Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha Rose Migiro, akizungumzia umuhimu wa Taifa kusimamia haki ya mtoto ya kuishi kwa amani na furaha bila kufanyiwa Ukatili wa aina yoyote, wakati wa Kilele cha uzinduzi wa ripoti ya Utafiti na Mpango wa Kitaifa wa kushughulikia "Ukatili kwa Watoto" na mpango wa Udhibiti wa Taifa.
************************************
HOTUBA
Ninayo furaha kubwa sana kuwa hapa pamoja nanyi leo hii katika tukio hili muhimu na la kihistoria kama alivyosema Mheshimiwa Sophia Simba.
Lakini nina furaha ya pekee kuwa miongoni mwenu kwa sababu mimi ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa niliyetokana na nchi hii nzuri.
Napenda awali kuchukua fursa hii kuishukuru taasisi ya kuthibiti magonjwa ya Marekani - Centre for Disease Control na pia kukishukuru Chuo Kikuu cha Muhimbili kwa kuendesha utafiti huu wa kipekee.
Nawapongeza pia wataalamu wote walioshiriki uchunguzi huu unaofungua ukurasa mpya wa sayansi.
Aidha naipongeza Serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuunga mkono juhudi zao na kutoa hadharani matokeo ya uchunguzi huo.
Kwa uzinduzi huu tunaandika historia kwani haijawahi kutokea katika Afrika nzima; kufanyika utafiti na uzinduzi unaoibua ushahidi kama huu unaoonyesha jinsi unyanyasaji wa watoto wa kike na wa kiume ulivyoenea katika jamii yetu.
Takwimu zilizopatikana zinaonesha unyanyasaji wa watoto katika sura zake zote, iwe ni kupigwa, kutukanwa, kusimangwa au kunajisiwa.
Na tumeona hapa hata kubebeshwa mizigo mizito.
Takwimu hizi zinatia huzuni, lakini ni lazima tuzitazame na tuzitizame kwa macho mawili na kuzitafakari ili tuweze kubuni njia madhubuti za kukabiliana na unyanyasaji huo.
Ili tuweze hatimaye kukomesha kabisa unyama huu, ni lazima tufahamu kiini na ukubwa wa tatizo lenyewe.
Ufahamu huo utapatikana kwa kuwa makini katika ukusanyaji wa takwimu, kufanya uchambuzi wa kina na kuzungumzia kwa uwazi yale tunayoyabaini kutokana na uchambuzi huo.
Aidha tutakapokuwa tumeng’amua kiini cha tatizo tutaweza kutunga sera zitakazotuwezesha kubuni mikakati imara ya kukomesha tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji.
Kwa kuwa tunayo dhamira ya dhati ya kulinda maslahi ya watoto wetu, yote hayo yanawezekana.
Umoja wa Mataifa unaona fahari kuwa unasimamia haki ya mtoto ya kuishi kwa amani na furaha bila kufanyiwa ukatili wa aina yeyote ile.
Tanzania ni moja ya nchi zilizomo katika kampeni ya Umoja wa Mataifa ya kukomesha ukatili kwa watoto.
Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Mtoto ulipitishwa mwaka 1990, na Tanzania ilijiunga mara mojakatika mwaka huo huo mkataba ulivyopitishwa.
Naipongeza Tanzania kwa hatua hii muhimu na natumaini Mheshimiwa
Sophia Simba utafikisha ujumbe huu muhimu kwa viongozi wa taifa letu.
Kwa upande wetu, Umoja wa Mataifa umejitahidi sana kushughulikia suala hili kwa kusaidiana na watu mbali mbali miongoni mwa wataalamu na watetezi wa haki za watoto pamoja na mashirika mengine ya Umoja huu.
Tumejitahidi kwa nguvu zetu zote kukabiliana na jukumu hilo zito la kukomesha ukatili kwa watoto.
Ndio maana, nimepata ari kubwa kuona kuwa Tanzania nchi yangu mwenyewe inachukua hatua madhubuti kukomesha ukatili kwa watoto.
