KLABU ya Zamalek ya Misri, imegoma kufanyika kazi ombi la timu ya Yanga ya Tanzania na kushikilia msimamo wake wa kutka timu hizo kucheza michezo yote miwili ukiwa ni ule utakaochezwa hapa nchini Februari 18 na ule wa marudiano unaotakiwa kuchezwa nchini Misri kati ya Machi 2 na 4.
Kwa mujibu wa ratiba ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), mechi hiyo ya marudiano ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, itapigwa wiki mbili baada ya ile ya kwanza itakayochezwa Februari 18, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Hivi karibuni uongozi wa Klabu ya Yanga uliandika barua kwa Caf, kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuomba kutokuwapo kwa mchezo wa marudiano unaotarajia kupigwa nchini Misri kutokana na vurugu zilizokuwa zikiendelea nchini humo na kuzua hofu ya usalama wa wachezaji na msafara mzima wa timu hiyo kwenda nchini humo.
Jumanne wiki hii, TFF lilituma ombi hilo Caf, ikitambua kuwa, uamuzi wa jambo hilo ungetegemea matakwa ya Zamalek, iwe kuchezwa mechi moja au pambano hilo kuhamishiwa nchi nyingine kwa sababu za kiusalama.
Yanga, wametaka mechi moja, wakisita kwenda Cairo, Misri kwa mechi ya marudiano, baada ya kutokea vurugu za mashabiki katika mechi ya Ligi Kuu kati ya Ahly na El Masry iliyopigwa kwenye Uwanja wa Port Said.
Kwa mujibu wa Kocha Msaidizi wa Zamalek, Ismail Youssef, bosi wake (Hassan Shehata), amekataa kucheza mechi moja na kama vipi, wapo tayari mechi hiyo ipigwe bila mashabiki nchini humo.
“Kocha (Hassan) Shehata amesisitiza kuwa, mechi ya marudiano dhidi ya Yanga, lazima ichezwe Misri, hata kama itakuwa bila mashabiki kwa sababu za kiusalama,” alisema kocha huyo msaidizi kupitia mtandao.
Zamalek, ambayo mwaka jana iliamriwa kucheza mechi mbili za nyumbani bila mashabiki, kutokana na vurugu za mashabiki wake.
Zamalek wametoa msimamo huo, huku Caf ikitarajia kujadili vurugu hizo kesho Jumamosi, kuangalia hatua za kuchukua dhidi ya waliohusika kwa namna moja au nyingine na maafa hayo makubwa zaidi katika soka ya Misri.
No comments:
Post a Comment