Habari za Punde

*NHIF KUVISHIKIA KIDEDEA VITUO VYA AFYA

Mwandishi Wetu, Rolya

UONGOZI wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umeapa kuwachukulia hatua kali za kisheria, wamiliki wa vituo vya afya watakaobainika kukiuka masharti ya mikataba iliyoridhiwa kwa pamoja katika kuwahudumia wanachama wa Mfuko huo.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Meneja Mfawidhi wa Mfuko huo wa NHIF Kanda ya Ziwa, Dkt. Rose Ntundu, wakati akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara, ambapo pamoja na mambo mengine aliwasihi madiwani hao kujiunga na mfuko huo kwa faida zao.

Dkt. Rose alisema, NHIF imeanza kupokea malalamiko kutoka kwa wateja wake kunyanyasika ikiwa ni pamoja na kunyimwa huduma muhimu, punde wanapokwenda katika baadhi ya vituo kupata huduma hizo bure, na kwamba NHIF kamwe haitawavumilia watu hao, iwapo watabainika kwenda kinyume na masharti ya mikataba hiyo.

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja Mfawidhi huyo wa NHIF, vipo baadhi ya vituo vya afya vimekuwa vikilalamikiwa na wateja wa mfuko huo, jambo ambalo ni ukiukaji mkubwa wa mkataba ulioridhiwa pande zote hizo mbili.

"Nawaombeni sana waheshimiwa madiwani tupeni taarifa kwa vituo vinavyowanyanyasa katika kuwapa huduma, ili tuvichukulie hatua kali. Hatuwezi kukubali waende kinyume na taratibu tulizokubaliana wakati wa mikataba.

"Kutokana na hilo, nawaomba sana pia mjitokeze kwa wingi kujiunga na Mfuko huu wa Taifa wa Bima ya Afya, ili mnufaike kwa kupata matibabu bure pamoja na familia zenu,

Karibuni sana NHIF tuboreshe maisha yetu kwa pamoja", alisema Dk. Rose.

 Alisema hadi sasa, NHIF imefanikiwa kuingia mikataba kwa kusajili vituo vya afya 5,544 kote nchini, kwa ajili ya utoaji wa huduma bure kwa wanachama wa mfuko huo, na hiyo ni sawa na asilimia 88.9.

Alizitaja baadhi ya huduma zinazotolewa bure na mfuko huo kupitia vituo hivyo kuwa ni pamoja na gharama 137 ya vipimo, dawa aina mbali mbali 623 zikiwemo za kansa, wagonjwa waliobadilishiwa figo, magonjwa nyemelezi.

Nyingine ni upasuaji mkubwa na mdogo, miwani ya kusomea, matibabu yote ya macho, kinywa na meno, magongo ya kutembelea, vifaa vya kusaidia kusikia, fimbo za kutembelea kwa wasioona.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.