Habari za Punde

*CCM YAMTEUA RASMI SIOI SUMARI KUWA MGOMBEA WA JIMBO LA ARUMERU MASHARIKI

BAADA ya Chama cha Mapinduzi CCM, kurudia zoezi la kupiga kura ili kumpata mwakilishi wake wa kuwania ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, hatimaye leo ametangazwa,  Sioi Sumari, kuwa ameteuliwa kuwa mgombea wake wa ubunge jimbo hilo baada ya kushinda kwa kishindo kwa mara ya pili katika uchaguzi,  mkoani Arusha.

Akitangaza hatua hiyo, jioni hii, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amesema uteuzi huo umefanywa na kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, katika kikao chake kilichofanyika leo mjini Dar es Salaam, chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete.

Nape alisema, imesema CCM ina uhakika Sioi ataipeperusha vyema bendera ya CCM kwenye uchaguzi huo na bila shaka CCM itaibuka na ushindi baada ya uchaguzi utakaofanyika Aprili mosi mwaka huu.

Alisema, wakati siku ya uzinduzi wa kampeni za CCM utapangwa na Kamati ya kampeni ya mkoa wa Arusha na wilaya ya Arumeru, Kamati Kuu imemteua Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kufungua kampeni hizo.

Nape alisema, wakati mfumo mzima wa kampeni kwa jumla utaratibiwa na mkoa husika, kitaifa kampeni hizo zitaratibiwa na Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha Mwigulu Nchemba ambaye ndiye alikuwa pia Mratibu wa Kampeni za CCM katika uchaguzi mdogo wa Igunga mkoani Tabora ambako CCM iliibuka na ushindi.

Uchaguzi mdogo jimbo la Arumeru Mashariki unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jeremiah Sumari ambaye ni baba mzazi wa mgombea wa CCM Sioi.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kampeni jimboni humo zitaanza rasmi tarehe tisa mwezi huu ambapo vyama vya CCM na CHADEMA vinatarajiwa kuonyeshana umahiri wao katika kampeni hivyo kwa kuwa ndivyo vyama pekee vinavyoonyesha kuwa na ushindani wa kutosha.

Sioi amefanikiwa kuteuliwa na Kamati Kuu ya CCM, baada ya kupita katika tanuru kali la mchakato wa kura za maoni jimboni kwake ambapo mara ya kwanza alishinda lakini uchaguzi ukalazimika kurudiwa kwa maagizo ya Kamati Kuu ya CCM baada ya yeye na mshindani wake wa karibu, Srakikya kupata kura zisizovuka asilimia 50 ya kura zote.

Uchaguzi wa marudio ulifanyika jana, kwa kuwapambanisha Sioi na Sarakikya tu, na hatimaye Sioi akaibuka mshindi kwa kura zilizozidi asilimia 50, hatua iliyofuatiwa na jina lake kupelekwa Kamati ya wilaya na mkoa wa mapendekezo kabla ya jina lake ktinga kamati kuu leo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.