Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Seneta Christopher Coons (wa pili kushoto kwa Makamu) aliyeongozana na ujumbe wake kutoka nchini Marekani, wakati walipofika Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam leo, kwa mazungumzo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na Seneta Christopher Coons (wa pili kushoto) na ujumbe wake kutoka nchini Marekani, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu Ikulu Dar es Salaam leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiagana na Seneta Christopher Coons, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu Ikulu Dar es Salaam leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,akizungumza jambo na Seneta Christopher Coons, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu Ikulu Dar es Salaam leo.
**********************************
DKT. BILAL AFANYA MAZUNGUMZO NA UJUMBE WA MAREKANI
Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo Ijumaa Juni Mosi, 2012 amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa watu saba kutoka Marekani ukiongozwa na Seneta kutoka Delaware Christopher Coons.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais alielezea kufurahishwa kwake na uhusiano mzuri ulipo kati ya Tanzania na Marekani na pia akafafanua kuwa Marekani imekuwa ni rafiki wa kweli kwa Tanzania kutokana na michango yake ya maendeleo iliyopo nchini.
Dk. Bilal aliueleza ujumbe huo uliomtembelea Ikulu leo kuwa, serikali ya Tanzania inaona faraja kushirikiana na Marekani na kueleza kuwa mchango wa Marekani kwa Tanzania ni mkubwa na Tanzania inakaribisha uhusiano zaidi hasa katika sekta za Kilimo na Nishati.
“Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Bibi Hillary Clinton alikuja hapa, akatupa matumaini ya kuondokana na tatizo la umeme. Tayari wapo wawekezaji wengi kutoka Marekani ambao wana nia ya kuwekeza katika nishati,” alisema Makamu wa Rais.
Kwa upande wake Seneta Coons alimueleza Makamu wa Rais kuwa, jimboni kwake Delaware wapo wakulima wengi ambao wangependa kuja nchini kuwekeza katika kilimo. Pia alifafanua namna Tanzania inavyoweza kuzalisha umeme wa ‘Geothermal’ kwa kushirikiana na wawekezaji kutoka Marekani.
Seneta Coons amewahi kuishi Afrika Mashariki katika miaka 25 iliyopita sambamba na mambo mengine ni seneta mwenye uwezo wa kuzungumza Kiswahili.
Seneta huyu anatokea katika eneo la uwakilishi ambalo pia anatokea Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden na amepata nafasi ya Useneta baada ya Biden kuachia kiti hicho.
Hata hivyo, Makamu wa Rais alisema pamoja na juhudi zote za kuhifadhi mazingira na viumbe hai bado Tanzania inakabiliwa na matatizo ya ujangiri, uvuvi haramu, magugu maji kufunika kabisa baadhi ya maziwa na mito.
Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu vurugu za hivi karibuni za Zanzibar Dkt. Bilal alisema haoni sababu yoyote ile kwa watu wanaohubiri kuwa hawataki Muungano kisha wakakimbilia kuchoma makanisa na kuvunja baa.
Alisema kuwa, kikundi hiki kimekuwepo siku nyingi na kinatumia kivuli cha dini katika kufanya siasa.
Vile vile Makamu wa Rais alieleza kuwa, Zanzibar ni kisiwa kidogo na kupitia Muungano wananchi wa Zanzibar wananufaika na kamwe serikali ya awamu ya nne haiwezi kuvumilia kuona watu wachache wenye agenda iliyojificha wakiharibu jambo bora kabisa lililofanyiwa kazi kwa zaidi ya miaka 48.
“Kila ukipita mikoani unakutana na Wazanzibar wanaishi. Kupitia Muungano tumefungua fursa nyingi. Sioni sababu ya watu kuibuka sasa kuupinga Muungano na tena kwa kufanya fujo. Tutaendelea kudhibiti hali hii na kuhakikisha kuwa amani inabakia katika nchi yetu,” alisema.
Dar es salaam
Ijumaa - Juni 1, 2012
No comments:
Post a Comment