Tukumbuke kuwa hapa Tanzania nusu yake ni watoto. Watoto ni hazina kubwa ya taifa hili kwani wao ndio kiungo kati ya kizazi na kizazi katika uhai wa taifa.
Kwa hiyo basi tukiwalea na kuwalinda watoto wetu kwa jicho la huruma na mapenzi tutakuwa na uhakika wa kujenga taifa lenye kusimamia haki na ustawi wa watu wake wote.
Aidha wahenga walisema kuwa watoto wa leo ndio viongozi wa kesho, basi tutayarishe viongozi watakaokidhi utashi huo.
Ndugu zangu, mtoto anayeishi kwa wasiwasi, akihofia kuwa wakati wowote anaweza kupigwa, kusimangwa au kunajisiwa, hatakuwa na maendeleo mazuri shuleni kwa sababu atakosa utulivu unaotakiwa katika kufuatilia masomo.
Aidha mtoto huyo atakuwa hana imani na mtu yeyote, atakuwa anamshuku kila mtu kuwa anaweza kumdhuru.
Mtoto anayeishi kwa wasiwasi wa kutokuwa na uhakika wa usalama wake, atakuwa kila wakati yuko katika hali ya kutaka kujihami dhidi ya jamii ambayo anaiona haimtendei haki wala haimlindi anapohitaji ulinzi.
Aghalabu kujihami huku kunachukua sura ya utovu wa nidhamu au uasi kwa jamii.
Mabibi na mabwana, ripoti hii inatuonesha mambo ya kustuwa kweli kweli. Kuna taarifa za kukithiri kwa ubakaji.
Tunaambiwa kuwa katika kila wasichana kumi, kuna wasichana watatu waliobakwa kabla hata hawajafikia umri wa miaka 18.
Wasichana hawa ndio tunawategemea kuwa wazazi na viongozi wa taifa hapo baadaye, tutarajie nini basi wanapotendewa uovu kama huu? Wanaweza wakapata athari za kisaikolojia kiasi kwamba itakapofika wakati wao wa kuwa
wazazi, wakawa na woga wa kudumu kuhusu masuala ya kujamiiana na afya ya uzazi.
Isitoshe, katika hizo harakati za kubakwa msichana anaweza kuambukizwa Virusi ya Ukimwi - VVU au magonjwa mengine ya aina hiyo.
Ni dhahiri kwamba tunalo jukumu la kukomesha kwa nguvu zetu zote ukatili wa kubaka na kunajisi vijana wetu wa kike na wa kiume.
Kwa mujibu wa utafiti mbali mbali, na kama nilivyokwishasema vitendo hivyo ndio njia kuu ya kuenea kwa VVU na UKIMWI wenyewe na magonjwa megine
yanayoambukizwa ka njia ya kujamiiana hapa Tanzania.
Ndani ya ripoti hii tunayoizindua leo, zimo pia taarifa za kutisha kuhusu ukatili unaofanyika shuleni. Imeelezwa kuwa zaidi ya nusu ya wavulana na wasichana wamefanyiwa vitendo vya ukatili na waalimu wao.
Takwimu zinaonesha kuwa katika kila wasichana kumi, kuna msichana mmoja aliyenyanyaswa kijinsia na mwalimu wake. Hali hii haifai haifai, haifai kabisa; tusiivumilie hata kidogo.
Tanzania ina maendeleo mengi ya kujivunia hususan upande wa kutoa elimu, hasa kwa wasichana. Na ninafurahi kwamba katika uzinduzi wa taarifa hii muhimu tunayo timu nzima hapa ya viongozi wa serikali akiwemo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dokta Shukuru Kawambwa.
Lakini haitoshi tu kuwapeleka watoto shule; lazima tuhakikishe kuwa huko shuleni kuna mazingira salama, yanayomwezesha mwanafunzi kuelekeza nguvu zake katika masomo na sio kuhangaikia usalama wake.
