NA MAGRETH KINABO – MAELEZO
WADAU wa mkutano wa Kongamano la Taifa la Usafiri wa Anga wamepewa changamoto ya kujadili jinsi kutafuta fedha kwa ajili ya kuendesha Shirika la Ndege la Taifa liweze kuwa na mtaji wa kutosha ili kuboresha huduma zake ziwe bora na endelevu katika kukuza uchumi wa nchi.
Kauli hiyo ilitolewa leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Usafiri wa Anga, Margaret Munyagi wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoa hutoba yake ya ufunguzi wa kongamano hilo la siku mbili linalofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Dares Salaam.
“Kongamano hili limehusisha wataalamu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ambao watatoa ushauri jinsi ya kurekebisha na kuboresha usafiri wa anga. Serikali haina mtaji wa kutosha za kuboresha shirika lake.
“Hivyo mkutano huu umehusisha wawekezaji,wafadhili na Benki ili tujadili Shirika la Ndege la Taifa litapataje mtaji ili uendeshaji wake uwe endelevu. Wataalamu hao ni wazoefu watatoa mawazo ili shirika hili liweza kufanya biashara ndani na nje ya nchi,” alisema Margaret.
Alisema mashirika ya ndege yaliyokuwepo hayatoshelezi kuuzia rasilimali nzilizopo nchini.
“Katika mkutano huu tutajadili serikali ikae pembeni au iwe na hisa katika shirika hili. Tutajadili suala hili ili kupata ufumbuzi,” alisisitiza huku akiongeza kuwa kwa sasa shirika hilo linaendeshwa kwa hisa za asilimia 100 kutoka serikalini.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa tangu shirika hilo lilipoanzishwa mwaka 1977 uendeshaji wake umekuwa upanda na kushuka.
Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu mkutano utajadili namna ya kupeleka mbele sekta hiyo katika kupanua viwanja vya ndege, vivutio na kuwa na ndege ya taifa iyakayopeperusgha bendera ndani na nje ya nchi.
“ Tunahitaji usafiri wa anga ambao utawezesha kuunganisha miji, majiji , Watanzania na nchi nyingine. Usafiri huu lazima uwe ni wenye gharama zitakazokidhi matakwa ya mpokeji na mtoaji huduma,” alisisitiza.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Shirikisho la Sekta Binafsi(TPSF), Esther Mkwizu alisema bila ya kuwepo usafiri wa anga unaotosheleza inakuwa ni vigumu kufanya biashara . Aliongeza kuwa sekta hiyo iko tayari kuwekeza ili kukuza uchumi wa nchi.
Kongamano hilo, limeshirikisha wataalamu 150 kutoka Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga(ICAO), kanda ya Afrika Mashariki, Chama cha Kimataifa cha Mashirika ya Usafiri wa Anga(IATA), mabalozi, wabunge na benki mbalimbali ikiwemo Benki ya Dunia.
No comments:
Post a Comment