TAARIFA KWA UMMA
Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe 4 Mei, 2012 alitangaza mabadiliko katika safu ya Baraza la Mawaziri. Katika uteuzi wa Mawaziri na Manaibu Waziri, Mheshimiwa Rais aliwateua Mawaziri wapya kutoka miongoni mwa Wabunge aliokuwa amewateua na kuwatangaza. Baada ya uteuzi huo, kumetolewa maoni kwamba hatua ya Mheshimiwa Rais kuwateua Wabunge Wapya ambao hawajaapishwa Bungeni kuwa Mawaziri ni kitendo cha uvunjaji wa Katiba.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inayachukulia maoni haya kama ni jambo lenye maslahi ya jamii na linalohitaji kufafanuliwa; kwa upande mmoja lakini pia, kutolewa kwa elimu ya Umma; kuhusu Mamlaka ya Rais ya uteuzi wa Wabunge.
Msingi wa Katiba tunaoanza nao ni maelekezo ya masharti yaliyomo kwenye Ibara ya 55(4) kwamba:
“Mawaziri na Naibu Mawaziri wote watateuliwa kutoka miongoni mwa Wabunge”
Pili, ni mamlaka ya Rais ya uteuzi wa Wabunge aliyopewa na masharti ya Ibara ya 66(1)(e) yenye aina ya Wabunge wasiozidi kumi watakaoteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizotajwa katika aya za (a) na (c) za ibara ya 67 na angalau Wabunge watano kati yao wakiwa Wanawake. Wabunge aliowateuwa Mheshimiwa Rais wanatokana na Ibara hii.
Tatu, baada ya hatua zote hizi ikumbukwe kwamba aliyeteuliwa au kuchaguliwa kuwa Mbunge anakuwa Mbunge ama baada ya kutangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi; au baada ya kuteuliwa na Tume ya Uchaguzi kwa wale Wabunge wa viti maalum au anapochaguliwa na Baraza la Wawakilishi au anapoteuliwa na Rais akitumia Mamlaka yake ya uteuzi yanayotokana na Ibara ya 66(1)(e). Hivyo Wabunge wanaohusika hawahitaji kuapishwa kwanza Bungeni ili wawe Wabunge. Kiapo cha Mbunge Bungeni kinamwezesha tu kushiriki katika shughuli za Bunge.
Katiba ya nchi haiweki kwa Rais masharti kwamba kabla ya kumteua Mbunge wa aina hiyo kuwa Waziri au Naibu Waziri Mbunge huyo awe ameapishwa Bungeni kwanza. Masharti mawili muhimu na ya kuzingatia ni kwamba mteule wa nafasi ya uwaziri au Naibu Waziri hatashika madaraka yake ila mpaka kwa mujibu wa Ibara ya 56 ya Katiba, awe ameapa kwanza mbele ya Rais kiapo cha uaminifu na pia kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi yake kitakachowekwa kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge. Sharti la pili, litahusu kiapo cha Uaminifu katika Bunge kabla Mbunge hajaanza kushiriki katika shughuli za Bunge kwa masharti ya Ibara ya 68 ya Katiba. Viapo hivyo havitegemeani na vinaweza kufanyika kwa nyakati tofauti.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inasisitiza kwamba Wabunge ambao hawajaapishwa ndani ya Bunge ni Wabunge na wanapoteuliwa kushika nafasi ya Uwaziri au Naibu Waziri ni halali kwa kuwa uteuzi huo haukiuki masharti yoyote ya Kikatiba au Sheria. Aidha, katika kutekeleza madaraka ya kazi ya Uwaziri au Naibu Waziri Mbunge atahitaji kiapo mbele ya Rais hata kama hajaapishwa Bungeni. Busara ya uandishi wa Katiba na Sheria imetambua kwamba kunaweza kukatokea uteuzi wa aina hiyo wakati Bunge limeahirishwa kama ilivyo sasa. Masharti ya Ibara ya 68 ya Katiba yatazingatiwa katika kikao cha Bunge kijacho.
Bila shaka ufafanuzi huu utaleta uelewa katika jambo hili na kuepusha mikangayiko isiyokuwa ya lazima.
Imetolewa na Jaji Frederick M. Werema (Mb)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
06 Mei, 2012
No comments:
Post a Comment