Habari za Punde

*PUSH OBSERVER YAPATA CEO MPYA

Joe Taylor, akizungumza wakati wa hafla fupi ya utambulisho wake.
Na Mwandishi wetu
KAMPUNI inayoongoza ya usimamizi wa vyombo vya habari katika nchi za Afrika Mashariki, Push Observer, imemtangaza gwiji wa sekta hiyo Duniani, Joe Taylor kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wake.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa Push Observer, Omari Salisbury, alisema kuwa hatua ya kumwajiri, Taylor, imetokana na historia yake nzuri katika sekta hiyo nchini Marekani na kampuni yao inataka mafanikio makubwa katika sekta hiyo katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.
Salisbury, alisema kuwa Taylor ambaye kwa sasa amekwisha anza kazi, alikuja nchini kwa mara ya kwanza mwezi Septemba na kuendesha ‘mafunzo maalum’ kwa wadau mbali mbali kwenye hotel ya Sea Cliff na kuwafumbua macho wadau wengi wa sekta hiyo.
Aidha alisema kuwa wanaamini kuwa ujio wake na kufanya kazi na kampuni hiyo kutawawezesha kupata maendeleo makubwa huku wakitoa huduma bora zaidi katika Nchi za Afrika Mashariki.
“Lengo ni kupata maendeleo makubwa katika sekta ya usimamizi wa habari, tumeamua kuajiri mtu bora kabisa kwa lengo la kutoa huduma bora, naamini wadau wetu wakiwemo waandishi wa habari watapata kile wanachokihitaji katika kazi zao,” alisema Salisbury.
Alisema kuwa Taylor ni kiongozi bora na amekuwa katika fani hiyo kwa miaka 30 nchini Marekani.
 
Kabla ya kujiunga na Push Observer, alikuwa ni mkurugenzi wa kampuni ya VMS na mwaka 2009, ambapo walifanikiwa kushinda tuzo ya mwaka ya Innovation (Innovation of the Year Award) na mwaka huo huo wakashinda tuzo ya Cost Saving Award.
Vilevile Talylor, amewahi kushika nyadhifa mbali mbali ikiwa ni pamoja na makamu wa Rais wa kampuni ya Broadcast Monitoring for Medalink na Rais wa Broadcast News Mid-America, Oklahoma.
Taylor alisema kuwa amefurahi kujiunga na Push Observer na kufanya kazi Tanzania na anaamini kuwa kampuni hiyo itafika mbali kwa kupata maendeleo makubwa.

 

 

 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.