JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
BUNGE LA TANZANIA
|
||
Simu: +255 022 2112065-7
Fax No. +255 022 2112538
E-mail: tanzparl@parliament.go.tz
(Barua zote za kiofisi ziandikwe
kwa KATIBU
WA BUNGE)
|
|
Ofisi ya Bunge,
S.L.P. 9133,
DAR ES SALAAM.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
YAH: MKUTANO
WA SABA WA BUNGE UNAOTARAJIA KUANZA TAREHE10 APRILI, 2012 NA KUMALIZIKA TAREHE
21 APRILI, 2012.
Ofisi
ya Bunge inapenda kuwatangazia wanahabari wote na wananchi kwa ujumla kuwa Mkutano wa Saba wa Bunge utaanza tarehe10
Aprili, 2012 na unatarajiwa kumalizika tarehe 21 Aprili, 2012. Orodha za
shughuli zinazotarajiwa kuwasilishwa katika Mkutano huo ni kama ifuatavyo:
- KIAPO CHA UTII KWA WABUNGE WAPYA:
Kwa mujibu wa masharti ya
Kanuni ya 24(1) ya Kanuni za Bunge, toleo la 2007 kutakuwa na Kiapo cha Utii
kwa Wabunge wapya wawili. Wabunge hao ni Mheshimiwa Cecilia Danieli Paresso
(Viti Maalum CHADEMA) aliyeteuliwa kujaza nafasi iliyoachwa wazi Kufuatia kifo
cha marehemu Regia Estalatus Mtema aliyefariki kwa ajali ya gari, na Mheshimiwa
Joshua Nassari (CHADEMA) aliyechaguliwa katika Uchaguzi mdogo wa Jimbo la
Arumeru Mashariki uliofanyika tarehe 1 Aprili, 2012 kufuatia kifo cha aliyekuwa
Mbunge wa Jimbo hilo marehemu Jeremiah Solomon Sumari (CCM).
- SHUGHULI ZA SERIKALI:
kwa Mujibu wa Kanuni ya 17
(1) (d) Toleo la 2007, Serikali ilikwishaziwasilisha kwa Katibu wa Bunge na shughuli
za Serikali Bungeni katika Mkutano Ujao na kuorodheshwa kwenye Kitabu cha
Shughuli za Bunge kama ifuatavyo:-
A.
MISWADA YA SHERIA YA
SERIKALI:
Miswada ya Sheria ya Serikali Minne(4) ambayo
ilishasomwa kwa mara ya kwanza katika Mikutano ya Bunge iliyopita itawasilishwa
Bungeni katika Mkutano ujao wa Bunge.. Miswada inayotarajiwa kusomwa kwa Mara ya Pili
na kuendelea na hatua zake zote ni hii ifuatayo:-
(Kusomwa kwa
Mara ya Pili na Hatua Zake Zote Kwa Mujibu wa Kanuni ya 86 ya Kanuni za Bunge):
i.
Muswada
wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania wa Mwaka 2011 [The Tanzania Livestock Research Institute
Act, 2011];
ii.
Muswada
wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wa Mwaka 2012 [The Social Security Laws (Amendments) Act,
2012 (No.2) Act, 2011];
iii.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho wa Sheria Mbalimbali
wa Mwaka 2011 [The Written Laws
(Miscellaneous Amendments) (No. 2) Act, 2011];
iv.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali
za Biashara wa Mwaka 2011. [The Business
Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2011].
B.
HOJA ZA
SERIKALI:
(i)
Bunge kukaa kama Kamati ya
Mipango:
Kwa Mujibu wa Kanuni ya 94, Bunge
litakaa kama Kamati ya Mipango ili kutekeleza matakwa ya Ibara ya 63(3)(c) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, kujadili na kuishauri
Serikali juu ya mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na
Serikali katika Mwaka wa Fedha 2012/2013.
(ii)
Taarifa ya Serikali ya
utekelezaji wa Maazimio ya Bunge:
Katika
Mkutano wa Tano wa Bunge Serikali ilipokea Mapendekezo yaliyotolewa na Kamati
Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati
na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha Bajeti Bungeni. Hivyo basi katika Mkutano huu Serikali itatoa Bungeni
Taarifa ya utekelezaji wa Maazimio hayo.
- SHUGHULI NYINGINE:
A. MASWALI:
(i) Maswali kwa Waziri Mkuu:
Kwa
mujibu wa masharti ya Kanuni ya 38, Waziri Mkuu anatarajiwa kuulizwa na Wabunge
maswali 16 ya msingi.
(ii) Maswali ya Kawaida:
Kwa mujibu wa Masharti ya Kanuni ya 39, Jumla ya
Maswali 125 ya kawaida yanatarajiwa kuulizwa na Wabunge na kujibiwa na Serikali
katika mkutano ujao wa Saba.
- TAARIFA ZA KAMATI ZA BUNGE:
Kwa mujibu wa Kanuni ya 114 (15), Kamati za Bunge
zitawasilisha Taarifa za kazi za Kamati kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha
2010/2011 na Taarifa hizo zitajadiliwa na Bunge kwa kadri itakavyoonekana
inafaa. Hivyo Taarifa hizo zitawasilishwa mezani tarehe 10 Aprili, 2012 ili
kutoa fursa kwa Wabunge kuzipitia kabla ya kuanza kuchangia Bungeni.
5. UCHAGUZI WA WABUNGE WA BUNGE LA JUMUIYA YA AFRIKA
MASHARIKI:
Kufuatia
kufika ukomo wa kipindi cha Ujumbe wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki na
kwa kuzingatia masharti ya Mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na
Kanuni za Bunge, katika Mkutano wa Saba wa Bunge kutakuwa na Uchaguzi wa
Wabunge Tisa watakao iwakilisha Tanzania katika Bunge hilo. Hivyo kwa mujibu wa
utaratibu uliowekwa, siku ya uteuzi itakuwa ni Jumanne tarehe 10/4/2012 saa
kumi jioni na Uchaguzi utafanyika siku ya Jumanne tarehe 17/4/2012.
6. HOJA BINAFSI ZA WABUNGE:
Kwa mujibu wa
Kanuni ya 54, Katibu wa Bunge amepokea makusudio mawili ya Wabunge kutaka
kuwasilishwa Hoja binafsi. Aidha, kwa mujibu wa fasili ya (1) na (2) ya Kanuni
ya 55 Wabunge hao wameshaandikiwa barua ya kuwataka wawasilishe Taarifa za Hoja
zao kwa Katibu wa Bunge. Endapo hoja hizo zitakidhi matakwa ya Kanuni za Bunge
zitatengewa muda wa kuwasilishwa Bungeni katika Kikao kijacho cha Saba.
- MAMBO MENGINE:
- SEMINA ZA WABUNGE WOTE:
Ofisi
ya Bunge imepokea maombi mawili kutoka Taasisi mbili za Umma ya kufanya Semina
kwa Wabunge katika Mkutano wa Saba wa Bunge. Semina hizo ni kama ifuatavyo:-
i. Semina kwa
Wabunge wote kuhusu Anuani Mpya za Makazi na Simbo za Posta pamoja na
Mabadiliko ya Teknolojia ya Utangazaji kutoka Analojia kwenda Dijitali;
ii. Semina kwa
Wabunge wote kuhusu Sensa ya Watu na Makazi.
Imetolewa
na
Idara
ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa
Ofisi
ya Bunge
Dar
es Salaam
7 Aprili, 2012
No comments:
Post a Comment