Habari za Punde

*CHALZ BABA KUTUA EXTRA BONGO ZUGA SAFARINI KUELEKEA MASHUJAA

  · Apewa donge nono na mshahara wa nguvu
· Masharti mazito yamkabili
Na Mwandishi Wetu, Jijini 
MWIMBAJI wa zamani wa bendi ya African Stars maarufu kwa mtindo wa Twanga Pepeta, Chalz Baba inasemekana tayari amesaini mkataba wa miaka miwili na bendi ya Mashujaa kwa kupata donge nono.
Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa mwimbaji huyo amepewa sh. Milioni 15 kwa mkupuo na atakuwa analipwa mshahara wa sh. 400,000 kila mwezi.
Mbali ya malipo hayo, pia Chalz atakuwa analipwa sh. 200,000 ya kodi ya nyumba na shs. 50,000 kwa kila wiki (jumla sh. 200,000 kwa mwezi) na kupokea jumla ya sh. 800,000 kwa mwezi.
Aidha uchunguzi umebaini kuwa mwimbaji huyo kwa sasa anazuga tu kama anatafuta bendi wakati tayari amemalizana na bendi hiyo ya Mashujaa huku ikisemekana kuwa anatarajiwa kutua Jukwaa la Extra Bongo ambapo atakaa kwa muda mchache kabla kutangazwa rasmi kujiunga na Mashujaa.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mwimbaji huyo atakuwa chini ya sheria kali (Mkataba) ya Mshujaa.
Moja ya masharti hayo ni kutakiwa kushiriki bila kukosa shughuli za bendi hiyo na kutakiwa kutopanda jukwaa la bendi yoyote hata kama bendi yake haitakuwa kazini isipokuwa kwa kibali cha maandishi kutoka kwa mkurugenzi mtendaji.
Pia mkataba huo umeonyesha kuwa endapo mwajiriwa atavunja mkataba huo, basi hatoruhusiwa kufanya kazi katika kampuni nyingine inayomiliki bendi Tanzania ila tu kwa kibali maalum cha maandishi kutoka kwa mwajiri kitakachotolewa na maombi ya mwajiriwa.
Mbali ya masharti hayo, pia mwanamuziki huyo anatakiwa kutotumia kazi za bendi yake katika sherehe au shughuli za aina yoyote bila ya ridhaa ya uongozi.
Wakizungumza na Mtandao huu wa www.sufianimafoto.blogspot.com, wadau wa karibu wa mwanamuziki huyo ambao hawakupenda kuandikwa majina yao hewani, walisema kuwa, Chalz, amejiengua katika kundi hilo la Twanga akiwa na nia ya kutua Bendi ya Mashujaa.
Aidha walisema kuwa Chalz  anatarajia kutua jukwaa la Bendi ya Extra Bongo ambapo atakuwa akipita tu huku akijiandaa kukamilisha safari yake ambayo itaishia Bendi ya Mashujaa.
Kwa kauli hiyo inaendana na kauli iliyotolewa siku za hivi karibuni na Mkurugenzi wa Bendi ya Extra Bongo, Ally Choki, aliyesema kuwa anatarajia kufanya usajiri wa nguvu na wa aina yake kwa kusajiri wanamuziki mahiri kutoka katika bendi mahiri za jijini ambazo ni mahasimu wake.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.