Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh (katikati) akiwa ameambatana na wenyeviti wa kamati za kudumu za bunge akiwasilisha taarifa ya ripoti tano za kaguzi maalum kuhusu Ukaguzi wa ufanisi na Thamani ya Fedha kwa waandishi wa habari leo mjini Dodoma.
Kaguzi hizo zimehusisha Ukaguzi maalum wa wilaya ya Kishapu, Usimamizi wa matengenezo ya magari ya serikali, Usambazaji wa maji mijini, ukaguzi wa mapato yatokanayo na uvunaji wa misitu na Mapato yanayokusanywa na wakala katika Halimashauri.
Baadhi ya watendaji wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wakifuatilia ripoti mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa na Mkaguzi Mkuu Bw. Ludovick Utouh mjini Dodoma. Picha na Aron Msigwa – MAELEZO
******************************************************************
Na Aron Msigwa –MAELEZO.
Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini ubadhirifu mkubwa wa fedha za serikali kiasi cha shilingi bilioni 7 kufuatia ukaguzi maalum uliofanyika katika Halmashauri ya wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Dodoma wakati wa kuwasilisha ripoti za matokeo ya kaguzi 5 za ufanisi/Thamani ya fedha Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Rudovick Utouh akiwa ameambatana na baadhi ya wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge amesema kuwa Ofisi yake imebaini matukio 14 yenye jumla shilingi bilioni 7 ambayo yana kila dalili za ubadhirifu wa fedha za umma.
Bw. Utouh amefafanua kuwa ofisi yake imebaini ubadhirifu huo kufuatia uhakiki wa kina na ukusanyaji wa ushahidi kuhusiana na hati za malipo zilizokosekana wakati wa ukaguzi uliopita wa mwaka wa fedha 2009/2010 na pia kufanya mahojiano na viongozi na wahasibu ambao wanahusika na utunzaji wa nyaraka za malipo ili kubaini ukweli kuhusiana na upotevu wa hati hizo za malipo.
Amesema wataalam wa ofisi yake katika kubaini ubadhirifu huo ilipitia hati zote za malipo sanjari na kuhakiki stakabadhi za malipo ili kujua uhalali wa malipo yaliyofanywa na Halmashauri bila kuidhinishwa na mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na kufanya mahojiano na viongozi mbalimbali wa Halmashauri hiyo ili kupata maoni yao.
Amebainisha kuwa ukaguzi huo maalum uliofanywa katika wilaya ya Kishapu ofisi yake iligundua mambo mbalimbali yaliyojitokeza yakiwemo udhaifu katika mifumo ya udhibiti wa ndani ,mabadiliko ya wakurugenzi watendaji wa Halmashauri kila baada ya muda mfupi,Mabadiliko ya mara kwa mara katika Idara ya fedha yakihusisha mweka Hazina, Udhaifu wa kitengo cha ndani cha ukaguzi kutokuwa na mkuu wa kitengo pamoja na mabadiliko katika Idara ya Mipango.
Mambo mengine ni pamoja na udhaifu katika idara mbalimbali za wilaya hiyo zikiwemo Ujenzi,Idara ya maji,kitengo cha Ugavi pamoja na udhaifu katika kitengo cha Uhasibu ambacho kiligundulika kuandika vocha na kulipa fedha taslimu bila idhini pamoja na kutumia makusanyo ya fedha kabla ya kupelekwa benki.
Pia amefafanua kuwa ofisi yake iligundua taarifa mbalimbali za kibenki zilizoghushiwa na kutumika zaidi ya shilingi milioni 200 na hundi zilizoghushiwa na kulipwa kiasi cha shilingi milioni 500 na uhamisho wa fedha toka akaunti moja kwenda nyingine bila idhini ya mkurugenzi na kutumika kinyume na malengo pamoja na uhamisho wa fedha kwenda kwenye akaunti zisizofahamika.
Bw. Utouh ameongeza kuwa kulikuwa na matumizi yaliyofanywa kinyume na malengo yaliyokusudiwa katika miradi ya maji,mfuko wa afya wa pamoja huku akifafanua kuwa ofisi yake imebaini kuwepo kwa ushirikiano kati ya watumishi wa Halmashauri na watumishi wa benki katika kufanikisha vitendo hivyo vya ubadhirifu wa fedha za halmashauri.
“Hali hii ya ushirikiano kati ya watumishi wa Halmashauri na benki umeonekana katika kaguzi zetu maalum tulizofanya huko nyuma kwenye Halmashauri za wilaya ya Kilosa na Rombo” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za serikali za mitaa Augustino Mrema ambaye pia ni mbunge wa Vunjo ameipongeza ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali kwa kubainisha ubadhirifu huo na kusisitiza kuwa kuwa matokeo hayo lazima yafanyiwe kazi na serikali.
“Naiomba serikali izifanyie kazi ripoti hizi ili ili matokeo yake yazae matunda na wahusika wote walioshiriki katika kufanya uharifu huu wakamatwe na kufikishwa mahakamani na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi” amesisitiza.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma Zitto Kabwe ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini ameipongeza ofisi ya CAG kwa kazi nzuri iliyofanyika na kuiomba ikamilishe ukaguzi wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).
No comments:
Post a Comment