Habari za Punde

*MZEE YUSUPH 'ALIZWA' MKOANI IRINGA AIBIWA VIATU AKIFANYA MAHOJIANO NA KITUO CHA REDIO

 Mzee Yusuph akiwa katika shoo yake ambapo aliwapagawisha mashabiki lukuki waliohudhuria shoo hiyo katika Manispaa ya Iringa jana usiku baada ya 'kulizwa' viatu vyake wakati akiwa katika mahijiano na Kituo fulani hivi cha redio cha mkoani Iringa kuhusu onyesho lake la mkoani humo.

Na Francis Godwin, Iringa

MKURUGENZI na muimba mahiri wa kundi la Taarab la Jahazi Modern Taarab, Mzee Yusuph, ameibiwa viatu vyake wakati akiwa katika mahojiano na kituo kimoja cha Radio mkoani Iringa kabla ya kuingia ukumbini kutoa burudani kwa wakazi wa Manispaa ya Iringa jana.
 Chanzo cha habari hizi kutoka eneo la tukio kilimdokeza mwandishi wa mtandao huu wa http://www.sufianimafoto.blogspot.com, kuwa mzee Yusuph aliingizwa mjini na kuachwa mdomo wazi kwa mshangao jana majira ya saa 12 za jioni wakati akiwa ndani ya studio za radio hiyo akifanyiwa mahojiano ya moja kwa moja kuhusu onyesho lake.
Aidha chanzo hicho kilisema kuwa wakati msanii huyo akiingia katika studi hizo kama ilivyo kawaida ya taratibu za Studio, alilazimika kuvua viatu vyake na kuviacha sehemu ya mapokezi ya kituo hicho cha radio kabla ya kuingia studio kufanya mahojiano  na baada ya kumaliza mahojiano na kutoka nje hakuweza kuviona viatu vyake jambo lililozua mshangao mkubwa na kutoamini kilichotokea ndani ya himaya ya Ofisi za Studio hiyo.
Baada ya kutafuta viatu hivyo bila mafanikio ilibidi aazimwe viatu na wenyeji wake ili aweze kutoka eneo hilo na kuelekea hotelini kwake kwa ajili ya kujiandaa kuelekea ukumbini kupagawisha mashabiki wake.
Jambo hilo limezua utata mkubwa juu ya wizi huo wa viatu ndani ya ofisi hizo huku baadhi ya wa watu wakimshuku mmoja kati ya watangazaji wa kituo hicho kuwa huenda ndiye akawa amefanya wizi huo huku baadhi yao wakidai yawezekana ni vibaka walifika katika kituo hicho na kuiba viatu hivyo na kutokomea.

Swali la kujiuliza ni "je kama ni vibaka kutoka nje ya ofisi hizo alipita wapi hadi kufika eneo hilo linalotunziwa viatu na kuchagua kiatu hicho tu cha msanii huyo" 
 Akizungumza baada ya kutoa burudani kwa wakazi wa mji wa Iringa ndani ya Ukumbi wa Highland mjini Iringa, Mzee Yusuph, alisema kuwa kamwe katika maisha yake hataweza kusahau tukio hilo la aibu ambalo limemkuta mjini Iringa ndani ya kituo hicho cha radio.
"Kwa kweli napenda kuwapongeza wadau wangu kwa kujitokeza kwa wingi na kuendelea kupenda kazi zangu, ila katika maisha yangu kamwe sitasahau mkoa wa Iringa na ni vigumu kuamini ila yametokea mwenzenu leo nimeibiwa viatu tena nikiwa sehemu nyeti sana ila ni siri yangu sitaki kutaja sehemu hiyo ila nimeibiwa viatu vyangu nilivyovipenda sana"alisema mzee Yusuph na kwenda kukaa katika kiti.
Kutokana na tukio hilo la kuibiwa viatu mzee Yusuph alichelewa kupanda jukwaani na kupanda majira ya saa 6.45 usiku huku akionekana ni mtu wa kulazimisha furaha japo huzuni ndio ilichukuwa nafasi kubwa katika show yake hiyo mjini Iringa.
Hata hivyo baadhi ya mashabiki wake waliomba kufanya zoezi la kuchangisha fedha ukumbini humo ili kununua viatu hivyo japo mpango huo haukuzaaa matunda kutokana na muda.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.