Mabao matatu ya zawadi ya penati kutoka kwa mwamuzi Hashim Abdallah yamesheheresha ubingwa wa Simba wa ligi kuu ya Tanzania Bara. Timu hiyo kutoka mitaa ya Uhuru na Msimbazi iliibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya watani wake wa jadi, Yanga ambao mashabiki wake walitabiri kipigo hicho kabla kutokana na migogoro isiyokwisha na kususia kuja kuona mechi hiyo kama ilivyo kawaida.
Pichani juu ni mshambuliaji wa Simba Emmanuel Okwi, akishangilia bao lake la kwanza aliloifungia timu yake katika kipindi cha kwanza Dakika ya 1 na sekunde 10 muda mchache tu baada ya mpira kuanza, bao ambalo lilidumu hadi zilipomalizika dakika 45 za kipindi cha kwanza huku Yanga wakionekana kutawala mchezo huo kipindi chote na kufufua matumaini kwa mashabiki wake ambao wengi walihisi bao la kwanza lilikuwa ni la bahati tu.
Kipindi cha Pili kilipoanza Dakika ya 53, Beki wa Yanga Shadrack Nsajigwa alimchezea vibaya Emanuel Okwi katika eneo la hatari na kusababisha penati iliyowekwa kimiani na Felix Sunzu.
Dakika ya 62, Emmanuel Okwi aliwatoka mabeki wa Yanga na kumchungulia Kipa wa Yanga, Said Mohamed, na kuandika bao la 3 na mnamo Dakika ya 66 Emmanuel Okwi kwa mara nyingine tena alichezewa vibaya eneo la hatari na Beki, Goy Taita na kusababisha penati iliyopigwa na kipa wa Simba Juma Kaseja. Dakika ya 70, Emmanuela Okwi tena aliwekwa chini na kuzaa penati iliyopigwa na Patrick Mafisango na kuandika bao la 5 ambalo lilidumu hadi mwisho wa mchezo.
Baada ya mchezo huo Simba walikabidhiwa Kombe na kutawazwa kuwa mshindi mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Msimu wa 2012.
MATOKEO YA MICHEZO MINGINE YA KUMALIZIA LIGI ILIYOCHEZWA LEO NI : - Coast Union ya Tanga 1 Toto African ya Mwanza 0
Villa Squard 2 Ruvu Shooting 1
Azam Fc 2 Kagera Sugar 1
Moro Utd 0 Mtibwa Sugar 1
Polisi Dodoma 0 JKT Oljoro 1
Huku matokeo ya Dar es Salaa yakiongoza ambapo Simba 5 Yanga 0
na kwa matokeo hayo sasa timu za Villa Squard, Polisi Dodoma na Moro United zitakuwa zimeshuka Daraja msimu huu.
Beki wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, akimdhibiti Emmanuel Okwi, wakati wa mchezo huo, uliochezwa jioni ya leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Costadic Papic, akiwa amekaa jukwaani na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Salum Rupia pamoja na mashabiki baada ya kuwa amesusia mchezo huo na kuiacha timu hiyo ikishuka dimbani na Kocha msaidizi.
Sehemu ya mashabiki wa Simba.
Sehemu ya mashabiki wa Yanga.
No comments:
Post a Comment