Uchunguzi huu umeonesha kuwa watoto waliofanyiwa ukatili nao huwa wakatili wanapokuwa watu wazima. Kwa maana hiyo tusipoweza kuzuia ukatili kwa watoto wa leo basi tunaendeleza ukatili katika vizazi vijavyo.
Ukatili ni kama ugonjwa. Tukipuuza ukatili unaofanyiwa watoto wetu, ukatili huo utaenea na kusambaa, na mwishowe utazoeleka na kuonekana kama kitu cha kawaida katika jamii.
Aidha ukweli mwingine uliojitokeza katika utafiti huu ni kuwa mara nyingi watoto wanafanyiwa ukatili na ndugu na jamaa wa karibu ambao ndiyo walipaswa kuwa walinzi wao.
Hii ni dosari kubwa katika jamii. Ni lazima ulinzi na usalama wa watoto uwe ni wajibu wa jamii nzima. Hatuna budi kujenga jamii ambayo haivumilii, na inachukia vitendo vya ukatili kwa watoto.
Ni lazima tujenge jamii inayojipa jukumu la kukemea, kulaani na kuwaadhibu wale wote wanaotenda ukatili huo.
Ingawa ni muhimu kuwa na sera zinazolinda usalama na maslahi ya watoto, jambo kubwa zaidi ni kuleta mabadiliko katika fikra za watu. Watu waweze kuwa na mtazamo sahihi kuhusu suala hilo.
Na hapa napenda nitumie mfano ambao hata Mheshimiwa Sophia Simba ameuzungumzia. Kwa mfano, watu waweze kuelewa kwamba kumchapa mtoto kunabomoa zaidi ari yake kuliko kujenga nidhamu yake.
Na nafurahi kwamba serikali inaangalia upya adhabu ya viboko na kama nimewasikia vizuri waheshimiwa mawaziri hapa, adhabu hiyo ipo mbioni kufutwa. Utafiti umeonesha pia, watoto wanaotendewa vitendo vya ukatili na
udhalilishaji, mara nyingi hukaa kimya bila ya kutoa taarifa katika vyombo vinavyoweza kuwalinda, kwa hiyo hawanufaiki na huduma ambazo wanastahili kuzipata kutoka katika vyombo hivyo.
Hivyo basi ni lazima turejeshe imani ya watoto wetu katika vyombo hivyo. Tujenge mazingira ya kuwapa uhuru wa kujieleza wakijua kuwa watasikilizwa kwa faragha, taarifa zao zitaheshimiwa na watalindwa ipasavyo.
Vile vile ndugu zangu hatuna budi kuandaa mazingira yaliyo salama, yanayowasaidia watoto – na muhimu zaidi – yanayowapa watoto fursa ya kutoa taarifa za siri kuhusiana na ukatili.
Katika hili Polisi ni chombo kimojawapo muhimu. Ninafurahi kwamba Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema ametuma mwakilishi wake kuwa hapa na naona timu nyingine ya wanajeshi la Polisi wakiwa miongoni mwetu. Ninafurahi kufahamu kwamba Jeshi la Polisi Tanzania lipo mstari wa mbele katika mapambano haya. Nawapongeza Polisi kwa uwajibikaji huu na kwa kuhakikisha kuwa watoto wanapewa nafasi salama ya kueleza yaliyowasibu kwa ukweli na uwazi, bila woga wala haya, wakiamini kuwa watasikilizwa
kwa dhati.
Hali kadhalika tuhakikishe kwamba mahakama zetu zinawapunguzia watoto dhahama kwa kuweka utaratibu bora wa kusikiliza haraka mashauri yanayofikishwa kwao na watoto wenye ujasiri wa kujitokeza kutoa taarifa. Kwa mara nyingine napenda pia nitambue kuwapo kwa baadhi ya viongozi wa mahakama, nimemuona hapa mheshimiwa Jaji kwa hiyo tunatumaini kwamba ujumbe huu utakuwa umefika.
