Habari za Punde

*WANAFUNZI WAMCHARAZA BAKOLA MWALIMU MKUU WAO NA KUMJERUHI

Na Francis Godwin, Iringa
WANAFUNZI watatu wa kidato cha pili wa shule ya Sekondari, Ikola Tarafa ya Karema, wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma ya kumshambulia na kumjeruhi Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, kwa kile kilichodaiwa  mwalimu huyo kukataa kushinikizwa na wanafunzi wa kidato cha nne wa shule ili kuvujisha mtihani wa kidato cha nne uliofanyika hivi karibuni shuleni hapo.

Akielezea tukio hilo, Kamanda wa polisi mkoani Rukwa, .Isuto Mantage, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa tano asubuhi wakati  wanafunzi hao wa kidato cha kwanza cha pili na cha tatu walipofanya vurugu hizo baada ya kuwafungia walimu wengine kwenye ofisi yao kisha kwenda kuvamia ofisi ya mkuu wa shuile hiyo Kateka Chipeta.

Mantage, alidai kuwa wanafunzi hao walifanikiwa kuwashawishi wanafunzi wenzao 260 na kwenda kuvamia ofisi ya mkuu wa shule na kuanza kumshambulia  kwa fimbo na mangumi kabla ya mwalimu huyo  kufanikiwa kuchomoka na kutimkia katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata kujisalimisha.
 
Aidha imedaiwa kuwa, kufuatia kipigo hicho ilibidi Mkuu huyo wa  shule kupelekwa  katika Zahanati ya Kijiji hicho ambako alitibiwa na baadaye kuruhusiwa baada ya kupata michubuko kwenye maeneo mbalimbali ya mwili.

Uchunguzi uliofanywa awali kuhusiana na tukio hilo, umebaini kuwa wanafunzi hao waliamua kufanya vurugu hizo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wenzao wa kidato cha nne juu ya kushindikana  kwa mpango wao wa kumshawishi mkuu wa shule hiyo kupokea fedha walizochanga ili amshawishi msimamizi wa mitihani ya kidato cha nne ili aweze  kuwavujishia mitihani hiyo.

“Hawa wanafunzi wanadaiwa kuwa walichanga fedha na kumpatia mkuu wa shule yao ili ampatie huyo msimamizi lakini Mkuu wa shule hiyo alikataa kufanya kitendo hicho cha uvunjaji wa sheria jambo ambalo liliwaudhi wanafunzi hao kiasi cha kulazimika kuwaeleza wenzao wa madarasa ya chini waliobaki shuleni hapo ambao walioamua kumwadhibu  mkuu wao wa shule.” Alisema Mantage.

Kufuatia uchunguzi wa habari hizi ulibaini kuwa pia wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa wakichangishwa fedha kwa ajili ya kuchangia gharama za kuwalipa posho Walimu wa kujitolea wanaofundisha shuleni hapo kutokana na shule hiyo nzima kuwa na Walimu wawili pekee.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.