo uliowekwa na mwekezaji huyo haraka ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji na watoto kwenda shule na watu kuvuna mazao yao yanayoibiwa na walinzi wa kampuni ya Tanbreed Poultry Limited ambayo imemega mashamba yao.
“Katika hili ninaungana nanyi na ninawaomba Viongozi wa Mkoa na Wilaya wafike hapa wakiwa chini ya usimamizi wa dola na kukata uzio huu, ili wananchi muendelee na shughuli zenu za kijamii, si haki kufunga barabara mnayoitumia kwenda katika makazi yenu na mashambani, hili lisipofanyika tutatafuta mwanasheria na kufungua kesi Mahakamani ya kumpinga mwekezaji huyu”,alisema Mbunge Makala.
Makala pia aliwapongeza wakazi wa kijiji hicho kwa kuwa watulivu pasipo kufanya vurugu katika kipindi kirefu tangu kuibuka kwa mgogoro huo bila kupatiwa ufumbuzi kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu licha ya kuandikiwa barua tangu mwezi Aprili mwaka huu mgogoro huo ulipoanza kushika kasi.
“Wananchi mmefanya jambo jema sana la kuheshimu mamlaka za kisheria kwa kuwa watulivu kipindi chote lakini vinginevyo hapa kungeshamwagika damu na machafuko makubwa yangetokea maana wananchi mpo wengi kuliko hao askari wao wanaolinda hilo shamba”, alisema Makala.
No comments:
Post a Comment