Habari za Punde

*STARS KUTEMBELEA MAKUMBUSHO YA TAIFA

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ambayo hivi sasa iko kambini kujiandaa kwa mechi dhidi ya Chad, kesho (Novemba 5 mwaka huu) saa 5 asubuhi itatembelea Makumbusho ya Taifa.
Ziara yao ni ya kawaida, lakini pia kutakuwa na onyesho la Historia ya Soka Tanzania.
 
Wachezaji ambao tayari wapo kambini hoteli ya New Africa ni Juma Kaseja, Godfrey Taita, Shabani Nditi, Hussein Javu, Juma Jabu, Ramadhan Chombo, Shomari Kapombe, Nurdin Bakari, Nadir Haroub, Juma Nyoso, Erasto Nyoni, Mrisho Ngasa, Mwadini Ally na Aggrey Morris.
 
Idrisa Rajab wa Sofapaka ya Kenya tayari naye yuko kambini wakati wachezaji wengine kutoka nje wanatarajia kuwasili leo usiku. Wachezaji wa mwisho kutoka nje tunawatarajia kesho.
MORO UTD, SIMBA ZAINGIZA MIL 5.7
Mechi namba 86 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Moro United na Simba iliyochezwa Novemba 2 mwaka huu Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam imeingiza sh. 5,764,000.
Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 1,688 ambapo kiingilio kilikuwa sh. 10,000 kwa VIP na sh. 3,000 kwa majukwaa mengine. Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni asilimia 18 iliyolipwa ni sh. 879,254.
Gharama za awali kabla ya mchezo; kila klabu ilipata sh. 118,160 wakati Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata sh. 101,280 kutoka mfuko wa jichangie ambayo ni sh. 200 kwa kila tiketi.
Nauli ya ndani kwa waamuzi, kamishna na mtathimini wa waamuzi ni sh. 90,000. Posho ya kujikimu kwa kamishna ni sh. 40,000. Gharama ya tiketi ni sh. 1,230,000 wakati usafi na ulinzi ni sh. 500,000.
Baada ya gharama hizo za awali kila klabu ilipata sh. 907,424, gharama za mchezo sh. 302,475, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu- FDF (sh. 151,237), Uwanja sh. 302,475, DRFA (sh. 120,990) na Baraza la Michezo la Taifa- BMT (sh. 30,247).
Powered by Sorecson : Creation de site internet

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.