Wazazi, walezi na waalimu kwa upande wao wasisite kutoa taarifa kwenye vyombo vinavyohusika mara tu wanaposhuku kuwa mtoto fulani amefanyiwa ukatili au kunyanyaswa na mtu yeyote yule; awe mzazi wake, mwalimu wake, jirani au jamaa ili kuwanusuru na madhara zaidi.
Ninaipongeza tena Serikali ya Tanzania kwa kuanzisha huduma motomoto ya simu. Nimetaarifiwa kuwa tayari kuna namba imeshasajiliwa na kwamba itazinduliwa katika siku zijazo. Watoto kama hamna taarifa, mimi nimeambia kuna namba 116, namba ambayo imesajiliwa lakini bado haijaanza kutumika na hiyo ni hatua muhimu.
Hii ni huduma ya bure ya simu inayopatikana kwa saa 24 kwa ajili ya kutoa taarifa za unyanyasaji wa watoto. Tunaomba jeshi la polisi liharakishe
uzinduzi na matumizi ya huduma hii muhimu.
Huduma hii inatoa fursa kwa kila mwananchi kutoa taarifa pale anapoona au anaposhuku kuwa kuna mtoto amefanyiwa ukatili au kunyanyaswa . Basi hakuna sababu tena ya kukaa kimya!
Tukiitumia huduma hii ya simu kikamilifu tutaweza kuwanusuru watoto wengi. Ili kufanikisha matumizi ya huduma hii tunahitaji kuwa na fedha za kutosha na watendaji wa kutosha waliopata mafunzo stahiki.
Tunahitaji pia kuimarisha huduma nyingine zenye manufaa katika ulinzi na usalama wa watoto, kama vile huduma za ushauri na huduma zinazokidhi mahitaji mahsusi ya watoto na vijana.
Tayari Serikali imeshachukua hatua muhimu kwa kutunga na kupitisha Sheria ya Mtoto ambayo pia nafurahi kwamba Baraza la Watoto limeweza kufahamu kwamba sheria hii imepitishwa. Sasa yatupasa kuongeza juhudi.
Nimefurahi kwamba Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto – ambayo ni wizara ninayoienzi sana kwa kuwa niliisimamia kwa miaka mitano – ndiyo iliyoshika hatamu katika kutekeleza mpango-mkakati wa kitaifa.
Mpango huu wa miaka mitano wa Kuzuia na Kushughulikia Ukatili Kwa Watoto ni mwanzo madhubuti kabisa.
Tunapoungana na washirika wetu – washirika kama ninyi mlio hapa – tunaweza kwa pamoja kukomesha tatizo hili kwa watoto. Kila mshirika ana dhima yake. Vyombo vya habari vinaweza kuufahamisha umma.
Asasi za kidini zinaweza kuwajenga watu kimaadili. Asasi za Kiraia zinaweza
kuhamasisha jamii kuchukua hatua zinazostahiki.
Sisi sote tunaweza kutumia ushahidi ulio katika utafiti huu ili kujenga
mazingira salama kwa ajili ya watoto, na kusiwepo kamwe aina yoyote ya ukatili na utesaji.
Mabibi na mabwana, Mimi nikiwa Mtumishi wa Umoja wa Mataifa, na mwanasheria, na muhimu zaidi nikiwa mzazi, natambua kwamba si rahisi
kuleta mabadiliko mpaka kwanza tukubali kwamba lipo tatizo.
Kukiri kuwa kuna tatizo ni jambo gumu lakini Tanzania tayari imechukua hatua hiyo ngumu kwa kuanzisha utafiti huu na kusambaza matokeo yake.
Ninajivunia nchi yangu Tanzania kwa kuonesha uongozi wa kweli – kutambua kuwepo kwa tatizo na kusimama kidete kukabiliana na tatizo hilo sugu, na kuweka nia ya kulitokomeza kabisa.
Mwezi Juni tu mwaka huu, katika wilaya ya Hai, binti wa miaka 15 alipewa ulinzi. Kwa miaka mitatu tangu mama yake afariki, binti huyu maskini alikuwa akinajisiwa kwa nguvu na baba yake wa kambo.
