Machi 8 kila mwaka ni Siku ya Wanawake Dunia. Ili kuadhimisha siku hiyo kwa upande wa mpira wa miguu, TFF kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake (TWFA) imeandaa mashindano mafupi kwa shule nane za sekondari za Mkoa wa Dar es Salaam.
Mashindano yataanza Februari 24 mwaka huu kwenye viwanja viwili vya Jitegemee Sekondari ambapo kutakuwa na kundi B wakati kundi A litacheza mechi zake Makongo Sekondari. Mechi zitaanza saa 8 mchana na kumalizika saa 10 jioni.
Kundi A lina shule za Makongo, Goba, Twiga na Lord Barden wakati Jitegemee, Benjamin Mkapa, Kibasila na Tiravi zitakuwa kundi B.
Lengo la mashindano ni kuhamasisha mpira wa miguu kwa wasichana katika ngazi ya shule, kuandaa, kubaini na kuendeleza mafanikio yanayopatikana katika timu ya wanawake ya Taifa.
Pia kutoa fursa kwa watoto wa kike kusherehekea Siku ya Wanawake duniani kupitia mpira wa miguu, kutekeleza ushiriki wa TFF katika shughuli za kijamii na ni sehemu ya mchakato wa kuandaa mashindano ya ligi kwa wasichana.
Uchaguzi wa timu shiriki umezingatia mchango wa shule katika kuendeleza mpira wa miguu kwa wasichana/wanawake. Pia zawadi zitatolewa kwa mshindi wa kwanza, pili na tatu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano hayo ni Zainab Mbiro kutoka Twiga Sekondari wakati wajumbe ni Brighton Mbasha (Jitegemee), Yusuf Mohamed (Tiravi), Michael Bundala (TFF), Furaha Francis (TFF/TWFA) na Rose Kissiwa (TWFA).
Tunaomba wadau mbalimbali wajitokeze kusaidia gharama za uendeshaji wa mashindano hayo.
No comments:
Post a Comment