Habari za Punde

*UCHAGUZI WA VIONGOZI CECAFA

Uchaguzi wa viongozi wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) utafanyika Novemba 24 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
 
Mwenyekiti wa sasa Leodegar Tenga ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) anatetea nafasi yake. Mpinzani wa Tenga ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Djibouti, Fadoul Hussein.
 
Nafasi nne za Kamati ya Utendaji zinagombewa na watu wanane. Wagombea hao ni Abdiqani Saeed Arab wa Somalia, Tariq Atta Salih (Sudan), Justus Mugisha (Uganda), Tesfaye Gebreyesus (Eritrea), Hafidh Ali Tahir (Zanzibar), Sahilu Wolde (Ethiopia), Raoul Gisanura (Rwanda) na Abubakar Nkejimana (Burundi).
 
Nayo kozi ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa ajili ya waamuzi watakaochezesha mashindano ya CECAFA Tusker Challenge Cup itafanyika Novemba 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
Waamuzi walioteuliwa na CECAFA kuchezesha mashindano hayo ni Dennis Batte (Uganda), Bamlak Tessema (Ethiopia), Davis Omweno (Kenya), Wish Yabarow (Somalia), Israel Mujuni (Tanzania), Munyemana Hudu (Rwanda), Eric Gasinzigwa (Burundi) na Garvis Munyenziza (Rwanda).
 
Waamuzi wasaidizi ni Hassan Egueh (Djibouti), Clemence Erasmo (Tanzania), Idam Hamid (Sudan), Juma Ali Kombo (Zanzibar), Hamis Chang’walu (Tanzania), Yohanes Girmai (Eritrea), Brazan Mamati (Kenya), David Sagero (Kenya) na Mark Sonko (Uganda).
 
Pia waamuzi wote wa Tanzania wenye beji za FIFA nao watashiriki katika kozi hiyo.
 
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.