Lakini aliweza kupata ulinzi shuleni kwa sababu alijitokeza mwalimu mwenye msimamo sahihi. Mwalimu huyo alimpeleka kituo cha polisi.
Shauri lake likashughulikiwa haraka. Na hatimaye binti aliweza kusema maneno yafuatayo, ninanukuu; “Nilijisikia salama mahakamani kwa kujua
kwamba baba yangu wa kambo hatanifanyia ukatili huo tena.” Baba huyu alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Binti huyo sasa yuko huru, anaendelea kuishi na mama yake mlezi anayemjali na kumpenda. Kisa hiki kinatuonesha nini? Pale amabapo vyombo husika vimesimama imara, Polisi, mahakama, shule kama ukatili huu umefanyika shule, wazazi na wanajamii wakiungana pamoja, kwanza tutaweza kuwaokoa watoto na madhila haya lakini pili tutaweza kughakikisha kuwa sheria inachukua mkondo wake.
Nilikisikia kisa hiki kutoka kwa watumishi wa UNICEF ambao wanafanya kazi ya kufundisha makundi mbali mbali hapa nchini na kwingineko duniani mbinu za kutoa ulinzi kwa watoto.
Katika wilaya hiyo hiyo ya Hai, UNICEF imesaidia kutoa mafunzo kwa zaidi ya askari polisi 40. Kwenye kituo cha polisi cha Boma Ng’ombe, kuna chumba maalumu – cha hifadhi salama –kwa ajili ya wanawake na watoto wanaofika
kutoa taarifa nyeti za kutendewa ukatili wa aina mbalimbali pamoja na za kunajisiwa.
Hiki ni kielelezo bora cha ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa na Serikali katika juhudi za kuwalinda watoto dhidi ya ukatili.
Ndiyo sababu tunazindua utafiti huu leo kwenu nyote wanajamii. Ujumbe wangu mkuu wa leo, ni kwamba, tunazo takwimu, tunazo tarakimu, hoja si tarakimu na takwimu nyingi nyingi, ingawa zina umuhimu wake. Bali hoja ni kwamba, tunayoyazungumza hapa ni madhila halisi yanayowasibu binadamu halisi kama mimi na wewe, imetokea kwamba binadamu hao ni watoto wetu, wanyonge.
Tusiruhusu hali hii ya unyonge kwa watoto wetu, kwa hakika haki zao na usalama wao ni wajibu wetu sisi sote.
Takwimu na taarifa ni muhimu katika kazi zetu, nimekwishasema hilo, lakini kazi yetu kubwa kabisa ni kuwalinda watoto wetu, jamii zetu, rafiki zetu na binadamu wenzetu. Tujue kwamba takwimu hizi zinabeba sura ya mtu
halisi sio takwimu kavu.
Tukishirikiana, na tukisimama pamoja, tunaweza kukomesha ukatili kwa watoto. Tunaweza kukomesha kabisa vitendoviovu. Na tunaweza kuwapa watoto wa Tanzania fursa ya kustawi na kuwa na mustakabali mzuri ambao ni haki yao ya kuzaliwa.
Baadhi ya Watoto wa Shule za Msingi mbalimbali wakiandamana katika sherehe za uzinduzi wa ripoti ya Utafiti na Mpango wa Kitaifa wa kushughulikia "Ukatili kwa Watoto" na mpango wa Udhibiti wa Taifa.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Taifa Dkt. Asha Rose Migiro na Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia na Watoto Mh. Sophia Simba wakizindua rasmi RIPOTI YA UTAFITI NA MPANGO WA KITAIFA WA KUSHUGHULIKIA "UKATILI KWA WATOTO" NA MPANGO WA UDHIBITI WA TAIFA.
Wadau na watu mbalimbali kutoka taasisi za Kimataifa na Kitaifa wakifuatilia kwa umakini kilele cha uzinduzi huo.
Mabalozi wawakilishi wa nchi mbalimbali nchini wakifuatilia uzinduzi wa ripoti hiyo.
No comments:
Post a Comment