Habari za Punde

*LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA BARA INAINGIA RAUNDI YA 18 KESHO

Ligi Kuu ya Vodacom inaingia raundi ya 18 kesho (Februari 15 mwaka huu) kwa mechi nne zitakazochezwa viwanja vya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha, Azam Chamazi jijini Dar es Salaam, Mkwakwani jijini Tanga na Kaitaba mjini Bukoba.

Mwamuzi Israel Mujuni atazichezesha JKT Oljoro na Ruvu Shooting jijini Arusha, Azam na Villa Squad zitachezeshwa na Judith Gamba jijini Dar es Salaam, Oden Mbaga ndiye atapuliza filimbi kwenye mechi ya Coastal Union na JKT Ruvu jijini Tanga. Mjini Bukoba kutakuwa na mechi kati ya Kagera Sugar na Moro United.

Mechi nyingine ya raundi ya 18 itachezwa keshokutwa (Februari 16 mwaka huu) kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambapo Toto Africans itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar.

LIGI DARAJA LA KWANZA
Timu nane zinaingia viwanjani kesho (Februari 15 mwaka huu) kusaka pointi tatu katika mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambayo sasa iko katika mzunguko wa pili hatua ya makundi.

Kundi B ni kati ya Majimaji na Small Kids zitakazooneshana kazi Uwanja wa Majimaji mjini Songea wakati Mbeya City itaumana na Polisi Iringa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Mechi za Kundi C zitakuwa kati ya Polisi Morogoro na Polisi Tabora kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro huku 94 KJ ikiwa mwenyeji wa AFC katika Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.

Keshokutwa (Februari 16 mwaka huu) Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga utakuwa mwenyeji wa mechi ya Kundi A kati ya Mgambo Shooting na Polisi Dar es Salaam jijini Tanga. Februari 17 mwaka huu kwenye uwanja huo huo kutakuwa na mechi kati ya Transit Camp na Morani ya mkoani Manyara.

Mechi nyingine ya Kundi B itapigwa keshokutwa (Februari 16 mwaka huu) ikizikutanisha timu za Tanzania Prisons na JKT Mlale kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.